074-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Yapendeza Kupiga Chafya Na Yachukiza Kupiga Miayo
Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 74
Yapendeza Kupiga Chafya Na Yachukiza Kupiga Miayo
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أنَّ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((إِنَّ اللَّهَ يُحِبُّ الْعُطَاسَ وَيَكْرَهُ التَّثَاؤُبَ، فَإِذَا عَطَسَ أَحَدُكُمْ وَحَمِدَ اللَّهَ تَعَالى كَانَ حَقًّا عَلَى كُلِّ مُسْلِمٍ سَمِعَهُ أَنْ يَقُولَ لَهُ "يَرْحَمُكَ اللَّهُ" وَأَمَّا التَّثَاؤُبُ فَإِنَّمَا هُوَ مِنْ الشَّيْطَانِ فَإِذَا تَثَاءَبَ أَحَدُكُمْ فَلْيَرُدَّهُ مَا اسْتَطَاعَ، فَإِنَّ أَحَدَكُمْ إِذَا تَثَاءَبَ ضَحِكَ مِنْهُ الشَّيْطَانُ)) البخاري
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم ) amesema: ((Hakika Allaah Anapenda chafya na Anachukia kupiga miayo. Anapopiga chafya mmoja wenu akamhimidi Allaah (تعالى) ni wajibu kwa kila Muislamu anayemsikia kumwambia: “Yarhamuka Allaah” (Allaah Akurehemu). Ama kupiga miayo, hakika hivyo ni kutoka kwa shaytwaan, basi anapopiga miayo mmoja wenu ajizuie kadiri awezavyo. Mtu anaposema: “Aaawh” shaytwaan humcheka)). [Al-Bukhaariy]
Mafunzo Na Mwongozo:
1. Himizo la kufanya Anayoyapenda Allaah (سبحانه وتعالى) na kuacha Anayoyachukia.
2. Inapasa Kumuombea Rahma Muislamu anapopiga chafya baada ya kumhimidi Allaah (سبحانه وتعالى), kwani ni Sunnah na miongoni mwa haki baina ya Waislamu. Ameamrisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):
عن أبي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ قَالَ سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ: ((حَقُّ الْمُسْلِمِ عَلَى الْمُسْلِمِ خَمْسٌ: رَدُّ السَّلَامِ وَعِيَادَةُ الْمَرِيضِ وَاتِّبَاعُ الْجَنَائِزِ وَإِجَابَةُ الدَّعْوَةِ وَتَشْمِيتُ الْعَاطِسِ)) البخاري ومسلم
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba: Nimesikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: ((Haki ya Muislamu kwa nduguye Muislamu ni tano: Kujibu Salaam, kumtembelea mgonjwa, kulisindikiza jeneza, kuitikia mwito na kumuombea mwenye kupiga chafya)) [Al-Bukhaariy Muslim]
3. Mafunzo kwa Waislamu kuombeana du’aa za Sunnah katika kupiga chafya; du’aa ya anayepiga chafya na anayemsikia mwenziwe kama ifuatavyo:
Anapopiga chafya mtu aseme:
الْحَمْـدُ للهِ
AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah)
Kisha mwenzake amwambie:
يَرْحَمُـكَ الله
Yarhamuka-Allaah (Allaah Akurehemu)
Kisha naye amjibu:
يَهْـديكُـمُ اللهُ وَيُصْـلِحُ بالَـكُم
Yahdiykumu-Allaahu wa Yuswlihu baalakum (Allaah Akuhidi na Akutengenezee mambo yako [Hadiyth ya Abu Hurayrah (رضي الله عنه) katika Al-Bukhaariy (7/125)]
4. Kupiga chafya ni miongoni mwa neema za Allaah (سبحانه وتعالى) zisizohesabika, nayo ni inahusiana na afya ya mwana Aadam. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَآتَاكُم مِّن كُلِّ مَا سَأَلْتُمُوهُ ۚ وَإِن تَعُدُّوا نِعْمَتَ اللَّـهِ لَا تُحْصُوهَا ۗ إِنَّ الْإِنسَانَ لَظَلُومٌ كَفَّارٌ ﴿٣٤﴾
Na Akakupeni kila mnachomuomba. Na mkihesabu neema za Allaah hamtoweza kuziorodhesha hesabuni. Hakika insani ni mwingi wa dhulma, mwingi wa kukufuru akosaye shukurani. [Ibraahiym (14: 34)]
5. Inafaa kujihamasisha mtu apige chafya kwa kufanya mazoezi ya mwili ili abakie katika afya. Ama kuzuia kwenda miayo, ni kutokula hadi mtu ashibe mno akavimbiwa na akawa mvivu mno hadi apige miayo.
6. Masisitizo ya kuzuia mdomo mtu anapopiga miayo, nayo ina manufaa ya kiafya kwa bin Aadam kuzuia viini vya maradhi (vijidudu) kuingia mdomoni.
7. Uislamu unasisitiza afya na usalama bin Aadam.
8. Kujiepusha na kila jambo baya analopenda shaytwaan, na kuomba kujikinga naye. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَقُل رَّبِّ أَعُوذُ بِكَ مِنْ هَمَزَاتِ الشَّيَاطِينِ ﴿٩٧﴾
Na sema: “Rabb wangu! Najikinga Kwako kutokana na udokezi wa mashaytwaan,”
وَأَعُوذُ بِكَ رَبِّ أَن يَحْضُرُونِ ﴿٩٨﴾
“Na najikinga Kwako Rabb wasinihudhurie.” [Al-Muuminuwn (23: 97-98)]
Na pia kuomba kinga katika hali inayomkabili mtu inayopelekea wasiwasi na uchochezi wa shaytwaan, kama vile unapotaka kuanza kusoma Qur-aan au kuswali na kadhalika kama tulivofundishwa katika Qur-aan na Sunnah kwa kusema:
أَعـوذُ بِاللهِ مِنَ الشَّيْـطانِ الرَّجيـم
A’uwdhu biLLaahi minash-shaytwaanir-rajiym
Najikinga kwa Allaah kutokana na shaytwaan aliyeepushwa na kuwekwa mbali na Rehma za Allaah [Hadiyth ya Sulaymaan bin Swuradi -(رضي الله عنه) - Al-Bukhaariy (7/99) [6048], Muslim (4/2015) [2610]
9. Maagizo yote yanayotolewa na Allaah (سبحانه وتعالى) na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم ) ni kwa maslahi ya bin Aadam basi yasipuuzwe kabisa.