055-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Matendo Ya Aliyeneemeshwa Na Aliye Na Shida Duniani Ndiyo Yenye Kuzingatiwa Aakhirah

Lu-ulu-un-Manthuwrun

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 55

Matendo Ya Aliyeneemeshwa Na Aliye Na Shida Duniani

Ndiyo Yenye Kuzingatiwa Aakhirah

Alhidaaya.com

 

 

عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ (رضي الله عنه)  قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((يُؤْتَى بِأَنْعَمِ أَهْلِ الدُّنْيَا مِنْ أَهْلِ النَّارِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ، فَيُصْبَغُ فِي النَّارِ صَبْغَةً ثُمَّ يُقَالُ: يَا ابْنَ آدَمَ! هَلْ رَأَيْتَ خَيْرًا قَطُّ؟ هَلْ مَرَّ بِكَ نَعِيمٌ قَطُّ؟ فَيَقُولُ لاَ وَاللَّهِ يَا رَبِّ! وَيُؤْتَى بِأَشَدِّ النَّاسِ بُؤْسًا فِي الدُّنْيَا مِنْ أَهْلِ الْجَنَّةِ، فَيُصْبَغُ صَبْغَةً فِي الْجَنَّةِ، فَيُقَالُ لَهُ: يَا ابْنَ آدَمَ! هَلْ رَأَيْتَ بُؤْسًا قَطُّ؟ هَلْ مَرَّ بِكَ شِدَّةٌ قَطُّ؟ فَيَقُولُ لاَ وَاللَّهِ يَا رَبِّ مَا مَرَّ بِي بُؤْسٌ قَطُّ ولاَ رَأَيْتُ شِدَّةً قَطُّ)) مسلم

 

Imepokelewa kutoka kwa Anas (رضي الله عنه) amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Siku ya Qiyaamah ataletwa mtu wa motoni katika watu wa dunia aliyeneemeshwa neema nyingi mno, ataingizwa motoni kidogo kisha atatolewa: Ataulizwa: Ee mwana Aadam!  Je, umeona kheri yoyote? Ushawahi kuneemeka aslan? Atajibu: Hapana Wa-Allaahi Rabb wangu! Na ataletwa mtu aliyekuwa ana shida mno duniani katika watu wa Jannah. Ataingizwa Jannah kidogo kisha atatolewa. Ataulizwa: Ee mwana Aadam! Je, umeona shida yoyote? Ushawahi kutaabika aslan? Atajibu: Hapana Wa-Allaahi Rabb wangu! Haikunipitia shida yoyote abadan, wala sikuona taabu yoyote abadan)). [Muslim]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

1. Bishara kwa Muumin masikini kuhusu neema za Jannah yenye kudumu.

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أُولَـٰئِكَ هُمْ خَيْرُ الْبَرِيَّةِ ﴿٧﴾

Hakika wale walioamini na wakatenda mema, hao ndio wema kabisa wa viumbe.

 

 

جَزَاؤُهُمْ عِندَ رَبِّهِمْ جَنَّاتُ عَدْنٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًاۖ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُۚ ذَٰلِكَ لِمَنْ خَشِيَ رَبَّهُ ﴿٨﴾

Jazaa yao iko kwa Rabb wao; Jannaat za kudumu milele zipitazo chini yake mito ni wenye kudumu humo abadi. Allaah Ataridhika nao, nao wataridhika Naye; hayo ni kwa yule anayemkhofu Rabb wake.  [Al-Bayyinah (98: 7-8)]

 

 

Rejea pia: Aal-‘Imraan (2: 14-15), At-Tawbah (9: 20-22) (72), Huwd (11: 108), Az-Zukhruf (43: 33-35).

 

 

2. Onyo kwa kafiri au muovu aliyetajiri kwamba Aakhirah kuna adhabu ya kudumu.

 

Rejea: An-Nahl (16: 117), Aal-‘Imraan (3: 197), Luqmaan (31: 23-24).

 

 

3. Aliye na shida, dhiki na taabu yoyote duniani, ni bishara kwake avute subira na atende mema apate starehe ya milele Aakhirah, kwani maisha ya dunia si lolote si chochote. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 وَمَا هَـٰذِهِ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلَّا لَهْوٌ وَلَعِبٌ ۚ وَإِنَّ الدَّارَ الْآخِرَةَ لَهِيَ الْحَيَوَانُ ۚ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ ﴿٦٤﴾

Na huu uhai wa dunia si chochote isipokuwa ni pumbao na mchezo; na hakika Nyumba ya Aakhirah bila shaka hiyo ndiyo yenye uhai wa kweli hasa (wa milele), lau wangelikuwa wanajua! [Al-‘Ankabuwt (29: 64)].

 

 

 4. Funzo kwa mtu muovu aliye na mali, utajiri, na ukwasi kwamba starehe yake na mali haitamfaa kitu au kumuokoa na moto. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

يَوْمَ لَا يَنفَعُ مَالٌ وَلَا بَنُونَ ﴿٨٨﴾

 “Siku hayatofaa mali wa watoto.

 

إِلَّا مَنْ أَتَى اللَّـهَ بِقَلْبٍ سَلِيمٍ ﴿٨٩﴾

 “Isipokuwa yule atakayemfikia Allaah na moyo uliosalimika. [Ash-Shu’araa (26: 88-89)].

 

 

Rejea pia: Aal-’Imraan (3: 91), Al-Maaidah (5: 36), Al-Kahf (18: 46).

 

 

5. Maisha ya dunia si lolote si chochote, bali ni starehe ya muda tu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

اعْلَمُوا أَنَّمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا لَعِبٌ وَلَهْوٌ وَزِينَةٌ وَتَفَاخُرٌ بَيْنَكُمْ وَتَكَاثُرٌ فِي الْأَمْوَالِ وَالْأَوْلَادِ ۖ كَمَثَلِ غَيْثٍ أَعْجَبَ الْكُفَّارَ نَبَاتُهُ ثُمَّ يَهِيجُ فَتَرَاهُ مُصْفَرًّا ثُمَّ يَكُونُ حُطَامًا ۖ وَفِي الْآخِرَةِ عَذَابٌ شَدِيدٌ وَمَغْفِرَةٌ مِّنَ اللَّـهِ وَرِضْوَانٌ ۚ وَمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلَّا مَتَاعُ الْغُرُورِ ﴿٢٠﴾

Jueni kwamba uhai wa dunia ni mchezo na pumbao na mapambo, na kufakharishana baina yenu na kushindana kukithiri katika mali na watoto; ni kama mfano wa mvua inayowafurahisha wakulima mimea yake, kisha yananyweya, basi utayaona yamepiga manjano, kisha yanakuwa mabua yaliyonyauka na kupondekapondeka.  Na Aakhirah kuna adhabu kali, na maghfirah kutoka kwa Allaah na radhi. Na uhai wa dunia si chochote isipokuwa ni sterehe fupi za kughuri. [Al-Hadiyd (57: 20)]

 

Rejea pia: Aal-‘Imraan (3: 185), Ar-Ra’d (13: 26)].

 

 

6. Muumin ajitahidi kuchuma mema apate Jannah ya Neema na raha tupu.

 

 

7. Umasikini na utajiri duniani ni mtihani tu kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى), hivyo mwana Aadam asidanganyike na maisha yake.

 

 

Share