072-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Enezeni Salaam, Lisheni Chakula, Ungeni Undugu, Swalini Tahajjud, Mtaingia Jannah Kwa Amani

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 72

Enezeni Salaam, Lisheni Chakula, Ungeni Undugu, Swalini Tahajjud,

Mtaingia Jannah Kwa Amani

 

 

Alhidaaya.com

 

 

عَنْ أبِي يُوسُفَ عَبْدُ اللَّهِ بْنُ سَلاَمٍ (رضي الله عنه) قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ الله صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ  يَقُول: ((يَا أَيُّهَا النَّاسُ، أَفْشُوا السَّلاَمَ، وَأَطْعِمُوا الطَّعَامَ، وَصِلُوا الأَرْحَامَ، وَصَلُّوا وَالنَّاسُ نِيَامٌ،  تَدْخُلُوا الْجَنَّةَ بِسلاَمٍ)) رواه الترمذي وقال: حديث حسن صحيح

Imepokelewa kutoka kwa Abu Yuwsuf ‘Abdullah bin Salaam  (رضي الله عنه) amesema: “Nilimsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: ((Enyi watu! Enezeni [amkianeni kwa] Salaam! Na lisheni chakula, na ungeni undugu [na jamaa wa uhusiano wa damu], na swalini wakati watu wamelala, mtaingia Jannah kwa amani)). [At-Tirmidhiy na amesema: Hadiyth Hasan Swahiyh]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Maamkizi ya Kiislamu, kulisha watu, kuunga undugu na kuamka usiku kuswali, ni sababu mojawapo ya kumuingiza Muislamu Jannah, nayo ni mambo mepesi kabisa kuyatenda.

 

 

2. Amri, umuhimu na fadhila za kuamkiana kwa maamkizi ya Kiislamu.

 

Rejea:  An-Nisaa (4: 86), An-Nuwr (24: 27-28).

 

Na rejea pia Hadiyth namba (42).

 

Bonyeza Kiungo kifuatacho kwa faida ziyada:

 

Maamkizi Ya Kiislaam: Maamrisho Na Fadhila Zake

 

 

3. Sisitizo na himizo la kulisha maskini. Fadhila zake ni adhimu kama kuingizwa katika neema tele za Allaah (سبحانه وتعالى) huko Jannah.  Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

إِنَّ الْأَبْرَارَ يَشْرَبُونَ مِن كَأْسٍ كَانَ مِزَاجُهَا كَافُورًا﴿٥﴾

Hakika Waumini watendao wema kwa wingi watakunywa katika vikombe vya mvinyo mchanganyiko wake ni (kutoka chemchemu iitawayo) kaafuwraa.

 

 

عَيْنًا يَشْرَبُ بِهَا عِبَادُ اللَّـهِ يُفَجِّرُونَهَا تَفْجِيرًا﴿٦﴾

Chemchemu watakayokunywa humo waja wa Allaah, wataibubujua kwa wingi.

 

يُوفُونَ بِالنَّذْرِ وَيَخَافُونَ يَوْمًا كَانَ شَرُّهُ مُسْتَطِيرًا﴿٧﴾

Wanatimiza nadhiri na wanaiogopa siku ambayo shari yake ni yenye kuenea kwa upana.

 

وَيُطْعِمُونَ الطَّعَامَ عَلَىٰ حُبِّهِ مِسْكِينًا وَيَتِيمًا وَأَسِيرًا﴿٨﴾

Na wanalisha chakula, juu ya kukipenda kwake, masikini na mayatima na mateka.

 

إِنَّمَا نُطْعِمُكُمْ لِوَجْهِ اللَّـهِ لَا نُرِيدُ مِنكُمْ جَزَاءً وَلَا شُكُورًا﴿٩﴾

“Hakika sisi tunakulisheni kwa ajili ya Wajihi wa Allaah, hatukusudii kwenu jazaa na wala shukurani. [Al-Insaan (76: 5-9)]

 

 

Neema hizo za Jannah zimeendelea kutajwa kwa wingi katika Suwrah hiyo tukufu ya Al-Insaan mpaka Aayah namba 22.  

 

Kinyume cha kutokulisha masikini ilhali mtu ana uwezo au kutokuhimiza kulisha maskini ni matahadharisho na adhabu zilizotajwa katika:

 

 

Rejea: Al-Haaqah (69: 34), Al-Fajr (89: 18), Al-Maa’uwn (107: 3).

 

 

 

4. Maamrisho ya kuunga udugu na fadhila zake na maonyo ya kukata undugu.

 

Rejea: Al-Baqarah (2: 27), Ar-Ra’d (13: 21 – 25), Muhammad (47: 22-23).

