080- Lu-ulu-un-Manthuwrun:Allaah Anamnawirisha Anayesikia Ujumbe Akabalighisha

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 80

 

Allaah Anamnawirisha Anayesikia Ujumbe Akabalighisha

 

 

 

 

 عن إبْنِ مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) ِقَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ الله صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ: ((نَضَّرَ اللَّهُ امْرَأً سَمِعَ مِنَّا شَيْئًا فَبَلَّغَهُ كَمَا سَمِعَه، فَرُبَّ مُبَلِّغٍ أَوْعَى مِنْ سَامِعٍ)) وراوه الترمذي وقَالَ: حَدِيثٌ حَسَنٌ صَحِيحٌ  

 

Imepokelewa kutoka kwa bin Mas’uwd (رضي الله عنه)  ambaye amesema: Nilimsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: ((Allaah Amnawirishe mtu aliyesikia kitu kutoka kwetu naye akakibalighisha kama alivyosikia. Huenda anayefikishiwa akawa ana fahamu zaidi kuliko aliyesikia)). [At-Tirmidhiy na amesema Hadiyth Hasan Swahiyh]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Fadhila na himizo la kutafuta elimu.

 

Rejea Hadiyth namba (16), (76) (78).

 

 

2. Umuhimu wa da’wah (kulingania Dini) japo kwa Aayah moja.

 

Rejea Hadiyth namba (77).

 

 

3. Tahadharisho na ukumbusho wa jukumu la kubalighisha elimu sahihi kwani ni amaana. Pindi mtu akibalighisha yasiyo sahihi akapotosha watu atabeba dhambi zao juu ya dhambi zake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

لِيَحْمِلُوا أَوْزَارَهُمْ كَامِلَةً يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۙ وَمِنْ أَوْزَارِ الَّذِينَ يُضِلُّونَهُم بِغَيْرِ عِلْمٍ ۗ أَلَا سَاءَ مَا يَزِرُونَ﴿٢٥﴾

Ili wabebe mizigo (ya madhambi) yao kwa ukamilifu Siku ya Qiyaamah, na mizigo ya wale waliowapoteza bila ya kujua. Tanabahi!  Uovu ulioje wanayoyabeba. [An-Nahl (16: 25)]

 

Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَلَا تَقْفُ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ ۚ إِنَّ السَّمْعَ وَالْبَصَرَ وَالْفُؤَادَ كُلُّ أُولَـٰئِكَ كَانَ عَنْهُ مَسْئُولًا ﴿٣٦﴾

Na wala usifuatilie usiyo na elimu nayo. Hakika masikio na macho na moyo; vyote hivyo vitaulizwa. [Al-Israa (17: 36)]

 

 

Rejea pia: Yaasiyn (36: 16), Al-‘Ankabuwt (29: 13)].

 

Rejea pia Hadiyth namba (16).

 

 

4. Umuhimu wa kuhifadhi Qur-aan na Hadiyth ili Muislamu aweze kubalighisha kwa Ummah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

بَلْ هُوَ آيَاتٌ بَيِّنَاتٌ فِي صُدُورِ الَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ ۚ

 Bali hizo ni Aayaat bayana (zimehifadhika) katika vifua vya wale waliopewa elimu. [Al-‘Ankabuwt: 49]

        

 

 

5. Sikio ni kiungo muhimu kwa mwana Aadam kutokana na taathira yake ya kuingizwa iymaan baada ya kusikiliza Qur-aan na kauli za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), na ndio maana aghlabu katika Qur-aan utakuta Allaah (سبحانه وتعالى) Anatanguliza ‘kusikia’ kabla ya viungo vinginevyo. Mfano wa kauli Zake Allaah (سبحانه وتعالى) ni:

 

إِنَّا خَلَقْنَا الْإِنسَانَ مِن نُّطْفَةٍ أَمْشَاجٍ نَّبْتَلِيهِ فَجَعَلْنَاهُ سَمِيعًا بَصِيرًا﴿٢﴾

