101-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Anayeghushi Katika Biashara Amekanwa Na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

 

Hadiyth Ya  101

 

Anayeghushi Katika Biashara Amekanwa Na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)

 

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ مَرَّ عَلَى صُبْرَةِ طَعَامٍ فَأَدْخَلَ يَدَهُ فِيهَا فَنَالَتْ أَصَابِعُهُ بَلَلاً فَقَالَ: ((مَا هَذَا يَا صَاحِبَ الطَّعَامِ؟)) قَالَ:  أَصَابَتْهُ السَّمَاءُ يَا رَسُولَ اللَّهِ. قَالَ: ((أَفَلاَ جَعَلْتَهُ فَوْقَ الطَّعَامِ كَيْ يَرَاهُ النَّاسُ، مَنْ غَشَّ فَلَيْسَ مِنِّي))  مسلم

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alipitia katika mrundo wa chakula (nafaka), akaingiza mkono wake ndani. Vidole vyake vikagusa umajimaji. Akasema: ((Ee mwenye chakula, ni nini hii?)). Akajibu: “Ee Rasuli wa Allaah! Kimepatwa na manyunyu”. Akasema: ((Si ungeliweka juu ya chakula ili watu wakione! Anayeghushi si katika mimi)). [Muslim]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Haramisho la kughushi katika kuuza, na muuzaji anapaswa adhihirishe bidhaa anayoiuza inapokuwa na kasoro au ila.  Allaah Anaonya Anaposema:

 وَيْلٌ لِّلْمُطَفِّفِينَ ﴿١﴾

Ole kwa wanaopunja.

الَّذِينَ إِذَا اكْتَالُوا عَلَى النَّاسِ يَسْتَوْفُونَ ﴿٢﴾

Ambao wanapopokea kipimo kwa watu wanataka wapimiwe kamilifu.

وَإِذَا كَالُوهُمْ أَو وَّزَنُوهُمْ يُخْسِرُونَ ﴿٣﴾

Na wanapowapimia (watu) kwa kipimo au wanawapimia kwa mizani wanapunja. [Al-Mutwaffifiyn: 1-3]

 

Rejea pia: Aal-‘Imraan (3: 161), Huwd (11: 85), Ash-Shu’araa (26: 83),  Al-Israa (17: 35).

 

 

2. Kughushi ni kula mali za watu bila ya haki jambo ambalo Ameliharamisha Allaah (سبحانه وتعالى) Anaposema:

 

وَلَا تَأْكُلُوا أَمْوَالَكُم بَيْنَكُم بِالْبَاطِلِ وَتُدْلُوا بِهَا إِلَى الْحُكَّامِ لِتَأْكُلُوا فَرِيقًا مِّنْ أَمْوَالِ النَّاسِ بِالْإِثْمِ وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿١٨٨﴾

Na wala msiliane mali zenu kwa ubatilifu na mkazipeleka (rushwa) kwa mahakimu ili mle sehemu katika mali ya watu kwa dhambi na hali mnajua. [Al-Baqarah (2: 1880]

 

Rejea pia An-Nisaa (4: 29, 161)

 

 

3. Kughushi kunasababisha ufisadi katika ardhi na uadui baina ya jamii.

 

 

4. Kughushi ni khiyana na dhulma, nako ni kuchukua haki ya mtu. Ni dhambi ambazo Allaah (سبحانه وتعالى) Hazisamehi. Aliyefanya hivyo atachukuliwa ‘amali zake njema Siku ya Qiyaamah apewe mdhulumiwa, kama hana, atabebeshwa maovu ya mdhulumiwa.

Rejea Hadiyth namba (19).

 

 

5. Kuingiza kwake Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) mkono wake katika chakula kunatoa mafunzo kwa wenye majukumu ya masoko kuchunguza biashara na bidhaa zinazouzwa ili kuzuia dhulma.

 

 

 

 

Share