139-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Kujiepusha Na Aliyoyaharamisha Allaah

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 139

 

Kujiepusha Na Aliyoyaharamisha Allaah

 

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنَّهُ قَالَ: ((إِنَّ اللَّهَ يَغَارُ وَغَيْرَةُ اللَّهِ أَنْ يَأْتِيَ الْمُؤْمِنُ مَا حَرَّمَ اللَّه)) متفق عليه

 

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه  وآله وسلم ) amesema: ((Hakika Allaah Ana hisia ya  ghera, na ghera  ya  Allaah [inachomoza] pale mtu anapofanya [maasi] Aliyoyaharamisha Allaah)) [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Amesema Shaykh Muhammad bin Swaalih bin ‘Uthaymiyn (رحمه الله): “Ghera ni sifa ya hakika ya Allaah (سبحانه وتعالى) lakini si ghera kama ghera yetu, bali Yake ni kubwa na tukufu zaidi. Na Allaah (سبحانه وتعالى) kwa Hikma Yake, Amewajibisha kwa waja Wake mambo fulani na Ameharamisha mengine. Aliyowajibisha ni khayr kwao kwa ajili ya Dini yao na dunia yao, kwa   ukaribu wao na mustakbali wao. Na Aliyowaharamishia ni shari kwao kwa ajili ya Dini yao na dunia yao, kwa ukaribu na mustakbali wao. Hivyo basi, Anapoharamisha jambo, Allaah (سبحانه وتعالى) Huwa na ghera pale mtu anapoenda kutenda maharamisho Yake. Na vipi mja ayaendee Aliyoyaharamisha Allaah (سبحانه وتعالى) na hali Ameyaharamisha kwa ajili ya maslahi ya mja? Pamoja na kuwa hakuna madhara kwa Allaah (سبحانه وتعالى) pale mwana Aadam anapomuasi, lakini Allaah Ana ghera, kwa kuwa vipi mwana Aadam anajua kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) ni Al-Hakiym (Mwenye Hikma), na Ar-Rahiym (Mwenye Kurehemu), na wala Haharamishi jambo kwa sababu tu ya kumkosesha asilipate, bali kwa ajili ya maslahi yake, kisha anakuja  mja  akamuasi   Allaah (سبحانه وتعالى) kwa maasi? Seuze basi aje kutenda zinaa? Tunamuomba Allaah (سبحانه وتعالى) Al-‘Aafiyah, kwani Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم) amethibitisha kwa kusema: ((Hakuna mwenye ghera zaidi ya Allaah wakati anapozini mja wake au ummah Wake uzini)) [Al-Bukhaariy]

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Ameharamisha kwa waja Wake zinaa na Amekusanya hilo katika kauli Yake:

 

وَلَا تَقْرَبُوا الزِّنَىٰ ۖ إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَسَاءَ سَبِيلًا ﴿٣٢﴾

Na wala msiikaribie zinaa. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya kabisa.  [Al-Israa (17: 32)]  

 

 

Kwa hiyo mja anapozini, Allaah (سبحانه وتعالى) Huwa na ghera kali na tukufu kuliko ghera ya mja. Hali kadhalika kuyaendea maasi kama liwati ya kaumu Luutw.

 

Rejea: Al-A’raaf (7: 80).

 

Pia kuiba, kunywa pombe, kula haraam na kadhalika. Yote Allaah (سبحانه وتعالى) Huwa na ghera nayo…” [Sharhu Riyaadhwis-Swaalihiyn ya Ibn ‘Uthaymiyn]

 

 

 

2. Hadiyth hii ni miongoni mwa ‘Jawaami’ul-Kalim’ (Mjumuisho wa maana nyingi katika maneno machache) aliyopewa  Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), kwani imekusanya maharamisho yote yanayojulikana katika Shariy’ah ya Kiislamu. Na kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى) imethibitisha:

 

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۖ إِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ﴿٧﴾

Na lolote analokupeni Rasuli ((صلى الله عليه وآله وسلم basi lichukueni, na analokukatazeni, basi acheni. Na mcheni Allaah. Hakika Allaah ni Mkali wa kuakibu.  [Al-Hashr (59: 7)]

 

 

 

3. Hadiyth hii inathibitishia kuwa ghera ni miongoni mwa Sifa za Allaah (سبحانه وتعالى), na itikadi ya Ahlus-Sunnah wal-Jamaa’ah kwamba Sifa Zake zinazomuelekea Yeye Pekee kwa Dhati Yake na si kama sifa za bin Aadam kama Anavyosema Mwenyewe Allaah (سبحانه وتعالى):

