135-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Makatazo Ya Kustanji Na Kugusa Uchi Kwa Mkono Wa Kulia

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 135  

 

Makatazo Ya Kustanji Na Kugusa Uchi Kwa Mkono Wa Kulia

 

 

 

عَنْ أَبِي قَتَادة (رضي الله عنه) عن النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قال: ((إذا بَالَ أَحَدُكُمْ فَلا يَأْخُذَنَّ ذَكَرَهُ بِيَمِينِهِ وَلاَ يَسْتَنْجِ بِيَمِينِهِ وَلاَ يَتَنَفَّسْ فِي الإِنَاءِ)) متفق عليه

Imepokelewa kutoka kwa Abu Qataadah (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Anapokojoa mmoja wenu, asiishike kabisa dhakari yake [uchi wake] kwa mkono wake wa kulia, wala asistanji kwa mkono wake wa kulia, wala asipumue katika chombo)). [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Chukizo la kutumia mkono wa kulia wakati wa kustanji, kwani mkono huo wa kulia unatumika kwa kulia chakula. Amekataza Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) katika Hadiyth nyengineyo:

 

عن سَلْمَانَ ‏ رضى الله عنه ‏ قَالَ: لَقَدْ نَهَانَا رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏ "أَنْ نَسْتَقْبِلَ اَلْقِبْلَةَ بِغَائِطٍ أَوْ بَوْلٍ، أَوْ أَنْ نَسْتَنْجِيَ بِالْيَمِينِ، أَوْ أَنْ نَسْتَنْجِيَ بِأَقَلَّ مِنْ ثَلَاثَةِ أَحْجَارٍ، أَوْ أَنْ نَسْتَنْجِيَ بِرَجِيعٍ أَوْ عَظْمٍ" رَوَاهُ مُسْلِمٌ

Kutoka kwa Salmaan (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alitukataza kuelekea Qiblah wakati wa kwenda haja kubwa au ndogo, wala tusijisafishe kwa mkono wa kulia, au kujisafisha kwa mawe yasiyotimia matatu, au kujisafisha kwa kinyesi cha wanyama au mfupa.” [Imetolewa na Muslim]

Makatazo hayo yanawahusu wanaume na wanawake sawasawa.

 

Rejea Hadiyth namba (33).

 

 

2. Inaruhusiwa kustanji kwa mkono wa kulia kwa dharura. Mfano anapokuwa mtu ameumia mkono wa kushoto, au amekatazwa kutumia maji kutokana na madhara fulani ya kiafya au ugonjwa au kidonda.

 

 

3. Makatazo ya kupumua katika chombo anachonywea maji mtu. Hii imethibitika katika sayansi madhara yake kwamba viini vya maradhi huingia katika chombo vikamsababishia mtu magonjwa.

 

 

4. Uislamu umetahadharisha kila jambo linalopelekea katika uovu na maasi, na umefunza na kuhimiza siha na afya ya mtu kwa ujumla.

 

 

5. Uislamu umefunza tabia na maadili mema kabisa ya kutumia mkono wa kulia kwa ajili ya mambo mazuri na yenye utukufu kama kula, kunywa, kuandika, kuamkiana, kuvaa nguo, viatu, kutoka msalani (chooni), kumdhukuru Allaah (سبحانه وتعالى) kwa tasbiyh baada ya Swalaah, kulala pia iwe kwa ubavu wa kulia n.k. Ama mkono na mguu wa kushoto utumike kwa mambo ya kinyume chake, kama kuingia chooni, kujisafisha tupu, kuokota uchafu, kuubeba n.k.

 

 

 

 

Share