 

Rejea pia Hadiyth namba (38).

 

 

 

5. Umuhimu wa Qiyaamul-Layl (Kisimamo cha kuswali usiku) kama tarawiyh na kuamka usiku kuswali. Fadhila zake ni adhimu, Anasema Allaah (سبحانه وتعالى): 

 

تَتَجَافَىٰ جُنُوبُهُمْ عَنِ الْمَضَاجِعِ يَدْعُونَ رَبَّهُمْ خَوْفًا وَطَمَعًا وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ ﴿١٦﴾

Mbavu zao zinatengana na vitanda, wanamuomba Rabb wao kwa khofu na matumaini, na katika yale Tuliyowaruzuku wanatoa.

 

فَلَا تَعْلَمُ نَفْسٌ مَّا أُخْفِيَ لَهُم مِّن قُرَّةِ أَعْيُنٍ جَزَاءً بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٧﴾

Basi nafsi yoyote haijui yaliyofichiwa katika yanayoburudisha macho. Ni jazaa kwa yale waliyokuwa wakiyatenda. [As-Sajdah (32: 16-17)]

 

Aayah hiyo inahusiana na Hadiyth ifuatayo ya Al-Qudsiy:

 

   

 عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ عَنْ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((قَالَ اللَّهُ تَبَارَكَ وَتَعَالَى: أَعْدَدْتُ لِعِبَادِي الصَّالِحِينَ مَا لَا عَيْنٌ رَأَتْ وَلَا أُذُنٌ سَمِعَتْ وَلَا خَطَرَ عَلَى قَلْبِ بَشَرٍ)) قَالَ أَبُو هُرَيْرَةَ اقْرَءُوا إِنْ شِئْتُمْ: (( فَلَا تَعْلَمُ نَفْسٌ مَا أُخْفِيَ لَهُمْ مِنْ قُرَّةِ أَعْيُنٍ)) البخاري، مسلم، الترمذي وابن ماجه

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه)  kwamba  Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  amesema: ((Allaah تبارك وتعالى Amesema: Nimewatayarishia waja Wangu wema kile ambacho jicho lolote halijapata kuona na sikio lolote halijapata kusikia na wala haijapata kupita katika moyo wa binaadamu)) Akasema Abuu Hurayrah: Kwa hivyo, soma ukitaka: Basi nafsi yoyote haijui yaliyofichiwa katika yanayoburudisha macho. Ni jazaa kwa yale waliyokuwa wakiyatenda)) [Al-Bukhaariy, Muslim, At-Tirmidhiy na Ibn Maajah]

 

Rejea pia: Adh-Dhaariyaat (51: 16-18).

 

 

6. Qiyaamul-Layl imetajwa kuwa ni Swalaah bora kabisa baada ya Swalaah fardhi kama alivyosema Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):

 

((أَفْضَلُ الصَّلاةِ بَعْدَ الْفَرِيضَةِ صَلاةُ اللَّيْلِ))  رواه مسلم.

((Swalaah iliyo bora kabisa baada ya fardhi ni Swalaah ya usiku)) [Muslim]

 

 

7. Kuamka kuswali usiku ni miongoni mwa sifa za Waja wa Ar-Rahmaan kama ilivyotajwa katika Al-Furqaan (25: 63-64).

 

 

 

8. Waamkao usiku kuswali hawako sawa na waja wengine. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

أَمَّنْ هُوَ قَانِتٌ آنَاءَ اللَّيْلِ سَاجِدًا وَقَائِمًا يَحْذَرُ الْآخِرَةَ وَيَرْجُو رَحْمَةَ رَبِّهِ ۗ قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الَّذِينَ يَعْلَمُونَ وَالَّذِينَ لَا يَعْلَمُونَ ۗ إِنَّمَا يَتَذَكَّرُ أُولُو الْأَلْبَابِ ﴿٩﴾

Je, yule aliye mtiifu nyakati za usiku akisujudu, au akisimama (kuswali), anatahadhari na Aakhirah na anataraji rahmah ya Rabb wake (ni sawa na aliyekinyume chake?). Sema: “Je, wanalingana sawa wale wanaouja na wale wasiojua?” Hakika wanakumbuka wenye akili tu. [Az-Zumar (39: 9)]

 

Rejea pia: Aal-‘Imraan (3: 113)  

 

 

9. Kuamka kuswali usiku ni amri za Allaah (سبحانه وتعالى) kwa Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) na kwetu pia.

 

 

Rejea: Qaaf (50: 39-40), Al-Insaan (76: 25-26), Al-Israa (17: 78-79), Al-Muzammil (73: 3-4).

 

 

 

 

Share