077-Lu-ulu-un-Manthuwrun: ‘Amali Zinakatika Isipokuwa Mambo Matatu: Swadaqah Inayoendelea, Elimu Inayonufaisha, Mwana Mwema

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 77

 

‘Amali Zinakatika Isipokuwa Mambo Matatu: Swadaqah Inayoendelea, Elimu Inayonufaisha, Mwana Mwema Anayemuombea Mzazi Wake

 

 

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَة (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((إِذَا مَاتَ ابْنُ آدَم انْقَطَعَ عَمَلُهُ إلاَّ مِنْ ثَلاَث: صَدَقَةٍ جَارِيَةٍ  أَوْ عِلْمٍ يُنْتَفَعُ بِهِ أَوْ وَلَدٍ صَالِحٍ يَدْعُو لَهُ)) مسلم

 

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Bin Aadam akifa, ‘amali zake hukatika isipokuwa mambo matatu: Swadaqah inayoendelea, au elimu inayonufaisha, au mtoto mwema anayemuombea du’aa)). [Muslim]

 

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Umuhimu wa kutenda mema yatakayomfaa mwana Aadam Aakhirah baada ya kufariki kwake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 

 يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَلْتَنظُرْ نَفْسٌ مَّا قَدَّمَتْ لِغَدٍ ۖ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ﴿١٨﴾

Enyi walioamini! Mcheni Allaah, na nafsi itazame imetanguliza nini kwa ajili ya kesho, na mcheni Allaah. Hakika Allaah ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika kwa yale myatendayo. [Al-Hashr (59: 18)]

 

Rejea pia: Yaasiyn (36: 12).

 

 

2. Mifano ya kutoa swadaqah fiy SabiliLLaah (Katika njia ya Allaah) ni kama kujenga Msikiti, kuchimba kisima, kujenga hospitali au kuwahudumia wagonjwa, kuacha shamba linalotoa mazao wakanufaika nayo watu, n.k.

 

 

3. Fadhila za kutoa swadaqah zimetajwa tele katika Qur-aan na Sunnah. Rejea Hadiyth namba (8), (31), (62),

 

 

4. Umuhimu wa kujifunza elimu ya Dini na kuifunza ili ibakie kunufaisha watu.

 

 

5. Fadhila za elimu nyingi zimetajwa katika Qur-aan na Sunnah. Mfano wa Hadiyth rejea Hadiyth namba (16), (78), (81).

 

 

6. Asiyekuwa na ‘ilmu anaweza kupata fadhila hizo kwa kujitolea mali yake kwa kujenga maraakiz za Sunnah na kuandaa madarasa, kusaidia katika da’wah kwa ujumla.

 

 

7. Umuhimu wa kulea watoto malezi mema ya Kiislamu ili watoke wana wema watakaomwombea mtu baada ya kufariki kwake.

 

Du’aa ya kuomba ili ajaaliwe mtu kuwa na kizazi chema mojawapo ni ambayo imetajwa katika sifa za ‘Ibaadur-Rahmaan (waja wa Mwingi wa Rahmah).

 

  رَبَّنَا هَبْ لَنَا مِنْ أَزْوَاجِنَا وَذُرِّيَّاتِنَا قُرَّةَ أَعْيُنٍ وَاجْعَلْنَا لِلْمُتَّقِينَ إِمَامًا ﴿٧٤﴾

 “Rabb wetu! Tutunukie katika wake zetu na dhuria wetu viburudisho vya macho yetu, na Tujaalie kuwa waongozi kwa wenye taqwa.  [Al-Furqaan (25: 74)]  

 

Nabiy Zakariyaa (عليه السلام) naye aliomba pia aliposema:

 

  رَبِّ هَبْ لِي مِن لَّدُنكَ ذُرِّيَّةً طَيِّبَةً ۖ إِنَّكَ سَمِيعُ الدُّعَاءِ ﴿٣٨﴾

 “Rabb wangu Nitunukie kutoka Kwako kizazi chema hakika Wewe ni Mwenye kusikia du’aa yangu.” [Aal-‘Imraan (3: 38)]

 

 

 

8. Hakuna atakayeweza kumfaa mwenziwe Siku ya Qiyaamah ila ‘amali zake tu alizozitenda.  Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَأَن لَّيْسَ لِلْإِنسَانِ إِلَّا مَا سَعَىٰ ﴿٣٩﴾

Na kwamba insani hatopata (jazaa) isipokuwa yale aliyoyafanyia juhudi.

 

وَأَنَّ سَعْيَهُ سَوْفَ يُرَىٰ ﴿٤٠﴾

Na kwamba juhudi yake itakuja kuonekana

 

ثُمَّ يُجْزَاهُ الْجَزَاءَ الْأَوْفَىٰ ﴿٤١﴾

Kisha atalipwa jazaa kamilifu. [An-Najm (53: 39-41)]

 

 

 

Zaidi yake ni du’aa ya mwana mwema.

 

 

9. Kila mtu afanye juhudi ya kufanya ‘amali njema kabla ya kumfikia mauti kwa sababu hakuna kitakachomfaa katika safari yake ndefu ya maisha ya Al-Barzakh na Aakhirah isipokuwa kwa yale aliyoyatenda.

 

Rejea Hadiyth namba (54).

 

Share