034-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Kuswali Wakati Wake, Kuwafanyia Wema Wazazi, na Kufanya Jihaad

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 34

Kuswali Wakati Wake, Kuwafanyia Wema Wazazi, na Kufanya Jihaad

Alhidaaya.com

 

 

 

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بن مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) قَالَ: سَأَلْتُ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: أَيُّ الْعَمَلِ أَحَبُّ إِلَى اللَّهِ؟ قَالَ: ((الصَّلاَةُ عَلَى وَقْتِهَا)) قَالَ: ثُمَّ أَيٌّ؟ قَالَ: ((ثُمَّ بِرُّ الْوَالِدَيْنِ)) قَالَ: ثُمَّ أَيٌّ؟  قَالَ: ((الْجِهَادُ فِي سَبِيلِ اللَّهِ)) متفق عليه

Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin Mas’uwd (رضي الله عنه)  ambaye amesema: Nilimuuliza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):  ‘amali gani inayopendeza zaidi kwa Allaah? Akasema: ((Swalaah kwa wakati wake)). Akasema: Kisha ipi? Akasema: ((Kisha kuwafanyia wema wazazi wawili)). Akasema: Kisha ipi? Akasema: ((Kufanya Jihaad katika Njia ya Allaah)).  [Al-Bukhaariy na Muslim.]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. ‘Amali zinatofuatiana kwa daraja, kwa maana kuwa nyinginezo zina thawabu zaidi ya nyingine.

 

 

2. Hima kubwa ya Maswahaba kupenda kujifunza mambo ya Dini yao, kwani walikuwa wakimuuliza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kila jambo wasilolijua.

 

 

3. Tabia njema ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na upole wake wa kuvumilia maswali kadhaa ya Maswahaba zake akiwajibu bila ya kuchoka.

 

 

4. Kuswali kwa wakati ni ‘amali bora kabisa kwa Allaah na ni amrisho katika Qur-aan.  Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

إِنَّ الصَّلَاةَ كَانَتْ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ كِتَابًا مَّوْقُوتًا ﴿١٠٣﴾

Hakika Swalaah kwa Waumini ni fardhi iliyowekwa nyakati maalumu. An-Nisaa (4: 103).

 

Rejea pia Hadiyth namba (49), (79).

 

 

5. Uislamu unahimiza kuwafanyia wema wazazi wawili. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا ۚ إِمَّا يَبْلُغَنَّ عِندَكَ الْكِبَرَ أَحَدُهُمَا أَوْ كِلَاهُمَا فَلَا تَقُل لَّهُمَا أُفٍّ وَلَا تَنْهَرْهُمَا وَقُل لَّهُمَا قَوْلًا كَرِيمًا ﴿٢٣﴾

 

Na Rabb wako Amehukumu kwamba: “Msiabudu isipokuwa Yeye Pekee na (Ameamrisha) kuwafanyia ihsaan wazazi wawili. Kama mmoja wao akifikia uzee naye yuko pamoja nawe, au wote wawili basi usiwaambie, Uff! Na wala usiwakemee; na waambie maneno ya heshima.

 

 وَاخْفِضْ لَهُمَا جَنَاحَ الذُّلِّ مِنَ الرَّحْمَةِ وَقُل رَّبِّ ارْحَمْهُمَا كَمَا رَبَّيَانِي صَغِيرًا

﴿٢٤﴾

Na wainamishie bawa la unyenyekevu kwa huruma, na useme: “Rabb wangu! Warehemu kama walivyonilea udogoni.” [Al-Israa (17: 22-23)]

 

 

Rejea pia: Al-Baqarah (2: 83), An-Nisaa (4: 36), Al-An’aam (6: 151), Al-‘Ankabuwt (29: 8), Luqmaan (31: 14)].

 

Rejea pia Hadiyth namba (125).

 

 

6. Kuwafanyia wema wazazi ina thawabu zaidi kuliko kufanya Jihaad katika njia ya Allaah kwa dalili ya Hadiyth: Abdullaah bin ‘Amr Al-‘Aasw (رضي الله عنهما) alisimulia: Mtu mmoja alimkabili Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akamwambia: Nitakubai juu ya Hijrah na kupigana jihaad katika njia ya Allaah nikitafuta ujira kutoka kwa Allaah. Akamuuliza: ((Je katika wazazi wako yuko aliye hai?)) Akajibu: Ndio, wote wako hai. Akamuuliza: ((Unatafuta ujira kutoka kwa Allaah?)) Akajibu: Ndio. Akamwamiba: ((Rudi kwa wazazi wako na uwafanyie wema)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

7. Kufanya jihaad katika njia ya Allaah ni mojawapo wa ‘amali kipenzi kwa Allaah (سبحانه وتعالى) na Allaah (سبحانه وتعالى) Amewaahidi wafanyao jihaad kuwakinga na adhabu na kupata mema ya Jannah   Anasema:

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا هَلْ أَدُلُّكُمْ عَلَىٰ تِجَارَةٍ تُنجِيكُم مِّنْ عَذَابٍ أَلِيمٍ﴿١٠﴾

Enyi walioamini! Nikujulisheni biashara itakayokuokoeni na adhabu iumizayo?

 

 

 

تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَتُجَاهِدُونَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ بِأَمْوَالِكُمْ وَأَنفُسِكُمْ ۚ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ﴿١١﴾

Mumuamini Allaah na Rasuli Wake, na mfanye jihaad katika njia ya Allaah kwa mali zenu, na nafsi zenu. Hivyo ndiyo bora kwenu mkiwa mnajua.

 

 

يَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ وَيُدْخِلْكُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ وَمَسَاكِنَ طَيِّبَةً فِي جَنَّاتِ عَدْنٍ ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ﴿١٢﴾

 (Allaah) Atakughufurieni madhambi yenu, na Atakuingizeni Jannaat zipitazo chini yake mito na masikani mazuri katika Jannaat za kudumu milele. Huko ndiko kufuzu adhimu.

 

وَأُخْرَىٰ تُحِبُّونَهَا ۖ نَصْرٌ مِّنَ اللَّـهِ وَفَتْحٌ قَرِيبٌ ۗ وَبَشِّرِ الْمُؤْمِنِينَ﴿١٣﴾

Na jengine mlipendalo; nusura kutoka kwa Allaah na ushindi wa karibu. Na wabashirie Waumini. [Asw-Swaff 61: 10-13]

 

Fadhia nyenginezo mbali mbali zimetajwa za kufanya jihaad. Rejea: Al-Maaidah (5: 35), Al-Anfaal (8: 74), Al-Baqarah (2: 218), An-Nisaa (4: 95), Al-‘Ankabuwt (29: 69), Al-Hujuraat (49: 15).

 

 

 

8. Mwanafunzi anatakiwa amuulize maswali mwalimu wake ambayo yatamsaidia katika dunia na Aakhirah yake.

 

 

9. Mwanafunzi anapaswa awe na adabu nzuri kwa mwalimu wake wala asitoke katika nidhamu hiyo ya adabu na haki za mwalimu na mwanafunzi kwa Mwalimu.

 

 

 

Share