114-Lu-ulu-un-Manthuwrun :Wanawake Wanaovaa Nguo Lakini Wako Uchi Wenye Vichwa Vya Manundu Hawatoingia Jannah Wala Hawatasikia Harufu Yake

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 114  

 

Wanawake Wanaovaa Nguo Lakini Wako Uchi Wenye Vichwa Vya Manundu

Hawatoingia Jannah Wala Hawatasikia Harufu Yake

 

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((صِنْفَانِ مِنْ أَهْلِ النَّارِ لَمْ أَرَهُمَا: قَوْمٌ مَعَهُمْ سِيَاطٌ كَأَذْنَابِ الْبَقَرِ يَضْرِبُونَ بِهَا النَّاسَ، وَنِسَاءٌ كَاسِيَاتٌ عَارِيَاتٌ مُمِيلاَتٌ مَائِلاَتٌ رُءُوسُهُنَّ كَأَسْنِمَةِ الْبُخْتِ الْمَائِلَةِ، لاَ يَدْخُلْنَ الْجَنَّةَ وَلاَ يَجِدْنَ رِيحَهَا، وَإِنَّ رِيحَهَا لَيُوجَدُ مِنْ مَسِيرَةِ كَذَا وَكَذَا)) مسلم

 

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah(رضي الله عنه)  kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه  وآله وسلم ) amesema: ((Aina mbili za watu wa motoni sijawaonapo [hawapo katika zama zangu]: Watu walio na mijeledi mfano wa mikia ya ng’ombe wanawapiga watu kwa mijeledi hiyo [kwa dhulma], na wanawake waliovaa nguo na ilhali wako uchi, wakitembea kwa maringo huku wakiyanyonga mabega yao na wakiwafunza wengineo kutenda kama hivyo, vichwa vyao ni kama nundu za ngamia-bukhti wanaodemadema. Hawatoingia Jannah wala hawataisikia harufu yake, na kwa hakika harufu yake husikika umbali kadha wa kadhaa)). [Muslim]

 

Ngamia bukhti – ni aina ya ngamia wenye shingo ndefu.

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Haramisho la kuwapiga watu kwa dhulma na tisho kwamba hawatoingia Jannah bali wala hawatasikia  harufu yake.

 

 

 

2. Haramisho kwa wanawake kutokuvaa vazi la Hijaab Aliloamrisha Allaah (سبحانه وتعالى) lenye sitara na heshima. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا ۖ وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِهِنَّ ۖ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ أَبْنَائِهِنَّ أَوْ أَبْنَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي أَخَوَاتِهِنَّ أَوْ نِسَائِهِنَّ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ أَوِ التَّابِعِينَ غَيْرِ أُولِي الْإِرْبَةِ مِنَ الرِّجَالِ أَوِ الطِّفْلِ الَّذِينَ لَمْ يَظْهَرُوا عَلَىٰ عَوْرَاتِ النِّسَاءِ ۖ وَلَا يَضْرِبْنَ بِأَرْجُلِهِنَّ لِيُعْلَمَ مَا يُخْفِينَ مِن زِينَتِهِنَّ ۚ

Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao na wahifadhi tupu zao, na wala wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika. Na waangushe khimaar (shungi) zao mpaka vifuani mwao, na wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa kwa waume zao, au baba zao, au baba za waume wao, au wana wao wa kiume, au wana wa kiume wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kiume wa kaka zao, au wana wa kiume wa dada zao, au wanawake wao (wa Kiislamu), au wale iliyowamiliki mikono yao ya kuume, au wafuasi wanaume wasio na matamanio ya jimai miongoni mwa wanaume au watoto ambao hawatambui kitu kuhusu sehemu za siri za wanawake. Na wala wasipige miguu yao yakajulikana yale wanayoyaficha katika mapambo yao. [An-Nuwr (24: 31)]

 

 

Na rejea Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى) katika Al-Ahzaab (33: 59).

 

3. Hadiyth imetoa pia onyo kali la mwenye kuasi kutokuingia Jannah na kutoisikia harufu yake. 

 

 

4. Wanawake wengi hawatambui vazi khasa la Hijaab. Hujifunika kichwa na huku uso umejaa mapambo, na nguo za mikono mifupi, za kubana zinazodhirisha maumbile ya mwili wote na nyinginezo hata kuonekana mwili wake ndani, na zilizojazwa mapambo ya rangi na ming’aro. Mwanamke anapaswa ajifunze sharti la vazi la Hijaab kwamba;

 

