136-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Kutabiri Ya Ghayb Kwa Kupiga Fali (Rajua Mbaya) Kutokana Na Tukio Fulani Ni Shirki

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 136

 

Kutabiri Ya Ghayb Kwa Kupiga Fali (Rajua Mbaya)

Kutokana Na Tukio Fulani Ni Shirki

 

 

 

 

عنْ عُرْوَةَ بْنِ عامِرِ (رضي الله عنه) قال: ذُكِرتِ الطَّيَرَةُ عِنْد رَسُولِ اللَّه صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فقَالَ: ((أحْسَنُهَا الْفَألُ، وَلا تَرُدُّ مُسْلِماً، فَإذا رأى أحَدُكُمْ ما يَكْرَه، فَلْيقُلْ: اللَّهُمَّ لا يَأتى بالحَسَناتِ إلاَّ أنتَ، وَلا يَدْفَعُ السَّيِّئاتِ إلاَّ أنْتَ، وَلا حوْلَ وَلا قُوَّةَ إلاَّ بك)) حديثٌ صَحيحٌ رَوَاهُ أبو داودُ بإسنادٍ صَحيحٍ

 

Imepokelewa kutoka kwa ‘Urwah bin ‘Aamir (رضي الله عنه) amesema: Ilitajwa habari ya kupiga fali mbaya (mkosi) mbele ya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: ((Ilio bora zaidi ni kupiga fali nzuri, wala [kupiga fali mbaya] haimrudishi Muislamu [kutokutenda aliloazimia]. Mmoja wenu atakapoona analochukia, aseme: “Allaahumma laa yaa-tiy bil-hasanaat illaa Anta, walaa yadfa’us-sayyiaat illa Anta, walaa hawla walaa quwwata illaa Bika - Ee Allaah, hakuna anayeweza kuleta mambo mema isipokuwa ni Wewe, wala hakuna anayeweza kukinga mabaya isipokuwa ni Wewe. Hakuna uwezo wala nguvu isipokuwa kutoka Kwako)) [Hadiyth Swahiyh ameipokea Abu Daawuwd kwa Isnaad Swahiyh]

 

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Maana ya twayr (ndege) ni  kupiga fali.

 

 

Wakati wa ujahiliya, Waarabu walikuwa wakichukua ndege (طير) na humtumilia kuonyesha ishara nzuri au mbaya. Mfano wanapotaka kusafiri humrusha ndege yule, akiruka upande wa kulia, basi wanaamini kuwa ni safari ya salama, na kama akiruka upande wa kushoto, basi huwa hawasafiri. Uislamu umekuja na kuondoa shirki kama hiyo kama alivyotukataza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) katika Hadiyth kadhaa, miongoni mwa hizo ni:   

 

 

عَنْ أَنَسٍ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): ((لَا عَدْوَى وَلَا طِيَرَةَ وَيُعْجِبُنِي الْفَأْلُ))  قَالُوا:  وَمَا الْفَأْلُ؟ قَالَ: ((الْكَلِمَةُ الطَّيِّبَةُ))

Kutoka kwa Anas (رضي الله عنه)  amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Hakuna ‘adwaa wala hakuna twiyarah [itikadi ya kutabiri mkosi, nuksi] na inanipendekeza Al-Fa-l)) Wakauliza: Nini Al-Fa-lu? Akajibu: ((Neno zuri)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Na pia:

 

عن ابْنِ مَسْعُودٍ مَرْفُوعًا: ((الطِّيَرَةُ شِرْكٌ، الطِّيَرَةُ شِرْكٌ، وَمَا مِنَّا إِلاَّ وَلَكِنَّ اللَّهَ يُذْهِبُهُ بِالتَّوَكُّلِ)) رَوَاهُ أَبُو دَاوُدَ وَالتِّرْمِذِيُّ وَصَحَّحَهُ. وَجَعَلَ آخِرَهُ مِنْ قَوْلِ ابْنِ مَسْعُودٍ

Na kutoka kwa Ibn Mas’uwd ni Hadiyth Marfuw’: ((Atw-Twiyarah [itikadi ya kutabiri nuksi, mikosi n.k] ni shirki, Atw-Twiyarah ni shirki. Na hakuna yeyote miongoni mwetu asiyehisi jambo moyoni [Kuhusu Atw-Twiyarah] lakini Allaah Huiondoa kwa kutawakali Kwake)) [Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy na amesema Hadiyth hii Hasan Swahiyh] Na imetajwa kwamba kauli ya mwisho ni ya Ibn Mas’uwd.

 

Pia Hadiyth: 

 

((Hakuna mkosi, na ni bora tegemea khayr [matumaini mema])). Wakauliza nini matumaini mema (matarajio ya kufanikiwa) ee Rasuli wa Allaah? Akasema: ((Ni neno jema alisikialo mmoja wenu)) [Al-Bukhaariy]

 

 

2. Kubashiria jambo la ghayb ni miongoni mwa madhambi makubwa, kwani ni kumshirikisha Allaah (سبحانه وتعالى) katika Qadhwaa na Qadar Yake. (Yaliyohukumiwa na Yaliyokadiriwa).

