Ndoa Inafaa Bila Ya Bi Harusi Kuweko?

SWALI:

 

Assalam aleikum warahmatullahi wabarakatu

Mimi naishi nchi za kikafiri na nimependana na kijana ambaye ni mwema mwenye dini na tunataka kuoana. Lakini mimi bado sikupata bado karatasi zangu za immigration ili nisafiri kwa hivyo nitashindwa kwenda nyumbani kufanya nikah. Nami sitaki kuchelewesha nikah kwa khofu ya kuingia katika dhambi ya zina. Maswali yangu ni haya:

Inawezekana kufanya nikah bila ya mimi kuhudhuria?  Na inawezekana uncle yangu awe walii wangu ikiwa wazazi hawataki?  Na ndoa huwa vipi bila ya biharusi? Inawezekana kuulizwa katika simu?

Je Alhidaaya inaweza kunisaidia katika jambo hili la muhimu maishani mwangu? Nakutgemeeni kuwa ndio suluhisho la mwisho kwangu munisaidie na namuomba Allah atuongoze katika njia iliyonyooka. Amin.

 


JIBU:

Sifa zote njema anastahiki Allah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'Anhum)  na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 Jazakillahu, dada kwa swali hili lako ambalo ni nyeti. Na swali hili lina vipengele vingi na nyeti katika jamii yetu. Japokuwa hujataja ni dada wa wapi tunaweza kubahatisha ya kwamba huenda ukawa ni kutoka Kenya, Tanzania au Uganda. Na lau tungejua unatoka wapi huenda tukawa tunaweza kukusaidia vyema zaidi.

Kama tulivyoelewa katika swali lako ni kuwa una elimu angalau kidogo ya Dini na hasa Fikihi ya ndoa. Ndoa haiswihi mpaka masharti kadhaa yawe yatatimizwa. Bila ya hivyo ndoa yenyewe inakuwa ni batili na baadhi ya vipengele umevitaja. Labda tunaweza kuekea muhtasari wake:

 

1.        Kuwe na walii.

2.        Ridhaa ya mume na mke mwenyewe.

3.        Mashahidi wawili waadilifu.

4.        Hotuba ya nikaha.

 

Sharti nambari mbili na mbili inaweza kupatikana kwani wewe uko tayari na mume yupo na hotuba inaweza kufanywa bila ya tatizo lolote. tatizo kubwa ni walii, kwani sheria imeweka mipango ya uwalii. Akiwepo baba hakuna anayeweza kuchukua nafasi yake hiyo, ikiwa hayupo ni babu upande wa baba (yaani babake baba yako), ikiwa hayupo basi kaka yako aliyebalighi na ikiwa hayupo anakuwa ami (paternal uncle). Uncle iliyotumika ina utata kwani anaweza kwa Kiswahili kuwa ni mjomba au ami, na mjomba hawezi kuwa walii wako.

Sasa ili kuweza kukusaidia tungependa kuuliza ni kwa nini   wazazi wako na wazazi wa atakayekuwa mume wako hawataki harusi hiyo iendelee? Je, huyo mvulana hana maadili mema? Je, ni kwa sababu ya kuwa yeye ni kutoka ukoo au kabila jengine? Je, ni kuwa hana kazi nzuri? Je, na je, na kadhalika. Ikiwa mvulana hana maadili mazuri basi kukataa kwao kupo katika sheria na ni vyema wewe ungojee mume mwengine. Ikiwa ana maadili mema na wazazi wako hawataki tu kwa sababu ambazo si za kisheria, kama kabila au ukoo tofauti na kadhalika jambo ambalo unaweza fanya ni kwenda kwa Qadhi ambaye atamwandikia barua baba aje ajieleze, na ikiwa hataweza kutoa sababu za kisheria, Qadhi huyo atakuwa walii wako na atakuozesha.

Lakini lengo la ndoa, si kukata kizazi bali kukiimarisha na kuunga ujamaa ambao Allah (Subhaanahu wa Ta'aala) na Mtume Wake (Swalla Llaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wamehimiza sana kiasi ambacho hata kama wanakukata wewe unafaa kuwaunga. Na kawaida wazazi wanawatakia mema watoto wao. Huenda mukaona lakini watoto wenu wakawa hawawezi kwenda kwa babu zao, hivyo itawafanya wawe wanyonge sana. Kitu ambacho tunaweza kukunasihi mwanzo ni uzungumze na wazee wako na kuwakinaisha kuwa haya yatakuwa ni maslahi ya familia zote mbili. Usije ukajuta baadaye na ikawa huna pa kwenda. Labda tukiuliza ni kuwa huyu kijana unamjua vipi? Je, maadili yake ni yepi? Je, anatekeleza ibadah zake?

Na nasiha nyengine kutoka kwetu ni kuwa kabla ya kutoa maamuzi ya mwisho tunakuomba uswali Swalah ya Istikhaarah, ambayo ni kumtaka ushauri Allah kuhusu mas-ala hayo.

Wabillahi at-Tawfiq.

 

 

Share