103-Lu-ulu-un-Manthuwrun Allaah Hatowazungumzisha Wala Kuwatazama Wanaoburuza Nguo Zao, Msimbulizi, Na Mwapaji Uongo Kwa Ajili Ya Kuuza Bidhaa

 

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya  103

 

Allaah Hatowazungumzisha Wala Kuwatazama Wanaoburuza Nguo Zao, Msimbulizi,

Na Mwapaji Uongo Kwa Ajili Ya Kuuza Bidhaa

 

 

 

 

عَنْ أَبِي ذَرٍّ (رضي الله عنه)  عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((ثلاَثَةٌ لاَ يُكَلِّمُهُمْ اللَّهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَلاَ يَنْظُرُ إِلَيْهِمْ وَلاَ يُزَكِّيهِمْ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ)) قَالَ فَقَرَأَهَا رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ثلاَثَ مِرَارٍ. قَالَ أَبُو ذَرٍّ: خَابُوا وَخَسِرُوا، مَنْ هُمْ يَا رَسُولَ اللَّهِ؟ قَالَ: ((الْمُسْبِلُ، وَالْمَنَّانُ، وَالْمُنَفِّقُ سِلْعَتَهُ بِالْحَلِفِ الْكَاذِبِ)) مسلم و في رواية له: ((وَالْمُسْبِلُ إِزَارَهُ)) يَعْن الْمُسْبِلَ إزَارَهُ وَثوْبَهُ أسْفَلَ مِنَ الْكَعْبَيْنِ لِلْخُيَلاءِ

 

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Dharr (رضي الله عنه)  amesema: “Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم ) amesema: ((Watu watatu Allaah Hatowazungumzisha Siku  ya Qiyaamah, wala Hatowatazama, wala Hatowatakasa, na watapata adhabu inayoumiza)). Akayakariri maneno hayo mara tatu. Abuu Dharr akasema: “Wamepita patupu na wamekhasirika! Ni nani hao ee Rasuli wa Allaah?”  Akasema: ((Al-Musbil - mwenye kuburuza nguo yake, mwenye kutoa na kukizungumzia [kusimbulia] alichokitoa, na mwenye kuuza bidhaa zake kwa kutumia kiapo cha uongo)). [Muslim] Na pia: ((anayeburuza izari yake)). [Muslim] yaani nguo yake kuvuka chini ya mafundo ya miguu kwa kiburi.

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

1. Haramisho la mwanamme kuburuza nguo yake, kwani ni alama ya kiburi

 

Hadiyth: ((Ole wako na kuburuza nguo [kuvuka mafundo ya miguu], kwani kuburuza nguo ni alama ya kiburi)). [Fat-hul-Baariy Mj. (10), uk. (264)]

 

 

2. Haramisho la masimbulizi, kwani yanasababisha udhalilifu kwa yule anayepewa. Allaah (سبحانه وتعالى) Anataja makatazo yake na makemeo yake, na pia Anataja fadhila za asiyesimbulia kutoa mali yake katika Aayah zifuatazo: 

 

 الَّذِينَ يُنفِقُونَ أَمْوَالَهُمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ ثُمَّ لَا يُتْبِعُونَ مَا أَنفَقُوا مَنًّا وَلَا أَذًى ۙ لَّهُمْ أَجْرُهُمْ عِندَ رَبِّهِمْ وَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ ﴿٢٦٢﴾

Wale wanaotoa mali zao katika njia ya Allaah kisha hawafuatishii kwa waliyoyatoa masimbulizi wala udhia watapa ujira wao kwa Rabb wao, na wala hakuna khofu juu yao na wala hawatohuzunika.

 

قَوْلٌ مَّعْرُوفٌ وَمَغْفِرَةٌ خَيْرٌ مِّن صَدَقَةٍ يَتْبَعُهَا أَذًى ۗ وَاللَّـهُ غَنِيٌّ حَلِيمٌ ﴿٢٦٣﴾

Kauli njema na msamaha ni bora kuliko swadaqah inayoifuata udhia. Na Allaah ni Mkwasi, Mvumilivu.

