115-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Makatazo Ya Kunyoa Baadhi Ya Nywele Na Kuacha Baadhi

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 115

 

Makatazo Ya Kunyoa Baadhi Ya Nywele Na Kuacha Baadhi

 

 

 

 

عَنْ ابْنِ عُمَرَ (رضي الله عنهما) أَنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ رَأَى صَبِيًّا قَدْ حُلِقَ بَعْضُ شَعْرِهِ وَتُرِكَ بَعْضُهُ فَنَهَاهُمْ عَنْ ذَلِكَ وَقَالَ: ((احْلِقُوهُ كُلَّهُ أَوْ اتْرُكُوهُ كُلَّهُ)) أبوا داود بإسناد صحيح على شرط البخاري و مسلم

 

Imepokelewa kutoka kwa Ibn ‘Umar (رضي الله عنهما) kwamba Nabiy (صلى الله عليه  وآله وسلم) alimuona mvulana zimenyolewa baadhi ya nywele kichwani mwake na nyingine zimeachwa. Akawakataza, na akasema: ((Mnyoweni zote au ziacheni zote)). [Abuu Daawuwd kwa isnaad Swahiyh ‘alaa shartw (kwa mujibu wa masharti ya) Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Katazo la kunyoa baadhi ya nywele na kuacha baadhi, ambao Kiislamu inaitwa Qaza‘, hivyo ni kujibadilisha umbile na pia kuiga makafiri wanaonyoa kila aina za staili ya nywele.

 

 

2. Uislamu umetoa kila aina ya mafunzo hata ya kumweka Muislamu katika mandhari nzuri kabisa ya fitwrah (maumbile ya asili) na heshima. Kujibadilisha maumbile hayo ya asili ni katika hila za shaytwaan aliyeahidi kuwapotoa watu:

 

 وَلَأُضِلَّنَّهُمْ وَلَأُمَنِّيَنَّهُمْ وَلَآمُرَنَّهُمْ فَلَيُبَتِّكُنَّ آذَانَ الْأَنْعَامِ وَلَآمُرَنَّهُمْ فَلَيُغَيِّرُنَّ خَلْقَ اللَّـهِ ۚ 

 “Na hakika nitawapoteza, na nitawashawishi matamanio ya kulaghai, na nitawaamrisha. Basi watakata masikio ya wanyama (wawatukuze), na nitawaamrisha watabadili maumbile ya Allaah.”  [An-Nisaa (4: 119)]

    

Rejea Hadiyth namba 113.

 

 

3. Baadhi ya wazazi wanawaachia watoto wao kunyoa nywele staili za makafiri ‘panki’ na kuona kuwa ni maendeleo na fakhari kuiga makafiri na hali ni kumpotosha mtoto. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amekataza kuiga makafiri katika Hadiyth:

 

 عَنْ ابْنِ عُمَرَ قَالَ : قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((مَنْ تَشَبَّهَ بِقَوْمٍ فَهُوَ مِنْهُمْ))

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رضي الله عنهما) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Atakayejifananisha na watu basi yeye ni miongoni mwao)) [Abuu Daawuwd na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh Abiy Daawuwd (3401)]

 

 

4. Ruhusa ya ima kunyoa nywele zote au kuziacha zote, ila tu zisiachwe ndefu hadi kushabihiana na wanawake. Na pia zikiwa ndefu basi zisibakishwe matimtimu, bali zinatakiwa zitizamwe kwa kuchanwa na kupakwa mafuta.

 

 

 

 

Share