 

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ﴿١١﴾

Hakuna chochote kinachofanana Naye, Naye Ndiye Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote. [Ash-Shuwraa (42: 11)]

 

 

 

4. Muislamu anapaswa kujiepusha na maharamisho yote ya Allaah (سبحانه وتعالى) na yaliyokuja katika Sunnah za Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) khasa maasi makubwa kama kumshirikisha Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kila njia, kuzini, liwati, kuua bila ya haki, kuiba, kula ribaa, kutoa shahada ya uongo n.k. Allaah (سبحانه وتعالى) Anayataja baadhi ya hayo katika kauli Zake:

 

وَالَّذِينَ لَا يَدْعُونَ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ وَلَا يَقْتُلُونَ النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّـهُ إِلَّا بِالْحَقِّ وَلَا يَزْنُونَ ۚ وَمَن يَفْعَلْ ذَٰلِكَ يَلْقَ أَثَامًا ﴿٦٨﴾

Na wale ambao hawaombi pamoja na Allaah mwabudiwa mwengine na wala hawaui nafsi ambayo Allaah Ameiharamisha isipokuwa kwa haki, na wala hawazini. Na atakayefanya hivyo atakutana na adhabu.

 

يُضَاعَفْ لَهُ الْعَذَابُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَيَخْلُدْ فِيهِ مُهَانًا ﴿٦٩﴾

Ataongezewa adhabu maradufu Siku ya Qiyaamah, na mwenye kudumu humo akiwa amedhalilika.

 

 

إِلَّا مَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ عَمَلًا صَالِحًا فَأُولَـٰئِكَ يُبَدِّلُ اللَّـهُ سَيِّئَاتِهِمْ حَسَنَاتٍ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٧٠﴾

Isipokuwa yule aliyetubu na akaamini na akatenda ‘amali njema; basi hao Allaah Atawabadilishia maovu yao kuwa mema.  Na Allaah daima ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu.

 

وَمَن تَابَ وَعَمِلَ صَالِحًا فَإِنَّهُ يَتُوبُ إِلَى اللَّـهِ مَتَابًا ﴿٧١﴾

Na atakayetubu na akatenda mema, basi hakika yeye anatubia kwa Allaah tawbah ya kweli.

 

وَالَّذِينَ لَا يَشْهَدُونَ الزُّورَ وَإِذَا مَرُّوا بِاللَّغْوِ مَرُّوا كِرَامًا ﴿٧٢﴾

Na wale ambao hawashuhudii uongo, na wanapopita kwenye upuuzi hupita kwa heshima.

 

وَالَّذِينَ إِذَا ذُكِّرُوا بِآيَاتِ رَبِّهِمْ لَمْ يَخِرُّوا عَلَيْهَا صُمًّا وَعُمْيَانًا ﴿٧٣﴾

Na wale ambao wanapokumbushwa Aayaat za Rabb wao, hawapinduki kuzifanyia uziwi na upofu. [Al-Furqaan (25: 68-73)]

 

 

Na Aayah nyingi nyinginezo zimetaja maharamisho kama hayo.

 

Rejea pia Hadiyth namba, (15), (19), (36), (38), (66), (82), (87), (88), (89), (90), (92), (93), (94), (97), (101), (102), (103), (108), (109), (113), (114), (116), (119), (120), (124), (125), (126), (128), (130), (131), (132).

 

Kinyume chake, Muislamu anapaswa kwa ujumla kumtii Allaah (سبحانه وتعالى) na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kama Anavyoamrisha katika Aayah nyingi miongoni mwazo ni:

 

 قُلْ أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ ۖ فَإِن تَوَلَّوْا فَإِنَّمَا عَلَيْهِ مَا حُمِّلَ وَعَلَيْكُم مَّا حُمِّلْتُمْ ۖ وَإِن تُطِيعُوهُ تَهْتَدُوا ۚ وَمَا عَلَى الرَّسُولِ إِلَّا الْبَلَاغُ الْمُبِينُ ﴿٥٤﴾

 

Sema: “Mtiini Allaah na mtiini Rasuli.” Mkigeukilia mbali, basi hakika jukumu lake ni lile alobebeshwa tu nanyi ni juu yenu yale mliyobebeshwa. Na mkimtii mtaongoka; na hapana juu ya Rasuli isipokuwa ubalighisho bayana. [An-Nuwr (24: 54)]

 

 

 

 

 

Share