Hakika Sisi Tumemuumba insani kutokana na tone la manii iliyochanganyika ili Tumjaribu; Tukamjaalia mwenye kusikia na kuona.  [Al-Insaan (76: 2)]

 

Na Anasema pia Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَهُوَ الَّذِي أَنشَأَ لَكُمُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَالْأَفْئِدَةَ ۚ قَلِيلًا مَّا تَشْكُرُونَ ﴿٧٨﴾

Naye (Allaah) Ndiye Ambaye Aliyekuumbieni  kusikia na kuona na nyoyo. Ni machache mnayoshukuru. [Al-Muuminuwn: 23: 78)]

 

 

Na Anasema pia (سبحانه وتعالى):

 

وَلَقَدْ مَكَّنَّاهُمْ فِيمَا إِن مَّكَّنَّاكُمْ فِيهِ وَجَعَلْنَا لَهُمْ سَمْعًا وَأَبْصَارًا وَأَفْئِدَةً فَمَا أَغْنَىٰ عَنْهُمْ سَمْعُهُمْ وَلَا أَبْصَارُهُمْ وَلَا أَفْئِدَتُهُم مِّن شَيْءٍ إِذْ كَانُوا يَجْحَدُونَ بِآيَاتِ اللَّـهِ وَحَاقَ بِهِم مَّا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ﴿٢٦﴾

Na kwa yakini Tuliwamakinisha katika ambayo Hatukumakinisheni humo (nyinyi Maquraysh); na Tukawajaalia masikio na macho na nyoyo za kutafakari; lakini hayakuwafaa chochote masikio yao na wala macho yao na wala nyoyo zao za kutafakari walipokuwa wakikanusha kwa ujeuri Aayaat (hoja, ishara) za Allaah na yakawazunguka ambayo walikuwa wakiyafanyia istihzai. [Al-Ahqaaf (46: 26)]

 

Na pia Anasema (سبحانه وتعالى):

 

قُلْ مَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أَمَّن يَمْلِكُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَمَن يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ وَمَن يُدَبِّرُ الْأَمْرَ ۚ فَسَيَقُولُونَ اللَّـهُ ۚ فَقُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ﴿٣١﴾

Sema: “Nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini. Au nani anayemiliki kusikia na kuona; na nani anayemtoa aliye hai kutoka mfu, na anayemtoa mfu kutoka aliye uhai; na nani anayeendesha mambo (yote)?”  Watasema: “Ni Allaah”; basi sema: “Je basi hamuwi na taqwa?”   [Yuwnus (10: 31)]

 

Rejea pia:  An-Nahl (16: 78), Al-Mulk (67: 23), Huwd (11: 20), As-Sajdah (32: 9), Al-Israa (17: 36).

 

 

Na makafiri waliwakataza watu wasisikilize Qur-aan kwa sababu ilikuwa ikiwaathiri wengineo pindi wanapoisikiliza, na baadhi yao waliingia katika Uislamu kwa kusikia maneno ya Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لَا تَسْمَعُوا لِهَـٰذَا الْقُرْآنِ وَالْغَوْا فِيهِ لَعَلَّكُمْ تَغْلِبُونَ﴿٢٦﴾

Na wale waliokufuru wakasema: “Msiisikilize hii Qur-aan na ifanyieni rabsha huenda mkashinda.” [Fusw-Swilat 41: 26)]

 

 

Na ndio maana Allaah (سبحانه وتعالى) Akamuamrisha Rasuli Wake  (صلى الله عليه وآله وسلم) :

 

وَإِنْ أَحَدٌ مِّنَ الْمُشْرِكِينَ اسْتَجَارَكَ فَأَجِرْهُ حَتَّىٰ يَسْمَعَ كَلَامَ اللَّـهِ ثُمَّ أَبْلِغْهُ مَأْمَنَهُ ۚ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ قَوْمٌ لَّا يَعْلَمُونَ﴿٦﴾

