102-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Allaah Atakhasimiana na Anayevunja Ahadi Kwa Kiapo, Anayemdhulumu Mwajiriwa
Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 102
Allaah Atakhasimiana na Anayevunja Ahadi Kwa Kiapo, Anayemdhulumu Mwajiriwa
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((قَالَ اللَّهُ تَعَالى: ثلاَثَةٌ أَنَا خَصْمُهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ: رَجُلٌ أَعْطَى بِي ثُمَّ غَدَرَ، وَرَجُلٌ بَاعَ حُرًّا فَأَكَلَ ثَمَنَهُ، وَرَجُلٌ اسْتَأْجَرَ أَجِيرًا فَاسْتَوْفَى مِنْهُ وَلَمْ يُعْطِ أَجْرَهُ)) البخاري
Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم ) amesema:((Allaah Aliyetukuka Amesema: Watu watatu Mimi Nitakhasimiana nao Siku ya Qiyaamah: Mtu aliyempa nduguye ahadi kwa kutumia Jina Langu kisha akavunja ahadi hiyo. Mtu aliyemuuza muungwana na akala thamani yake. Na mtu aliyemwajiri mwajiriwa naye akammalizia kazi yake, wala asimpe ujira wake)). [Al-Bukhaariy]
Mafunzo Na Mwongozo:
1. Maamrisho ya kutimiza ahadi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَأَوْفُوا بِالْعَهْدِ ۖ إِنَّ الْعَهْدَ كَانَ مَسْئُولًا ﴿٣٤﴾
Na timizeni ahadi; hakika ahadi itakuwa ni ya kuulizwa [Al-Israa (17: 34)]
Rejea pia Al-Maaidah (5 :1)
Na asiyetimiza ahadi, atakuwa na sifa ya wanafiki ambao walikuwa hawaachi kuvunja ahadi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّ شَرَّ الدَّوَابِّ عِندَ اللَّـهِ الَّذِينَ كَفَرُوا فَهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ﴿٥٥﴾
Hakika viumbe viovu kabisa mbele ya Allaah ni wale waliokufuru nao hawaamini.
الَّذِينَ عَاهَدتَّ مِنْهُمْ ثُمَّ يَنقُضُونَ عَهْدَهُمْ فِي كُلِّ مَرَّةٍ وَهُمْ لَا يَتَّقُونَ﴿٥٦﴾
Ambao umepeana nao ahadi, kisha wanavunja ahadi yao kila mara, na wala hawana taqwa. [Al-Anfaal (8: 55-56)]
Rejea pia: Al-Baqarah (2: 100), Ar-‘Rad (13: 25).
Rejea pia Hadiyth namba (18).
2. Kutimiza ahadi ni miongoni mwa sifa za wenye taqwa kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى):
لَّيْسَ الْبِرَّ أَن تُوَلُّوا وُجُوهَكُمْ قِبَلَ الْمَشْرِقِ وَالْمَغْرِبِ وَلَـٰكِنَّ الْبِرَّ مَنْ آمَنَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَالْمَلَائِكَةِ وَالْكِتَابِ وَالنَّبِيِّينَ وَآتَى الْمَالَ عَلَىٰ حُبِّهِ ذَوِي الْقُرْبَىٰ وَالْيَتَامَىٰ وَالْمَسَاكِينَ وَابْنَ السَّبِيلِ وَالسَّائِلِينَ وَفِي الرِّقَابِ وَأَقَامَ الصَّلَاةَ وَآتَى الزَّكَاةَ وَالْمُوفُونَ بِعَهْدِهِمْ إِذَا عَاهَدُوا ۖ وَالصَّابِرِينَ فِي الْبَأْسَاءِ وَالضَّرَّاءِ وَحِينَ الْبَأْسِ ۗ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ صَدَقُوا ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُتَّقُونَ ﴿١٧٧﴾
Sio wema kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande wa Mashariki na Magharibi lakini wema ni mwenye kuamini Allaah na Siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii, na akawapa mali juu ya kuipenda kwake jamaa wa karibu na mayatima na masikini na msafiri na waombao na katika kukomboa watumwa na akasimamisha Swalaah, na akatoa Zakaah na watimizao ahadi zao wanapoahidi, na wanaosubiri katika dhiki za ufukara na maafa ya magonjwa na njaa na katika vita. Hao ndio waliosadikisha na hao ndio wenye taqwa. [Al-Baqarah (2: 177)]
Na pia kutimizia ahadi ni miongoni mwa sifa zitakazomfikisha Muumin katika Jannah ya Al-Firdaws. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ
قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ ﴿١﴾
Kwa yakini wamefaulu Waumini.
الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ ﴿٢﴾
Ambao katika Swalaah zao huwa wananyenyekea.
وَالَّذِينَ هُمْ عَنِ اللَّغْوِ مُعْرِضُونَ ﴿٣﴾
Na ambao wanajiepusha na mambo ya upuuzi.
وَالَّذِينَ هُمْ لِلزَّكَاةِ فَاعِلُونَ ﴿٤﴾
Na ambao wanatoa Zakaah.
وَالَّذِينَ هُمْ لِفُرُوجِهِمْ حَافِظُونَ ﴿٥﴾
Na ambao wanazihifadhi tupu zao.
إِلَّا عَلَىٰ أَزْوَاجِهِمْ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ فَإِنَّهُمْ غَيْرُ مَلُومِينَ ﴿٦﴾
Isipokuwa kwa wake zao, au kwa iliyowamiliki mikono yao ya kuume basi hao hawalaumiwi.
فَمَنِ ابْتَغَىٰ وَرَاءَ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْعَادُونَ ﴿٧﴾
Lakini atakayetaka kinyume ya hayo; basi hao ndio wapindukao mipaka.
وَالَّذِينَ هُمْ لِأَمَانَاتِهِمْ وَعَهْدِهِمْ رَاعُونَ ﴿٨﴾
Na ambao amana zao na ahadi zao wanazichunga.
وَالَّذِينَ هُمْ عَلَىٰ صَلَوَاتِهِمْ يُحَافِظُونَ ﴿٩﴾
Na ambao wanazihifadhi Swalaah zao.
أُولَـٰئِكَ هُمُ الْوَارِثُونَ ﴿١٠﴾
Hao ndio warithi.
الَّذِينَ يَرِثُونَ الْفِرْدَوْسَ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿١١﴾
Ambao watarithi (Jannah) ya Al-Firdaws, wao humo ni wenye kudumu. [Al-Muuminuwn (23: 1-11)]
Rejea pia: Ar-Ra’d (13: 20-24), Al-Ma’arij (70: 32).
3. Inaruhusiwa kuvunja kiapo kwa kubadilisha jambo ovu kwa jambo jema.
Rejea Hadiyth namba (5).
4. Allaah (سبحانه وتعالى) Amemsifu Nabii Ismaa’iyl kwa sifa ya kutimizia ahadi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى)
وَاذْكُرْ فِي الْكِتَابِ إِسْمَاعِيلَ ۚ إِنَّهُ كَانَ صَادِقَ الْوَعْدِ وَكَانَ رَسُولًا نَّبِيًّا ﴿٥٤﴾
Na mtaje katika Kitabu Ismaa’iyl. Hakika yeye alikuwa mkweli wa ahadi na alikuwa Rasuli na Nabiy. [Maryam (19: 54)]
5. Uislamu unahimiza haki baina ya watu na uhuru wa bin Aadam.
6. Makatazo ya kumdhulumu mwajiriwa kwa kutokumlipa ujira wake, kwani kufanya hivyo ni khiana, nayo ni dhulma. Allaah (سبحانه وتعالى) Amekataza hilo Anaposema:
وَمَا كَانَ لِنَبِيٍّ أَن يَغُلَّ ۚ وَمَن يَغْلُلْ يَأْتِ بِمَا غَلَّ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۚ ثُمَّ تُوَفَّىٰ كُلُّ نَفْسٍ مَّا كَسَبَتْ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ﴿١٦١﴾
Na haikuwa (ni tabia) kwa Nabiy yeyote kukhini (ngawira). Na yeyote atakayekhini atakuja na kile alichokikhini Siku ya Qiyaamah. Kisha italipwa kamilifu kila nafsi yale iliyoyachuma nao hawatodhulumiwa [Aal-‘Imraan (3: 161)]
7. Mtu anayekhasimiwa na Allaah (سبحانه وتعالى), tena Siku ya Qiyaamah, atakuwa katika adhabu kali. Hivyo, ni juu yetu tufanye yatakayotupatia uhusiano mzuri na Muumbaji wetu, na mambo yote Aliyotukataza tuwe mbali nayo.
8. Aina nyingi za dhulma na adhabu zake zimetajwa mno katika Qur-aan na Sunnah.