043-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Wanaopendana Kwa Ajili Ya Allaah Watakuwa Chini Ya Kivuli Chake

Lu-ulu-un-Manthuwrun

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya   43 

Wanaopendana Kwa Ajili Ya Allaah Watakuwa Chini Ya Kivuli Chake

Alhidaaya.com

 

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((إِنَّ اللَّهَ يَقُولُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ: أَيْنَ الْمُتَحَابُّونَ بِجَلاَلِي الْيَوْمَ أُظِلُّهُمْ فِي ظِلِّي يَوْمَ لاَ ظِلَّ إِلاَّ ظِلِّي)) مسلم

 

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Hakika Allaah Atasema Siku ya Qiyaamah: Wako wapi wanaopendana kwa Utukufu Wangu? Leo Nitawaweka kivulini katika kivuli Changu, Siku ambayo hakuna kivuli isipokuwa kivuli Changu)). [Muslim]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Bishara kwa Waumini wanaopendana kwa ajili ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwamba watapata fadhila ya kuwekwa kivulini Siku ambayo hakuna kivuli isipokuwa kivuli cha Allaah (سبحانه وتعالى).

 

 

2. Fadhila ya kujumuishwa pamoja katika Ardhw Al-Mahshar (ardhi ya mkusanyiko) Siku ya Qiyaamah, kabla ya kuingia Jannah.

 

 

3. Kupenda kwa ajili ya Allaah (سبحانه وتعالى) ni jambo dogo mno kulingana na thawabu na fadhila zake.

 

 

4. Hadiyth hii ni tashjiy’ (himizo) kwa Waumini wanaopendana kwa ajili ya Allaah (سبحانه وتعالى) wazidi kutenda mema, waambatane katika    kuamrishana mema na kukatazana maovu, na kufanyiana kila aina ya wema. Na fadhila yao ni Rahma ya Allaah (سبحانه وتعالى) juu yao ya kivuli hicho, pamoja na mazuri walioandaliwa huko Jannah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 

 وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۚ يَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَيُطِيعُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ أُولَـٰئِكَ سَيَرْحَمُهُمُ اللَّـهُ ۗ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ﴿٧١﴾

Na Waumini wanaume na Waumini wanawake ni marafiki wandani wao kwa wao, wanaamrisha mema na wanakataza munkari na wanasimamisha Swalaah na wanatoa Zakaah na wanamtii Allaah na Rasuli Wake. Hao Allaah Atawarehemu. Hakika Allaah ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote. [At-Tawbah (9: 71)]

 

 

Hivyo ndivyo hali ilivyokuwa ya Maswahaba wao kwa wao na kwa kipenzi chao Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kama Anavyosema Allaah. [Rejea Al-Fat-h (48: 29)].

 

 

5. Kuna haja kubwa ya kupendana kwa ajili ya Allaah (سبحانه وتعالى) ili kupata kivuli Chake, kwani jua Siku hiyo litakuwa kali mno si kama jua la duniani, bali litakuwa karibu mno na utosi wa watu.

 

[Hadiyth: ((Watu saba Allaah  Atawafunika katika kivuli Chake, Siku ambayo hakutokuwa na kivuli ila kivuli Chake: Imaam muadilifu, kijana ambaye amekulia katika ‘Ibaadah ya Rabb wake, Mtu ambaye moyo wake umeambatana na Misikiti, watu wawili wanaopendana kwa ajili ya Allaah; wanakutana kwa ajili Yake na wanafarikiana kwa ajili Yake, mwanamme aliyetakwa na mwanamke mwenye hadhi na mrembo wa kuvutia akasema: "Mimi namkhofu Allaah!" Mtu aliyetoa Swadaqah yake akaificha hadi kwamba mkono wake wa kushoto usijue nini ulichotoa mkono wake wa kulia, na mtu aliyemdhukuru Allaah kwa siri macho yake yakatokwa machozi)) [Al-Bukhaariy, Muslim].

 

 

 

Share