124-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Anayeapa Kwa Asiyekuwa Allaah Amekufuru

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 124  

 

Anayeapa Kwa Asiyekuwa Allaah Amekufuru

 

 

 

عَنْ عَبْد الله ابْنَ عُمَرَ (رضي الله عنهما) أّنَّهُ سَمِعَ رَجُلاً يَقُولُ: لاَ وَالْكَعْبَةِ. فَقَالَ ابْنُ عُمَرَ: لاَ يُحْلَفُ بِغَيْرِ اللَّهِ فَإِنِّي سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ: ((مَنْ حَلَفَ بِغَيْرِ اللَّهِ فَقَدْ كَفَرَ أَوْ أَشْرَكَ)) رواه الترمذي وَقَالَ حَدِيثٌ حَسَنٌ

Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar  (رضي الله عنهما) kwamba amemsikia mtu akiapa: “Hapana! Naapa kwa Al-Kaabah!” Ibn ‘Umar akamwambia: Haifai kuapiwa chochote isipokuwa Allaah, kwani hakika mimi nimemsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: ((Mwenye kuapa kwa asiyekuwa Allaah hakika ameshakufuru, au ameshafanya shirki)). [At-Tirmidhiy na amesema ni Hadiyth Hasan]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

 

1. Haramisho la kuapia kitu au chochote isipokuwa kwa Jina la Allaah (سبحانه وتعالى).

Rejea Hadiyth namba (92), (125).

 

 

2. Hatari ya kuapia kisichokuwa Allaah (سبحانه وتعالى) kinamtia mtu katika madhambi makubwa ya shirki. Na ikiwa amekusudia juu ya kwamba anajua haijuzu, basi kunamtoa mtu nje ya Uislamu.

 

 

3. Baadhi ya yanayotumika kimakosa katika jamii katika kuapia ni:

 

  • Kuapia Mswahafu.
  • Kuapia kwa mama mzazi au wazazi wawili.
  • Kuapia Al-Ka’bah
  • Kuapia kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم).
  • Kuapia kwa vitukufu mbali mbali vya Allaah (سبحانه وتعالى).

 

4. Allaah (سبحانه وتعالى) Pekee Ndiye Mwenye Kustahiki kuapia chochote Atakacho, kwani Yeye Ni Muumba wa kila kitu. Na hivyo Ameapia vitu vingi katika Qur-aan. Suwrah nyingi katika Juzuu za 29 na 30 zimeanza na viapo vya Allaah (سبحانه وتعالى), mfano Allaah (سبحانه وتعالى) Ameapia kwa Tiyn na Zaytuwn, Ameapia kwa Siku ya Qiyaamah, Ameapia kwa jua, mwezi, nyota, nchi ya Makkah, mbingu, ardhi, usiku, mchana, Alfajiri, zama au Swalaah ya Alasiri, na vitu vingi vinginevyo.

 

 

5. Anapoapia jambo mtu, kisha akafanya kinyume chake, basi atimize kafara ya kiapo cha yamini kutokana na amri ya Allaah (سبحانه وتعالى):

 

لَا يُؤَاخِذُكُمُ اللَّـهُ بِاللَّغْوِ فِي أَيْمَانِكُمْ وَلَـٰكِن يُؤَاخِذُكُم بِمَا عَقَّدتُّمُ الْأَيْمَانَ ۖ فَكَفَّارَتُهُ إِطْعَامُ عَشَرَةِ مَسَاكِينَ مِنْ أَوْسَطِ مَا تُطْعِمُونَ أَهْلِيكُمْ أَوْ كِسْوَتُهُمْ أَوْ تَحْرِيرُ رَقَبَةٍ ۖ فَمَن لَّمْ يَجِدْ فَصِيَامُ ثَلَاثَةِ أَيَّامٍ ۚ ذَٰلِكَ كَفَّارَةُ أَيْمَانِكُمْ إِذَا حَلَفْتُمْ ۚ وَاحْفَظُوا أَيْمَانَكُمْ ۚ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمْ آيَاتِهِ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ﴿٨٩﴾

Allaah Hatokuchukulieni kwa viapo vyenu vya upuuzi, lakini Atakuchukulieni kwa (kuvunja) viapo mlivyoapa kwa niyyah mlioifunga thabiti. Basi kafara yake ni kulisha maskini kumi chakula cha wastani mnachowalisha ahli zenu, au kuwavisha nguo, au kuacha huru mtumwa. Lakini asiyeweza kupata (katika hayo), basi afunge Swiyaam siku tatu. Hiyo ndio kafara ya viapo vyenu mnapoapa. Na hifadhini yamini zenu. Hivyo ndivyo Allaah Anavokubainishieni Aayaat (na hukmu) Zake ili mpate kushukuru. [Al-Maaiidah (5:89)]

 

 

Hata hivyo, kiapo kisiapiwe kwa chochote isipokuwa kwa Jina la Allaah (سبحانه وتعالى).

 

 

6. Juu ya hivyo, Allaah (سبحانه وتعالى) Hamchukulii mtu kwa kiapo cha upuuzi ila kile kilokusudiwa kama Anavyosema:

 

 لَّا يُؤَاخِذُكُمُ اللَّـهُ بِاللَّغْوِ فِي أَيْمَانِكُمْ وَلَـٰكِن يُؤَاخِذُكُم بِمَا كَسَبَتْ قُلُوبُكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ حَلِيمٌ ﴿٢٢٥﴾

Allaah Hatokushikeni kwa viapo vyenu vya upuuzi lakini Atakuchukulieni kwa yaliyochuma nyoyo zenu. Na Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mvumilivu [Al-Baqarah (2: 225)]

 

ila tu kiapo kisiapiwe kwa chochote isipokuwa kwa Jina la Allaah (سبحانه وتعالى).

 

 

7. Jambo la kuapa linachukuliwa wepesi na watu na hali linaweza kuwa ni la hatari mno, na Allaah (سبحانه وتعالى) Ametahadharisha kuhifadhi viapo vyetu kama ilivyotajwa katika Aayah ya juu hapo kwenye Al-Maaidah (5: 89).

 

 

 

 

 

Share