 

 

3 Muislamu awe na iymaan ya kutambua kwamba hakuna yeyote au lolote litakaloweza kumdhuru isipokuwa lile lililokwishaandikwa.

 

Rejea Hadiyth namba (6).

 

Pia

 

 

عن ابنِ عباسٍ رضي الله عنهما، قَالَ: كنت خلف النَّبيّ صلى الله عليه وسلم يومًا، فَقَالَ: ((يَا غُلامُ، إنِّي أعلّمُكَ كَلِمَاتٍ: احْفَظِ اللهَ يَحْفَظْكَ، احْفَظِ اللهَ تَجِدْهُ تُجَاهَكَ، إِذَا سَألْتَ فَاسأَلِ الله، وإِذَا اسْتَعَنْتَ فَاسْتَعِنْ باللهِ. وَاعْلَمْ: أنَّ الأُمَّةَ لَوْ اجْتَمَعَتْ عَلَى أنْ يَنْفَعُوكَ بِشَيءٍ لَمْ يَنْفَعُوكَ إلا بِشَيءٍ قَدْ كَتَبهُ اللهُ لَكَ، وَإِن اجتَمَعُوا عَلَى أنْ يَضُرُّوكَ بِشَيءٍ لَمْ يَضُرُّوكَ إلا بِشَيءٍ قَدْ كَتَبَهُ اللهُ عَلَيْكَ، رُفِعَتِ الأَقْلاَمُ وَجَفَّتِ الصُّحفُ)). رواه الترمذي، وَقالَ: ((حديث حسن صحيح)).

 

Imepokelewa kutoka kwa ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) amesema: “Siku moja nilikuwa nyuma ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akaniambia: ((Ee Ghulamu! [Kijana] nitakufundisha maneno [ya kufaa]; Mhifadhi Allaah [fuata maamrisho Yake na chunga Mipaka Yake] Atakuhifadhi.  Muhifadhi Allaah na utamkuta mbele yako. Ukiomba, muombe Allaah, ukitafuta msaada, tafuta kwa Allaah. [Lazima] ujue kuwa ikiwa taifa zima litaungana kukunufaisha wewe kwa kitu, basi hutonufaika ila tu kwa kile Alichokwisha kukuandikia Allaah. Na wakikusanyika kukudhuru kwa chochote, hutodhurika ila tu kwa kile Allaah Alichokwisha kukuandikia [kuwa kitakudhuru], kwani kalamu zimeshanyanyuliwa [kila kitu kishaandikwa] na sahifa zimeshakauka [Hakuna kupangwa tena wala kupanguliwa]) [Ahmad na at-Tirmidhiy]

 

 

 

4. Hata Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) hakuwa na uwezo wa kujikinga na dhara au kujua ya ghayb. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

قُل لَّا أَمْلِكُ لِنَفْسِي نَفْعًا وَلَا ضَرًّا إِلَّا مَا شَاءَ اللَّـهُ ۚ وَلَوْ كُنتُ أَعْلَمُ الْغَيْبَ لَاسْتَكْثَرْتُ مِنَ الْخَيْرِ وَمَا مَسَّنِيَ السُّوءُ ۚ إِنْ أَنَا إِلَّا نَذِيرٌ وَبَشِيرٌ لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ﴿١٨٨﴾

Sema: “Siimilikii nafsi yangu manufaa yoyote wala dhara yoyote isipokuwa Apendavyo Allaah. Na lau ningekuwa najua ya ghayb, bila shaka ningelijikithirishia ya kheri, na wala lisingelinigusa ovu. Mimi si chochote isipokuwa ni mwonyaji na mbashiriaji kwa watu wanaoamini.” [Al-A’raaf (7: 188)]

 

Rejea pia:  Al-An’aam (6: 50), (59), An-Naml (27: 65).

 

 

5. Baada ya Uislamu, shirki ya aina hii pia hutendeka ingawa si ya kutumia ndege, bali kubashiria ya ghayb kutokana na tendo fulani na kulihusisha na mkosi au nuksi. Mifano ifuatayo inayojulikana:

 

 

(a) Jicho likimpiga mtu upande wa kushoto husema ni shari hiyo inakuja.

 

 

(b) Akimuona mtu paka mweusi, basi siku hiyo itakuwa ni ya ukorofi.

 

(c) Mkono ukimuwasha mtu anasema pesa.

 

(d) Akifagia usiku anaondoa baraka.

 

(e) Akipaliwa mtu, husema kuwa mtu anamtaja.

 

(f) Akikata kucha zote pamoja (ya mikono na miguu) ina maana kwamba shida zikija zitakuja zote pamoja n.k!

 

Hivyo Muislamu anapaswa kuacha itikadi za kidhana kama hizi, kwani khatari yake zinapelekea kwenye kumshirikisha Allaah (سبحانه وتعالى) na mafikio yake ni makazi ya moto.

 

 

6.Kubashiria ya ghayb ni sawa na mtabiri, na pindi Muislamu akiamuamini anayoyatabiri, basi hukutoka nje ya Uislamu.

 

Rejea Hadiyth namba (119).

 

 

Share