(i) Avae Jilbaab lisitiri kiwiliwili chote cha mwanamke, (pamoja na khilafu iliyopo kati ya wanachuoni kuhusu suala la uwajibu wa kuufunika uso na kutoufunika);

 

(ii) Jilbaab la mwanamke lisiwe na mapambo;

 

(iii) Kitambaa cha Jilbaab kinatakiwa kiwe kizito (kisioneshe vazi la ndani);

 

(iv) Jilbaab linatakiwa liwe pana (lisibane);

 

(v) Jilbaab halitakiwi kutiwa manukato;

 

(vi) Jilbaab halitakiwi lifanane na mavazi ya kiume;

 

(vii) Jilbaab halitakiwi lifanane na mavazi ya makafiri;

 

(viii) Jilbaab halitakiwi liwe ni katika mavazi ya fakhari.

 

 

5. Mwili wa mwanamke ni thamani ambayo inapasa kuhifadhiwa na kufichwa ili isipotee thamani yake. Mfano wake ni kama lulu katika kombe ambayo imehifadhika humo.

 

 

6. Mwanamke ambaye havai vazi la Hijaab, anayejipamba na kudhihirisha mapambo yake mbele ya wasiokuwa mahram wake, anakusanya madhambi mengi kwa kuwatamanisha wanaume wenye nyoyo za matamanio. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى) kuhusu Wake wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Aayah hizi zinawahusu wanawake Waumini wengineo wote:

 

 

يَا نِسَاءَ النَّبِيِّ لَسْتُنَّ كَأَحَدٍ مِّنَ النِّسَاءِ ۚ إِنِ اتَّقَيْتُنَّ فَلَا تَخْضَعْنَ بِالْقَوْلِ فَيَطْمَعَ الَّذِي فِي قَلْبِهِ مَرَضٌ وَقُلْنَ قَوْلًا مَّعْرُوفًا ﴿٣٢﴾

Enyi wake wa Nabiy!  Nyinyi si kama yeyote yule katika wanawake; mkiwa na taqwa, basi msilegeze kauli asije akaingiwa tamaa ambaye moyoni mwake mna maradhi na semeni kauli inayokubalika.

 

 

وَقَرْنَ فِي بُيُوتِكُنَّ وَلَا تَبَرَّجْنَ تَبَرُّجَ الْجَاهِلِيَّةِ الْأُولَىٰ ۖ وَأَقِمْنَ الصَّلَاةَ وَآتِينَ الزَّكَاةَ وَأَطِعْنَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّـهُ لِيُذْهِبَ عَنكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ وَيُطَهِّرَكُمْ تَطْهِيرًا ﴿٣٣﴾

Na bakieni majumbani mwenu, na wala msionyeshe mapambo na uzuri kwa ajinabi kujishaua kama zama za ujahili. Na simamisheni Swalaah, na toeni Zakaah na mtiini Allaah na Rasuli Wake. Hakika Allaah Anataka Akuondosheeni maovu enyi ahli wa nyumba (ya Nabiy) na Akutakaseni mtakaso barabara.  [Al-Ahzaab (33: 32-33)]

 

 

7. Wenye majukumu juu ya wanawake; mume, baba, kaka n.k. wanapaswa kuwahimiza na kuhakikisha kuwa wanawake wao wanavaa vazi la Hijaab, kwani wasipofanya hivyo watakuja kuulizwa kuhusu jukumu na amana yao waliyopewa kuichunga.

 

Rejea Hadiyth namba  (27).

 

 

8. Wanawake wasiovaa Hijaab wanadhania kwamba wako katika maendeleo na kuwadharau wanaovaa Hijaab, na ilhali ni kinyume chake, kwamba wanaovaa vazi la Hijaab wana hadhi zaidi kuliko wasiovaa mbele ya watu na zaidi mbele ya Allaah (سبحانه وتعالى). Je, yupi aliyekuwa na heshima zaidi? Anayevaa Hijaab au wale  wanaotumiliwa kwa picha za tupu zao katika biashara zao? 

 

 

9. Makatazo kwa wanawake wanaovaa nguo za wazi mno maharusini kwa kisingizio kuwa wako mbele ya wanawake wenziwao. Hivyo, wanafikia kuvaa nguo za kudhihirisha sehemu za mwili na hali mipaka yake ni kuonyesha sehemu ambazo huwa wazi wanapokuwa wakifanya kazi za nyumba majumbani mwao kama uso, nywele, shingo, mikono na miguu. Hivyo ni kwa sababu sehemu hizo pia ndio sehemu zinazovaliwa mapambo ya wanawake kama herini, vidani, bangili, vikufu vya miguu.    

 

Rejea Hadiyth namba (111).

 

 

 

 

Share