012-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Kufanya ‘Ibaadah Kwa Wastani Ili Kuweza Kuidumisha

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 12  

 

  Kufanya ‘Ibaadah Kwa Wastani Ili Kuweza Kuidumisha

 

 

 

عَنْ عَائِشَةَ (رضي الله عنها)  أَنَّ النَّبِيَّ (صلى الله عليه و آله وسلم ( دَخَلَ عَلَيْهَا وَعِنْدَهَا امْرَأَةٌ قَالَ: ((مَنْ هَذِهِ؟)) قَالَتْ:  هذِهِ فُلاَنَةُ تَذْكُرُ مِنْ صَلاَتِهَا. قَالَ: ((مَهْ عَلَيْكُمْ بِمَا تُطِيقُونَ ، فَوَاللَّهِ لاَ يَمَلُّ اللَّهُ حَتَّى تَمَلُّوا ، وَكَانَ أَحَبَّ الدِّينِ إِلَيْهِ مَادَامَ عَلَيْهِ صَاحِبُهُ)) متفق عليه

Imepokelewa kutoka kwa ‘Aaishah (رضي الله عنها)  kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aliingia kwake akamkuta mwanamke mmoja. Akauliza: ((Nani huyu?)) Akasema: Huyu ni fulani. Na akamuelezea kuhusu wingi wa Swalaah zake. Akasema: ((Acha! fanyeni yale muwezayo! Kwani Wa-Allaahi, Allaah Hachoki [kulipa thawabu] mpaka mchoke wenyewe. Na ‘Ibaadah Aipendayo zaidi ni ile inayodumishwa na mtendaji)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

 

1. Uislamu haupendekezi wingi wa ‘Ibaadah wa kupita kiasi kwa khofu ya kuchoshwa nayo mtu akaiachilia mbali au kujikalifisha nayo.   Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:

 

طه ﴿١﴾

Twaahaa

مَا أَنزَلْنَا عَلَيْكَ الْقُرْآنَ لِتَشْقَىٰ ﴿٢﴾

Hatukukuteremshia Qur-aan ili upate mashaka. [Twaahaa (20: 1-2]

 

 

2. Ikiwa Allaah (سبحانه وتعالى) Hamkalifishi mtu, vipi mtu ajikalifishe nafsi yake? Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا

 

((Allaah Haikalifishi nafsi ila kwa wasaa [kadiri] iwezavyo)) [Al-Baqarah (2: 286)]

 

Na pia Anasema (سبحانه وتعالى):

لَا تُكَلَّفُ نَفْسٌ إِلَّا وُسْعَهَا

 

((Nafsi isijikalifishe ila kwa wasaa wake)) [Al-Baqarah (2: 233)]

 

 

3. Inapendekezwa kufanya wastani katika kufanya ‘Ibaadah ili mtu aweze kutimiza haki ya kila kitu.

 

Hadiyth: ((Na hakika Rabb wako Ana haki juu yako, na hakika mwili wako una haki juu yako, na hakika ahli wako ana haki juu yako…basi kipe kila kitu haki yake…)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

4. ‘Amali yenye thawabu zaidi ni ile inayodumishwa japokuwa ni kidogo.

 

 

5. Kufanya ‘Ibaadah kwa wastani kunapelekea zaidi kwenye utiifu wa ‘Ibaadah, umakini, ikhlaasw na kukubaliwa na Allaah (سبحانه وتعالى).

 

 

6. Kidogo kinachoendelea kinazidi kingi kinachokatika.

 

 

7. Kuagiziwa hivyo ni kuwa ‘Ibaadah ni nyingi na uwezo wa mja una mipaka. Kwa hiyo, mja ajiweke katika mipaka hiyo ambayo itamuwezesha yeye kufanya mengi.

 

 

 

 

Share