068-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Kuona Hayaa; Kusitahi Ni Katika Iymaan

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake) 

Hadiyth Ya 68

Kuona Hayaa; Kusitahi Ni Katika Iymaan

Alhidaaya.com

 

 

 

عَنْ ابن عُمر (رضي الله عنهما)  أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ مَرَّ عَلَى رَجُلٍ مِنْ الأَنْصَارِ وَهُوَ يَعِظُ أَخَاهُ فِي الْحَيَاءِ فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((دَعْهُ فَإِنَّ الْحَيَاءَ مِنْ الإيمَانِ)) متفق عليه

 

Imepokelewa kutoka kwa Ibn ‘Umar(رضي الله عنهما)   kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alipita kwa mtu miongoni mwa Answaar akimnasihi nduguye kuhusu kuacha kuona hayaa. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: ((Mwache, kwani hayaa ni katika iymaan)).  [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Neno lenyewe la ‘hayaa’ asili yake ni ‘hayaat’ yaani uhai. Na uhai wa mwana Aadam ima ni uhai wa kutenda mazuri au maovu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

مَنْ عَمِلَ صَالِحًا مِّن ذَكَرٍ أَوْ أُنثَىٰ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَلَنُحْيِيَنَّهُ حَيَاةً طَيِّبَةً ۖ وَلَنَجْزِيَنَّهُمْ أَجْرَهُم بِأَحْسَنِ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ﴿٩٧﴾

Mwenye kutenda mema miongoni mwa wanamume au wanawake naye ni Muumin, Tutamhuisha uhai mzuri, na bila shaka Tutawalipa ujira wao kwa mazuri zaidi ya yale waliyokuwa wakitenda.  [Al-Nahl (16: 97)]

 

 

2. Hayaa imeambatanishwa na iymaan, palipo na hayaa pana iymaan, na palipo na iymaan pana hayaa.

 

 

3. Kila mtu anapokuwa na hayaa zaidi, ndipo iymaan yake inapozidi, kwani anapotaka kufanya kitendo kiovu hukumbuka kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Anamuona japo Yeye hamuoni, na hivyo huona hayaa na huomba maghfirah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 وَالَّذِينَ إِذَا فَعَلُوا فَاحِشَةً أَوْ ظَلَمُوا أَنفُسَهُمْ ذَكَرُوا اللَّـهَ فَاسْتَغْفَرُوا لِذُنُوبِهِمْ وَمَن يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلَّا اللَّـهُ وَلَمْ يُصِرُّوا عَلَىٰ مَا فَعَلُوا وَهُمْ يَعْلَمُونَ ﴿١٣٥﴾

Na wale ambao wanapofanya machafu au wakajidhulumu nafsi zao (kwa maasi), humdhukuru Allaah wakaomba maghfirah kwa madhambi yao. Na nani anayeghufuria madhambi isipokuwa Allaah. Na hawaendelei katika waliyoyafanya na wao wanajua. [Aal-‘Imraan (3: 135)]

 

Hivyo basi, kutamzidishia mtu taqwa ya hali ya juu na kufikia daraja ya ihsaan.

 

Rejea Hadiyth namba 2 katika Aruba’iyn An-Nawawiy ya Jibriyl kuhusu Uislamu, Iymaan, Ihsaan].

 

4. Hayaa ni aina mbili: Inayohusu Dini na inayohusiana na watu, na baina yake kuna haya nzuri na mbaya.

 

Hayaa nzuri inayohusiana na Dini ni kuacha kutenda jambo linalochukiza mbele ya Allaah (سبحانه وتعالى) au limekatazwa na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

Hayaa mbaya inayohusiana na Dini, ni kuona aibu baada ya kufanya kitendo ambacho Allaah (سبحانه وتعالى) na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) wamekikataza.

 

Hayaa nzuri inayohusiana na watu ni kuacha kitendo kinachotia aibu kwa watu kama mke kutokumtolea ujeuri mumewe mbele za watu.

 

Na hayaa mbaya inayohusiana na watu ni kama vile mwanamke kuvaa mavazi yasiyositiri mwili wake na yasiyo ya heshima mbele ya watu.

 

5. Haya isiwe kisingizio cha kutokutenda mema.

 

 

 

 

 

Share