138-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Haramisho La Kuomboleza Zaidi Ya Siku Tatu

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 138

 

Haramisho La Kuomboleza Zaidi Ya Siku Tatu

 

 

 

عَنْ زَيْنَبَ بِنْتِ أَبِي سَلَمَةَ  (رضي الله عنهما) قَالَتْ: دَخَلْتُ عَلَى أُمِّ حَبِيبَةَ (رضي الله عنها) زَوْجِ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ حِينَ تُوُفِّيَ أَبُوهَا أَبُو سُفْيَانَ بْنُ حَرْبٍ، فَدَعَتْ بِطِيبٍ فِيهِ صُفْرَةُ خَلُوقٍ، أَوْ غَيْرِهِ،  فَدَهَنَتْ مِنْهُ جَارِيَةً، ثُمَّ مَسَّتْ بِعَارِضَيْهَا . ثُمَّ قَالَتْ: وَاللَّهِ مَا لِي بِالطِّيبِ مِنْ حَاجَةٍ غَيْرَ أَنِّي سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ، يَقُولُ عَلَى الْمِنْبَرِ: ((لا يَحِلُّ لامْرَأَةٍ تُؤْمِنُ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ أَنْ تُحِدَّ عَلَى مَيِّتٍ فَوْقَ ثَلاثِ لَيَالٍ، إِلا عَلَى زَوْجٍ أَرْبَعَةَ أَشْهُرٍ وَعَشْرًا)) قَالَتْ زَيْنَبُ: فَدَخَلْتُ عَلَى زَيْنَبَ بِنْتِ جَحْشٍ (رضي الله عنها) حِينَ تُوُفِّيَ أَخُوهَا، فَدَعَتْ بِطِيبٍ فَمَسَّتْ مِنْهُ ثُمَّ قَالَتْ: أَمَا وَاللَّهِ مَا لِي بِالطِّيبِ مِنْ حَاجَةٍ غَيْرَ أَنِّي سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ عَلَى الْمِنْبَرِ: ((لا يَحِلُّ لامْرَأَةٍ تُؤْمِنُ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ أَنْ تُحِدَّ عَلَى مَيِّتٍ فَوْقَ ثَلاثِ لَيَالٍ إِلاَّ عَلَى زَوْجٍ أَرْبَعَةَ أَشْهُرٍ وَعَشْرًا)) متفق عليه

 

Imepokelewa kutoka kwa Zaynab bin Abiy Salamah (رضي الله عنهما) amesema: “Niliingia kwa Ummu Habiybah (رضي الله عنها) mkewe Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alipofiliwa na baba yake Abuu Sufyaan bin Harb. Akaitisha manukato manjano au manukato ya aina nyingine. Akampaka mjakazi wake na akajipaka mashavuni. Kisha akasema: “Wa-Allaahi sikuwa na haja ya kujipaka manukato isipokuwa nimemsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema juu ya mimbari: ((Si halali kwa mwanamke anayemwamini Allaah na Siku ya Mwisho kumuombolezea maiti zaidi ya siku tatu, isipokuwa amkalie mumewe (eda) miezi minne na siku kumi)). Zaynab akasema: Kisha nikamwendea Zaynab bint Jahshi (رضي الله عنها) alipofiliwa na ndugu yake. Akaitisha manukato, akajipaka kisha akasema: “Wa-Allaahi sikuwa na haja ya manukato, isipokuwa nilimsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: ((Si halali kwa mwanamke anayemwamini Allaah na Siku ya mwisho kumuombolezea maiti zaidi ya siku tatu, isipokuwa amkalie mumewe (eda) miezi minne na siku kumi)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

 

1. Makatazo ya kuomboleza aliyefiwa zaidi ya siku tatu, kwani hivyo ni kinyume na Shariy’ah ya Dini yetu.

 

 

 

2. Ukamilifu wa iymaan kutokana na kauli ((…anayemwamini Allaah na Siku ya mwisho…)) ni kufuata amri hiyo ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kutokuomboleza zaidi ya siku tatu.  

 

 

 

3. Muda wa msiba katika Uislamu usizidi siku tatu, na mtu anaweza kujizuia na kustahamili hata siku moja inatosha kuomboleza, na hali hiyo inathibitisha iymaan ya hali ya juu ya kukubali Qadhwaa na Qadar (Yaliyohukumiwa Na Yaliyokadiriwa).

 

 

 

4. Hakuna katika mapokezi kunakoashiria kuwa wanaume wanaomboleza au wanakaa masiku kufanya maombolezi, hayo ni mambo ya wanawake kwa sababu ya maumbile yao na udhaifu wao wa kuhimili, hivyo Shariy’ah ikawaruhusu wanawake waomboleze lakini isizidi siku tatu. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alifiliwa na wanawe na ‘ami zake na jamaa zake wengine lakini hakuwahi kufanya maombolezi au kutenga masiku ya kuomboleza.

 

 

5. Ilivyo katika Sunnah, ni kumtayarishia chakula mfiwa ili awe katika mapumziko wakati wa huzuni. Hivyo ndivyo alivyoamrisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alipofariki Ja’far (رضي الله عنه) katika vita vya Tabuwk, akasema Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): ((Watengenezeeni familia ya Ja'far chakula, kwani wamefikwa na jambo lenye kuwashughulisha))  [Abuu Daawuwd na ameipa daraja ya Swahiyh Al-Abaaniy katika Ahkaam Al-Janaaiz.

 

 

 

6. Shariy’ah ya eda ya mwanamke aliyefiwa na mumewe ni miezi minne na siku kumi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 

 وَالَّذِينَ يُتَوَفَّوْنَ مِنكُمْ وَيَذَرُونَ أَزْوَاجًا يَتَرَبَّصْنَ بِأَنفُسِهِنَّ أَرْبَعَةَ أَشْهُرٍ وَعَشْرًا ۖ فَإِذَا بَلَغْنَ أَجَلَهُنَّ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ فِيمَا فَعَلْنَ فِي أَنفُسِهِنَّ بِالْمَعْرُوفِ ۗ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ ﴿٢٣٤﴾

Na wale wanaofishwa miongoni mwenu na wakaacha wake, hao wake wangojee peke yao (eda) miezi minne na siku kumi. Watakapofikia muda wao, si dhambi kwao katika yale waliyoyafanya katika nafsi zao kwa ada ya shariy’ah. Na Allaah kwa yale myatendayo ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. [Al-Baqarah (2: 234)]

 

 

7. Kumkalia aliyefiwa matanga ni kumkalifisha kwa kila upande; wasaa wake wa kupumzika, faragha yake, kuwahudumia na kutumia mali yake kwa mambo yasiyopasa. Imekuwa ada ovu katika jamii kumkalia matanga mfiwa, kisha husababisha kutendwa mambo ya bid'ah kama kusoma Khitmah au nyiradi kwa pamoja, mazungumzo ya siasa, mipira, upuuzi wa kidunia, kusengenyana na kucheza karata, dumna, na wengine kula mirungi, kuvuta sigara na mengineo ya haraam.

 

 

8. Anayefiwa anatakiwa awe na iymaan ya mafunzo ya Dini yake na awe na msimamo. Asijali kuambiwa kuwa hamthamini mtu wake aliyefariki kwa kutokuweka matanga kama ilivyokuwa ni itikadi ya baadhi ya watu.

 

 

 

Share