130-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Analaaniwa Anayefanya Haja Njia Wapitazo Watu Au Kivulini

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 130

 

Analaaniwa Anayefanya Haja Njia Wapitazo Watu Au Kivulini

 

 

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((اتَّقُوا اللَّعَّانَيْنِ)) قَالُوا: وَمَا اللَّعَّانَانِ يَا رَسُولَ اللَّهِ؟ قَالَ: ((الَّذِي يَتَخَلَّى فِي طَرِيقِ النَّاسِ أَوْ فِي ظِلِّهِمْ)) مسلم

 

Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Jilindeni [jiepusheni] na sehemu mbili zinazopelekea mtu kulaaniwa)). [Maswahaba] Wakauliza: Ni sehemu zipi hizo zinazopelekea mtu kulaaniwa? Akasema: ((Ni mtu kufanya haja katika njia wanazopita watu au katika vivuli wanavyoketi)). [Muslim]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Makatazo ya kufanya haja njiani kwani kufanya kunaleta maudhi kwa watu na pia upo uwezekano wa kusambaza ugonjwa.

 

2. Anaposhikwa mtu na haja akawa hana mahali basi aingie sehemu isiyopitwa na watu au kichakani kufanya haja.

 

 

3. Uislamu umehimiza usafi wa bin Aadam kwa kila upande; kiwiliwili, nguo hata njiani ili ajilinde na uchafu unaosababisha maradhi na abakie salama katika siha.

 

 

4. Usafi na tawahara ni jambo linalopendeza na Allaah (سبحانه وتعالى)  Anapenda wanaojiweka katika hali hiyo kama Anavyosema:

 إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ التَّوَّابِينَ وَيُحِبُّ الْمُتَطَهِّرِينَ ﴿٢٢٢﴾

Hakika Allaah Anapenda wenye kutubia na Anapenda wenye kujitwaharisha. [Al-Baqarah (2: 222)]

 

 

5. Uislamu unapendelea na kuhimiza heshima na sitara ya mtu. Kufanya haja njiani bila ya kuwa na udhuru ni kukosa hayaa, nako ni ukosefu wa Iymaan.

 

Rejea Hadiyth namba (68).

 

 

6. Makatazo ya kufanya haja njiani ni miongoni mwa madhambi makubwa kwa vile yanahusiana na laana ya Allaah (سبحانه وتعالى) na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

 

 7. Pia kukatazwa kwenda haja vivulini mwa watu ni kuwaudhi watu na kuwakosesha sehemu ya kupumzika.  Na tufahamu kuwa tumekatazwa kuwaudhi watu.

 

 

8. Pia tabia ya baadhi ya watu kutupa taka njiani, au wale walioko ndani ya magari kutupa vikopo vya soda, juisi na kadhalika, ni katika mambo yasiyokubalika kutendwa katika Uislamu. 

Share