133-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Makatazo Ya Kuvaa Hariri, Diybaaj (Hariri Iliyotariziwa) Na Kunywa Katika Vyombo Vya Dhahabu Na Fedha

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 133 

 

Makatazo Ya Kuvaa Hariri, Diybaaj (Hariri Iliyotariziwa)

Na Kunywa Katika Vyombo Vya Dhahabu Na Fedha

 

 

 

عَنْ حُذَيْفَة (رضي الله عنه) أنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ نَهَانَا عَنْ الْحَرِيرِ وَالدِّيبَاجِ وَالشُّرْبِ فِي آنِيَةِ الذَّهَبِ وَالْفِضَّةِ, وَقَالَ: ((هُنَّ لَهُمْ فِي الدُّنْيَا وَهِيَ لَكُمْ فِي الآَخِرَةِ)) متفق عليه. وفي رواية في الصحيحن عَنْ حُذَيْفَةُ  (رضي الله عنه) قَال: سَمِعْتُ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ: ((لاَ تَلْبَسُوا الْحَرِيرَ وَلاَ الدِّيبَاجَ ولاَ تَشْرَبُوا فِي آنِيَةِ الذَّهَبِ وَالْفِضَّةِ وَلاَ تَأْكُلُوا فِي صِحَافِهَا((

 

Imepokelewa kutoka kwa Hudhayfah (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم ) amekataza (kuvaa nguo za) Hariri, na diybaaj (hariri ya kimashariki iliyotariziwa) na kunywa katika vyombo vya dhahabu na fedha, akasema: ((Hivyo ni vyao [makafiri] duniani, navyo ni vyenu Aakhirah)). [Al-Bukhaariy na Muslim] Na katika riwaayah nyingine iliyopokelewa kutoka kwa Hudhayfah (رضي الله عنه) amesema: Nimemsikia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: ((Msivae hariri wala diybaaj (hariri iliyotariziwa), wala msinywe katika vyombo vya dhahabu na fedha, wala msile katika sinia zake)). [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Diybaaj: ni aina ya hariri nzito iliyotariziwa kama makhmeli.

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Haramisho la wanaume kuvaa hariri, kwa vile ni dalili ya kiburi, ufakhari na kujifananisha na makafiri. Ama wanawake wameruhusika kama walivyonukuu Ma’ulamaa.

 

 

2. Haramisho la kutumia vyombo vya kulia vya dhahabu na fedha, kwa vile ni dalili ya kiburi, na pia israfu ya mali.

 

Na Hadiyth pia imethibitisha haramisho hilo kwa onyo kali la moto wa Jahannam:

 

وَعَنْ أُمِّ سَلَمَةَ رَضِيَ الْلَّهُ عَنْهَا، قَالَتْ: قَالَ رَسُولُ الْلَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏:(( الَّذِي يَشْرَبُ فِي إِنَاءِ الْفِضَّةِ إِنَّمَا يُجَرْجِرُ فِي بَطْنِهِ نَارَ جَهَنَّمَ )) مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ 

Kutoka kwa Ummu Salamah (رَضِيَ اللهُ عَنْهَا) amesema kuwa: Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Hakika anayekunywa katika vyombo vya fedha anameza moto wa Jahannam tumboni mwake.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

3. Haramisho la wanaume kuvaa dhahabu ila pete ya fedha wanaruhusiwa. Ama wanawake, wao wameruhusiwa kuvaa dhahabu za kiasi na wachunge kuzilipia Zakaah.

 

 

4. Makatazo ya kuvaa hariri na kutumia dhahabu na fedha ni miongoni mwa madhambi makubwa kwa vile yameahidiwa adhabu kali ya moto Hadiyth: ((Anayekunywa katika chombo cha fedha, hakika anagogomoa [anasukutua mpaka kooni] tumboni mwake moto wa Jahannam))]. [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

5. Muislamu anapaswa atamani starehe za Aakhirah zilizoahidiwa Aakhirah kuliko starehe za duniani ambazo ni za wakati tu.  

Rejea Hadiyth namba (57), (58), (60), (61).

 

Kutamani starehe za Aakhirah na kuipa mgongo dunia ni katika sifa ya ‘zuhd’ apasayo kuwa nayo Muumin.

 

Rejea Hadiyth namba (59).

 

 

6. Aayah nyingi zimetaja starehe za watu wa Jannah kwamba huko watakuwa wanatumia vyombo vyao vya dhahabu, fedha na mapambo ya hariri, lulu n.k. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

يَا عِبَادِ لَا خَوْفٌ عَلَيْكُمُ الْيَوْمَ وَلَا أَنتُمْ تَحْزَنُونَ﴿٦٨﴾

 “Enyi waja Wangu! Hakuna khofu juu yenu leo, na wala nyinyi hamtohuzunika.”

 

الَّذِينَ آمَنُوا بِآيَاتِنَا وَكَانُوا مُسْلِمِينَ﴿٦٩﴾

“Ambao wameamini Aayaat Zetu na wakawa Waislamu.”

 

ادْخُلُوا الْجَنَّةَ أَنتُمْ وَأَزْوَاجُكُمْ تُحْبَرُونَ﴿٧٠﴾

Ingieni Jannah nyinyi na wake zenu mfurahishwe.

 

 

يُطَافُ عَلَيْهِم بِصِحَافٍ مِّن ذَهَبٍ وَأَكْوَابٍ ۖ وَفِيهَا مَا تَشْتَهِيهِ الْأَنفُسُ وَتَلَذُّ الْأَعْيُنُ ۖ وَأَنتُمْ فِيهَا خَالِدُونَ﴿٧١﴾

Watapitishiwa sahani za dhahabu na bilauri, na humo mna yale yanayotamani nafsi na ya kuburidisha macho, nanyi humo ni wenye kudumu.

 

وَتِلْكَ الْجَنَّةُ الَّتِي أُورِثْتُمُوهَا بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ﴿٧٢﴾

Na hiyo ni Jannah ambayo mmerithishwa kwa yale mliyokuwa mkitenda.

 

لَكُمْ فِيهَا فَاكِهَةٌ كَثِيرَةٌ مِّنْهَا تَأْكُلُونَ﴿٧٣﴾

Mtapata humo matunda mengi mtakayokuwa mnakula. [Az-Zukhruf: 68-73]

 

Rejea pia: Al-Kahf (18: 30-31), Al-Hajj (22: 22-23), Asw-Swaaffaat (37: 40-49), Ad-Dukhaan (44: 51-57), Muhammad (47: 15), Atw-Twuwr (52: 17-24), Ar-Rahmaan (55: 46-77), Al-Waaqi’ah (56: 14-40), Al-Insaan (76: 11-22),  An-Nabaa (78: 31-37), Al-Ghaashiyah (88: 8-16).

 

 

 

7. Muislamu anapasa kujiepusha na kila jambo linalotendwa na makafiri kama Anavyotahadharisha Allaah (سبحانه وتعالى) Rejea Al-Baqarah (2: 120).

 

 

Na inampasa Muislamu kushikamana na mila na desturi za Kiislamu

 

Share