035-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Starehe Bora Kabisa Ya Dunia Ni Mke Mwema
Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 35
Starehe Bora Kabisa Ya Dunia Ni Mke Mwema
عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عَمْرٍو بْنِ الْعَاص (رضي الله عنهما) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((الدُّنْيَا مَتَاعٌ وَخَيْرُ مَتَاعِ الدُّنْيَا الْمَرْأَةُ الصَّالِحَة)) مسلم
Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amr bin Al-‘Aasw (رضي الله عنهما) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Dunia ni starehe, na bora ya starehe zake ni mke mwema)) [Muslim]
Mafunzo Na Mwongozo :
1. Umuhimu wa kuchagua mke mwema, mwenye taqwa.
Rejea: Hadiyth namba (40).
2. Sababu mojawapo ya furaha ya dunia na Aakhirah ni kuwa na mke mwema, mwenye taqwa.
3. Fadhila za mwanamke mwema mwenye taqwa kufananishwa na starehe na pambo la dunia. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
زُيِّنَ لِلنَّاسِ حُبُّ الشَّهَوَاتِ مِنَ النِّسَاءِ وَالْبَنِينَ وَالْقَنَاطِيرِ الْمُقَنطَرَةِ مِنَ الذَّهَبِ وَالْفِضَّةِ وَالْخَيْلِ الْمُسَوَّمَةِ وَالْأَنْعَامِ وَالْحَرْثِ ۗ ذَٰلِكَ مَتَاعُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَاللَّـهُ عِندَهُ حُسْنُ الْمَآبِ ﴿ ١٤﴾
Watu wamepambiwa huba ya matamanio miongoni mwa wanawake, na watoto, na mirundi ya mali iliyorundikwa ya dhahabu na fedha na farasi wenye chapa ya aina bora na wanyama wa mifugo na mashamba. Hayo ni starehe za uhai wa dunia, na Allaah Kwake kuna marejeo mazuri. [Aal-‘Imraan (3: 14)]
4. Wema na taqwa ni miongoni mwa sifa njema anazopasa mwanamke wa Kiislamu kumiliki.
Rejea At-Tahriym (66: 11-12)
5. Mume anayeruzukiwa mke mwema ni neema kwake. Inampasa ailinde neema kwa kuishi naye vyema na kuwa na huruma naye na mapenzi ili apate kudiriki starehe za dunia na Aakhirah.
Rejea: Ar-Ruwm (30: 21), An-Nuwr (24: 26).
Na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ameusia waume kuwatendea wema wanawake zao katika Hadiyth kadhaa miongoni mwazo ni:
Kauli yake Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):
((Nakuusieni kuwafanyia wema wanawake)) [Al-Bukhaariy na Muslim
Na pia:
((واتَّقُوا اللهَ في النِّساءِ، فإنهن عندكم عَوَانٌ))
((Mcheni Allaah kuhusu wanawake kwani wao ni wasaidizi wenu…)
Na pia amesema Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):
((Mbora wenu ni yule aliye mbora kwa familia yake na mimi ni mbora kabisa kwa familia yangu)) [At-Twabaraaniy]
Na amesema pia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):
أن تطعمها إذا طعمت وتكسوها إذا اكتسيت ولا تضرب الوجه ولا تقبّح ولا تهجر إلاّ في البيت
((Kumlisha unapokula, na kumvisha unapovaa, wala usimpige usoni na kumharibu na usimtusi (kwa matendo yake na maneno yake) wala usimhame kwenda nyumba nyingine (umhame kitanda tu)) [Abuu Daawuwd, Ibn Maajah na Ahmad]
Na amesema Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):
ارفق بالقوارير
((Wafanyieni wema vyombo vyenu (qawaariyra).” [Al-Bukhaariy]
Rejea pia Hadiyth namba (28), (29), (40).