 

 

 يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُبْطِلُوا صَدَقَاتِكُم بِالْمَنِّ وَالْأَذَىٰ كَالَّذِي يُنفِقُ مَالَهُ رِئَاءَ النَّاسِ وَلَا يُؤْمِنُ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۖ فَمَثَلُهُ كَمَثَلِ صَفْوَانٍ عَلَيْهِ تُرَابٌ فَأَصَابَهُ وَابِلٌ فَتَرَكَهُ صَلْدًا ۖ لَّا يَقْدِرُونَ عَلَىٰ شَيْءٍ مِّمَّا كَسَبُوا ۗ وَاللَّـهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْكَافِرِينَ ﴿٢٦٤﴾

Enyi walioamini! Msibatilishe swadaqah zenu kwa masimbulizi na udhia kama yule ambaye anatoa mali yake kwa kujionyesha kwa watu wala hamwamini Allaah na Siku ya Mwisho. Basi mfano wake ni kama jabali juu yake pana udongo, kisha likapigwa na mvua kubwa ikaliacha tupu. Hawana uwezo juu ya lolote katika waliyoyachuma. Na Allaah Haongoi watu makafiri. [Al-Baqarah (2: 262-264)]

 

 

3. Haramisho la kuapa uongo kwa ajili ya kuuza bidhaa, kwani hivyo ni ulaghai na khiyana.

 

Rejea Hadiyth namba (101).

 

 

4. Kuburuza nguo, masimbulizi, kuapa uongo kwa ajili ya kuuza bidhaa ni miongoni mwa madhambi makubwa, kwani yatamharamisha Muislamu kutazamwa na Allaah (سبحانه وتعالى) Siku ya Qiyaamah na watapata adhabu kali.

 

 

5. Haya ni makosa ambayo athari yake inaonekana katika jamii. Na jamii yoyote ambayo ina matatizo haya, basi maendeleo huwa hayapatikani kwani yanaleta bughudha, uadui, khusma na kudharauliana.

 

 

6. Amri ya kutokuburuza nguo kwa wanaume imekuwa ni jambo la kufanyiwa istihzai, kejeli na masikhara kwa wanaotimiza amri hii, kwa kuwa kanzu zao ziko juu ya mafunzo ya miguu yao. Huchekwa na kupewa majina kadhaa ya istihzai kama vile ‘watawa’, ‘kirongwe’, ‘njiwa’ n.k. Watambue Waislamu wanaowafanyia istihzai ndugu zao hao kwamba ni maovu watakayohesabiwa Siku ya Qiyaamah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَلَوْ أَنَّ لِلَّذِينَ ظَلَمُوا مَا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا وَمِثْلَهُ مَعَهُ لَافْتَدَوْا بِهِ مِن سُوءِ الْعَذَابِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۚ وَبَدَا لَهُم مِّنَ اللَّـهِ مَا لَمْ يَكُونُوا يَحْتَسِبُونَ﴿٤٧﴾

Na kama wale waliodhulumu wangelikuwa na vile vyote vilivyomo ardhini na pamoja navyo mfano wake, bila shaka wangelifidia kwayo kutokana na adhabu mbaya ya Siku ya Qiyaamah. Na yatawafichukia kutoka kwa Allaah ambayo hawakuwa wanatarajia.  

 

وَبَدَا لَهُمْ سَيِّئَاتُ مَا كَسَبُوا وَحَاقَ بِهِم مَّا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ﴿٤٨﴾

Na yatawafichukia maovu ya yale waliyoyachuma, na yatawazunguka yale waliyokuwa wakiyafanyia istihzai. [Az-Zumar (39: 47-48)]

 

Na Anasema pia (سبحانه وتعالى):

إِنَّ الَّذِينَ أَجْرَمُوا كَانُوا مِنَ الَّذِينَ آمَنُوا يَضْحَكُونَ ﴿٢٩﴾

Hakika wale waliofanya uhalifu walikuwa (duniani) wakiwacheka wale walioamini.

 

وَإِذَا مَرُّوا بِهِمْ يَتَغَامَزُونَ ﴿٣٠﴾

Na wanapowapitia wanakonyezana.

 

وَإِذَا انقَلَبُوا إِلَىٰ أَهْلِهِمُ انقَلَبُوا فَكِهِينَ ﴿٣١﴾

Na wanaporudi kwa ahli zao, hurudi wenye kufurahika kwa dhihaka. …. [Al-Mutwwaffifiyn (83: 29-36)]

 

 

Rejea pia: Huwd (11: 8), An-Nahl (16: 34), At-Tawbah (9: 65).

 

 

 

 

Share