132-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Amelaaniwa Anayemwelekeza Nduguye Silaha

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 132

 

Amelaaniwa Anayemwelekeza Nduguye Silaha

 

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((لاَ يُشِيرُ أَحَدُكُمْ عَلَى أَخِيهِ بِالسِّلاَحِ فَإِنَّهُ لاَ يَدْرِي لَعَلَّ الشَّيْطَانَ يَنْزِعُ فِي يَدِهِ فَيَقَعُ فِي حُفْرَةٍ مِنْ النَّارِ)) متفق عليه – وفي رواية لمسلم قال: قَالَ أبو الْقاَسِم (صلى الله عليه و آله وسلم): ((مَنْ أَشَارَ إِلَى أَخِيهِ بِحَدِيدَةٍ فَإِنَّ الْمَلآئِكَةَ  تَلْعَنُهُ حَتَّى يَدَعَهُ وَإِنْ كَانَ أَخَاهُ لإبِيهِ وَأُمِّهِ(( 

 

Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah (رضي الله عنه)  kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Mmoja wenu asimwelekezee silaha nduguye, kwani hajui pengine shaytwaan huenda akamshopoa katika mkono wake ikawa ndio sababu ya kuingia katika shimo la moto)). [Al-Bukhaariy na Muslim] Na katika riwaya nyingine: “Amesema Abul-Qaasim (صلى الله عليه وآله وسلم): ((Atakayemwelekezea nduguye chuma [silaha], basi hakika Malaika wanamlaani mpaka aiondoshe, hata kama ni kaka yake kwa baba na mama)).  [Muslim]

 

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Haramisho la kumwelekezea mtu silaha, kwani hivyo ni kumtishia mtu na kumkosesha amani na utulivu wa nafsi.

 

Rejea Hadiyth namba (94).

 

 

2. Makatazo haya hayapasi hata kwa asiyekuwa Muislamu ikiwa hana hatia yoyote, kwani huenda akamuua bila ya haki jambo lililoharamishwa.

 

Rejea Al-Mumtahinah (60: 8-9).

 

Bali kumuua mtu ataingizwa motoni, na atapata ghadhabu za Allaah, laana Yake, na adhabu kubwa kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى):

 وَمَن يَقْتُلْ مُؤْمِنًا مُّتَعَمِّدًا فَجَزَاؤُهُ جَهَنَّمُ خَالِدًا فِيهَا وَغَضِبَ اللَّـهُ عَلَيْهِ وَلَعَنَهُ وَأَعَدَّ لَهُ عَذَابًا عَظِيمًا ﴿٩٣﴾

Na atakayemuua Muumini kwa kusudi, basi jazaa yake ni Jahannam, ni mwenye kudumu humo na Allaah Atamghadhibikia na Atamlaani na Atamuandalia adhabu kuu. [An-Nisaa (4: 93)]

 

 

3. Makatazo haya ni miongoni mwa madhambi makubwa kwa vile yanahusiana na laana za Malaika.

 

 

4. Mzaha katika kuleta madhara na kuhatarisha maisha ya mtu haukubaliki katika Shariy’ah ya Kiislamu.

 

 

5. Haipasi kubeba silaha bila ya kuwa na mahitaji nayo, kama upanga, kisu, kiwembe n.k.

 

 

6. Tahadharisho la vitimbi vya shaytwaan ambaye yuko tayari kumpotosha mtu aingie motoni kwa kila njia

 

Rejea Al-Hijr (15: 39), Al-A’raaf (7: 16-18).

 

 

7. Uislamu unalinda usalama na amani ya bin Aadam.

 

Rejea Hadiyth namba (93).

Share