Na ikiwa mmoja wa washirikina akikuomba umlinde, basi mlinde mpaka asikie Maneno ya Allaah (Qur-aan), kisha mfikishe mahali pake pa amani. Hivyo kwa kuwa wao ni watu wasiojua.  [At-Tawbah (9: 6)]

 

 

 

6. Athari ya sikio imewafanya Makafiri wajilaumu pale watakapoingizwa motoni kuwa laiti kama wangelisikiliza na kutia akilini. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَلِلَّذِينَ كَفَرُوا بِرَبِّهِمْ عَذَابُ جَهَنَّمَ ۖ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ﴿٦﴾

Na kwa wale waliomkufuru Rabb wao kuna adhabu ya Jahannam, na ubaya ulioje mahali pa kuishia. 

 

إِذَا أُلْقُوا فِيهَا سَمِعُوا لَهَا شَهِيقًا وَهِيَ تَفُورُ﴿٧﴾

Watakapotupwa humo, watausikia mkoromo wa pumzi wa kuchukiza nao unafoka.

 

تَكَادُ تَمَيَّزُ مِنَ الْغَيْظِ ۖ كُلَّمَا أُلْقِيَ فِيهَا فَوْجٌ سَأَلَهُمْ خَزَنَتُهَا أَلَمْ يَأْتِكُمْ نَذِيرٌ﴿٨﴾

Unakaribia kupasuka kwa ghadhabu. Kila wanapotupwa humo kundi, walinzi wake watawauliza: “Je, hajakufikieni mwonyaji yeyote?” 

 

 

قَالُوا بَلَىٰ قَدْ جَاءَنَا نَذِيرٌ فَكَذَّبْنَا وَقُلْنَا مَا نَزَّلَ اللَّـهُ مِن شَيْءٍ إِنْ أَنتُمْ إِلَّا فِي ضَلَالٍ كَبِيرٍ﴿٩﴾

Watasema: Ndio! Kwa yakini alitujia mwonyaji, lakini tulikadhibisha, na tukasema: “Allaah Hakuteremsha kitu chochote; nyinyi si chochote isipokuwa mumo katika upotofu mkubwa.”

 

وَقَالُوا لَوْ كُنَّا نَسْمَعُ أَوْ نَعْقِلُ مَا كُنَّا فِي أَصْحَابِ السَّعِيرِ﴿١٠﴾

Na watasema: “Lau tungelikuwa tunasikiliza au tunatia akilini, tusingelikuwa katika watu wa motoni.” 

 

فَاعْتَرَفُوا بِذَنبِهِمْ فَسُحْقًا لِّأَصْحَابِ السَّعِيرِ﴿١١﴾

Basi watakiri madhambi yao, na (wataambiwa): “Tokomeeni mbali watu wa motoni.”   [Al-Mulk 67: 6-11)]

 

 

 

7. Umuhimu wa kufikisha kwa wengine ambao hawakupata fursa ya kusikia kama vile Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alipokhutubia Maswahaba katika Hijjatul-Widaa’i (Hajj ya kuaga) akawaambia:

 

(( أَلا فَلْيُبَلِّغِ الشَّاهِدُ مِنْكُمُ الْغَائِبَ))

((…basi abalighishe (afikishe ujumbe) aliyekuweko shahidi hapa miongoni mwenu kwa asiyekuweko)) [Al-Bukhaariy]

 

 

 

8. Tofauti baina ya viumbe vya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa jinsi ambavyo mwenye kubalighishiwa huenda akawa na kipawa kizuri zaidi cha kufikisha kuliko aliyesikia mwanzoni akayafikisha kwa mwengine. Hata huenda mwanafunzi akaathirika zaidi na mafundisho baada ya kufikishiwa na mwalimu wake.

 

 

Share