123-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Anayekwenda Kuswali Asile Kitunguu Au Kitunguu Thomu

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 123

 

Anayekwenda Kuswali Asile Kitunguu Au Kitunguu Thomu

 

 

 

عَنْ عُمَرَ بْنَ الْخَطَّابِ (رضي الله عنه) أنَّهُ خَطَبَ يَوْمَ الْجُمُعَةِ فَقَالَ فِي خُطْبَتِهِ: ثُمَّ إِنَّكُمْ أَيُّهَا النَّاسُ تَأْكُلُونَ شَجَرَتَيْنِ مَا أَرَاهُمَا إلاَّ خَبِيثَتَيْنِ: الْبَصَلَ وَالثُّومَ! لَقَدْ رَأَيْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ إِذَا وَجَدَ رِيحَهُمَا مِنْ الرَّجُلِ فِي الْمَسْجِدِ أَمَرَ بِهِ فَأُخْرِجَ إِلَى الْبَقِيعِ، فَمَنْ أَكَلَهُمَا فَلْيُمِتْهُمَا طَبْخًا-    مسلم

Imepokelewa kutoka kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab (رضي الله عنه) kwamba alikhutubia Siku ya Ijumaa akasema katika khutbah yake: Kisha enyi watu! Mnakula miti miwili, siioni isipokuwa ni ya kukirihisha; kitunguu na kitunguu thomu; Hakika nimemuona Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه  وآله وسلم) anaposikia  harufu zake kwa mtu Msikitini, akiamrisha atolewe aende Al-Baqiy’. Atakayevila, basi aiue (harufu yake) kwa kuipika vyema.  [Muslim]

 

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Makatazo ya kula kitunguu na kitunguu thomu na chochote chenye harufu mbaya kwa anayekwenda Msikitini, ila ikiwa vimepikwa vizuri na harufu yake haipo tena.

 

 

2. Ni vizuri kwa Muislamu awe katika hali ya usafi kila mara na khasa anapochanganyika na wenziwe na mahali pa ‘Ibaadah ili asikirihishe watu kwa uchafu na harufu mbaya. 

 

 

3. Muislamu anapotaka kuswali au kwenda Msikitini, inampasa kubadilisha nguo zilokuwa chafu kwa mwenye kufanya kazi nje kwenye joto, au zinazonuka moshi wa sigara au aina yoyote ya harufu mbaya. Mwanamke pia anayekutoka jikoni baada ya kupika na kusafisha, inampasa aoge na avae nguo safi ndipo amkabili Allaah (سبحانه وتعالى) kwa ‘Ibaadah ya Swalaah, kwani hata Malaika wanachukizwa na harufu mbaya.

 

 

4. Uislamu umesisitiza usafi wa mtu binafsi na pia unajali kuweko amani baina ya watu na kutoudhiana au kukirihishana kwa jambo lolote litakalosababisha chuki au kufarikiana.

 

 

5. Viongozi wa Misikiti wahakikishe na wachunge usafi wa Msikiti na kukataza yote yanayotendwa ambayo ni kinyume na adabu za Msikitini.

 

 

6. Allaah (سبحانه وتعالى) Anastahiki zaidi kuvaliwa nguo nzuri zenye manukato mazuri anapokabiliwa kwa ajili ya ‘Ibaadah. Ameamrisha hivyo:

 

يَا بَنِي آدَمَ خُذُوا زِينَتَكُمْ عِندَ كُلِّ مَسْجِدٍ

Enyi wana wa Aadam! Chukueni mapambo yenu (ya mavazi ya sitara na twahara) katika kila mahala pa ‘Ibaadah. . [Al-A’raaf: 31]

 

Pia Hadiyth: 

إِنَّ اللَّهَ جَمِيلٌ يُحِبُّ الْجَمَالَ

((Hakika Allaah ni Mzuri Anapenda Uzuri)). [Muslim]

 

 

7. Usafi wa kila aina kwa ujumla utimizwe katika Swalaah; mwilini, nguo, mahali pa kuswalia n.k.

 

 

8. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ameamuru Waislamu wanapokwenda Msikitini kwa ajili ya Swalaah, wasiwe na harufu inayokutokana na kula vitu viwili ambavyo ni halaal kishariy’ah, seuze Muislamu kutumia vya haramu ambavyo vina harufu mbaya kama sigara, n.k.

 

 

 

Share