131-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Allaah Ameridhia Kuabudiwa, Kutokumshirikisha, Kuungana Na Anachukia Uvumi, Udadisi Na Kupoteza Mali

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 131

 

Allaah Ameridhia Kuabudiwa, Kutokumshirikisha, Kuungana

Na Anachukia Uvumi, Udadisi Na Kupoteza Mali

 

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((إِنَّ اللَّهَ يَرْضَى لَكُمْ ثلاَثًا وَيَكْرَهُ لَكُمْ ثلاَثًا: فَيَرْضَى لَكُمْ أَنْ تَعْبُدُوهُ ولاَ تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا، وَأَنْ تَعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّهِ جَمِيعًا ولاَتَفَرَّقُوا،

 وَيَكْرَهُ لَكُمْ قِيلَ وَقَالَ، وَكَثْرَةَ السُّؤَالِ، وَإِضَاعَةِ الْمَالِ )) مسلم

 

Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah (رضي الله عنه)  kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:  ((Hakika Allaah Anawaridhia mambo matatu na Anachukia kwenu mambo matatu; Anawaridhia mumwabudu Yeye, wala msimshirikishe kwa chochote, na mshikamane nyote na kamba ya Allaah wala msifarikiane. Na anachukia kwenu uvumi, kuuliza sana na   kupoteza mali)). [Muslim]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

 

1. Maana ya Tawhiyd ni kumwambudu Allaah (سبحانه وتعالى) bila ya kumshirikisha na chochote.

 

 

 

2. Himizo na amri ya kumwabudu Allaah (سبحانه وتعالى) Pekee. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُمْ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ ﴿٢١﴾

Enyi watu! Mwabuduni Rabb wenu Ambaye Amekuumbeni na wale wa kabla yenu mpate kuwa na taqwa. [Al-Baqarah (2: 21)]

 

Rejea pia: Yuwnus (10: 3), Al-An’aam (6: 102).

 

 

 

3. Haramisho la kumshirikisha Allaah (سبحانه وتعالى) na chochote. Aayah na Hadiyth nyingi zimekataza. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 قُلْ تَعَالَوْا أَتْلُ مَا حَرَّمَ رَبُّكُمْ عَلَيْكُمْ ۖ أَلَّا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا ۖ و

Sema: “Njooni nikusomeeni yale Aliyoyaharamisha Rabb wenu kwenu. Kwamba msimshirikishe na chochote. [Al-An’aam (6: 151)]

 

Rejea pia: An-Nisaa (4: 36), Al-A’raaf (7: 33).

 

 

 

4. Kumwabudu Allaah (سبحانه وتعالى) bila ya kumshirikisha na chochote ni ujumbe walioulingania Rusuli wote kwa kaumu zao. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ ﴿٢٥﴾

Na Hatukutuma kabla yako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) Rasuli yeyote isipokuwa Tulimfunulia Wahy ya kwamba: “Hakika hapana Muabudiwa wa haki ila Mimi; basi Niabuduni.” [Al-Anbiyaa (21: 25)]

 

Rejea pia: An-Nahl (16: 36), Al-‘Araaf (7: 59), (65), (73), (85), Al-‘Ankabuwt (29: 16), Al-Maaidah (5: 72).

 

 

 

5. Himizo na amri ya Waislamu kushikamana pamoja bila ya kufarikiana.

 

Rejea: Aal-‘Imraan (3: 103).

 

 

 

6. Chukizo na makatazo ya kuzungumza habari za uvumi, porojo n.k. Haya yanakutokana na uovu wa ulimi unaompelekea mtu katika ghiybah (kusengenya), namiymah (kufitinisha), n.k. Imesisitizwa kuuhifadhi ulimi mtu asitamke neno ila la kheri.

 

Rejea Hadiyth namba (37).

 

 

 

7. Makatazo ya kuuliza sana maswali au jambo ikiwa halina maana au halihitajiki, kuepusha mjadala na kupoteza muda wa Mwalimu.

 

 

 

8. Makatazo ya kupoteza mali katika njia zisizokubalika kishariy’ah na zisizomridhisha Allaah (سبحانه وتعالى), kama kufuja katika sherehe za harusi za kifakhari, ambazo watu kushindana na kujionyesha. Huu ni ubadhirifu Alioukataza Allaah (سبحانه وتعالى) na kusema kwamba wabadhirifu ni ndugu wa shaytwaan. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَآتِ ذَا الْقُرْبَىٰ حَقَّهُ وَالْمِسْكِينَ وَابْنَ السَّبِيلِ وَلَا تُبَذِّرْ تَبْذِيرًا ﴿٢٦﴾

 

Na mpe jamaa wa karibu haki yake, na masikini, na msafiri (aliyeharibikiwa); na wala usifanye ubadhirifu wa ufujaji mkubwa. 

 

إِنَّ الْمُبَذِّرِينَ كَانُوا إِخْوَانَ الشَّيَاطِينِ ۖ وَكَانَ الشَّيْطَانُ لِرَبِّهِ كَفُورًا ﴿٢٧﴾

 

Hakika wabadhirifu wamekuwa ni ndugu wa mashaytwaan, na shaytwaan amekuwa kwa Rabb wake ni mwingi wa kukufuru. [Al-Israa (17: 26-27)]

 

Rejea pia Al-Furqaan (25: 67).

 

 

 

9. Kutumia mali katika shughuli za bid’ah kama mawlid, matanga, khitmah n.k. ni kupoteza mali yake Muislamu na muda wake bure kwa ‘amali isiyokubaliwa.  

 

 

 

10. Muislamu anafaa afahamu kuwa mali ni amana kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى), hivyo basi asiitumie ovyo kwa sababu atasimama mbele ya Allaah (سبحانه وتعالى) kuulizwa vipi ameipata na vipi ameitumia:   

 

 

Hadiyth: Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

 

لا تزولُ قدَما عبدٍ يومَ القيامةِ حتَّى يُسألَ عن أربعٍ: ((عن عُمرِهِ فيمَ أفناهُ؟ وعن علمِهِ ماذا عمِلَ بهِ؟ وعن مالِهِ مِن أينَ اكتسبَهُ، وفيمَ أنفقَهُ؟ وعن جسمِهِ فيمَ أبلاهُ؟))

((Mguu wa mmoja wenu hautoweza kunyanyuka Siku ya Qiyaamah mpaka aulizwe mambo manne: Umri wake ameupitisha vipi; na elimu yake ameifanyia kazi vipi, mali yake ameipata na kuitumia vipi, na mwili wake ameutumia na kuuchakaa vipi))]. [At-Tirmidhiy kutoka kwa Ibn Mas’uwd (رضي الله عنه) ameisahihisha Al-Albaaniy katika: Swahiyh At-Targhiyb (3592)]

 

 

 

Share