140-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Hitimisho: Mfano Wa Mti Mzuri (Mtende) Na Muumin

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 140

 

Hitimisho - Mfano Wa Mti Mzuri (Mtende) Na Muumin

 

 

 

Kuhitimisha mkusanyiko wa Hadiyth hizi, Hadiyth ifuatayo na maelezo yanayofuatia, kunapatikana sifa za kila aina zinazolingana na sifa za Muumin: 

 

 

عَنْ ابْنِ عُمَرَ (رضي الله عنهما) قَال: كُنَّا عِنْد رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَقَالَ: ((أَخْبِرُونِي عَنْ شَجَرَة تُشْبِه - أَوْ - كَالرَّجُلِ الْمُسْلِم لاَ يَتَحَاتّ وَرَقهَا صَيْفًا وَلاَ شِتَاء وَتُؤْتِي أُكُلَهَا كُلّ حِين بِإِذْنِ رَبّهَا)) قَالَ اِبْن عُمَر: فَوَقَعَ فِي نَفْسِي أَنَّهَا النَّخْلَة وَرَأَيْت أَبَا بَكْر وَعُمَر لاَ يَتَكَلَّمَانِ فَكَرِهْت أَنْ أَتَكَلَّمَ فَلَمَّا لَمْ يَقُولُوا شَيْئًا. قَالَ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وآله وَسَلَّمَ: ((هِيَ النَّخْلَة)). فَلَمَّا قُمْنَا قُلْت لِعُمَرَ: يَا أَبَتَاهُ وَاَللَّه لَقَدْ كَانَ وَقَعَ فِي نَفْسِي أَنَّهَا النَّخْلَة. قَالَ: مَا مَنَعَك أَنْ تَتَكَلَّم؟ قُلْت: لَمْ أَرَكُمْ تَتَكَلَّمُونَ فَكَرِهْت أَنْ أَتَكَلَّم أَوْ أَقُول شَيْئًا.  قَالَ عُمَر: لَأَنْ تَكُون قُلْتهَا أَحَبُّ إِلَيَّ مِنْ كَذَا وَكَذَا - البخاري

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رضي الله عنهما)  ambaye amesema: "Tulikuwa na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akauliza: ((Niambieni kuhusu mti unaofanana na (au) ulio kama Muislamu, ambao majani yake hayaanguki wakati wa majira ya joto, wala wakati wa majira ya baridi, na hutoa matunda yake kila mara kwa idhini ya Rabb wake)). Ibn ‘Umar akasema: “Niliufikiria kuwa ni mtende, lakini niliona vibaya kujibu nilipoona Abuu Bakr na ‘Umar hawakujibu”. Akasema Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم): ((Ni mtende)). Tulipoondoka, nilimwambia ‘Umar: “Ee baba yangu! Wa-Allaahi nilihisi kuwa ni mtende”. Akasema: “Kwa nini basi hukutaja?” Nikasema: “Nilikuoneni kimya, nikaona vibaya kusema kitu”. Akasema ‘Umar: "Ungelisema, ingelikuwa bora kwangu kuliko kadhaa na kadhaa” (Yaani ningelikuwa na fakhari zaidi kuwa wewe mwanangu ndiye uliyeweza kujibu pekee). [Al-Bukhaariy]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Njia nzuri ya kumfunza mtu kwa kuuliza swali kama alivyokuwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akiwauliza Maswahaba mara nyingi katika mas-alah ya Dini, mfano Hadiyth namba (88) ((Je, mnajua maana ya Ghiybah? [Kusengenya])) Wakasema: Allaah na Rasuli Wake wanajua. Akasema: ((Ni kumtaja ndugu yako kwa jambo analolichukia)). [Muslim].

 

Na hii ni njia iliyokuwa ikitumiwa mara nyingi na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم). Na ni mbinu ya ufundishaji ambayo inatumiwa leo katika maraakiz mbalimbali.

 

 

 

2. Hikma ya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kupiga mifano mizuri.

 

Rejea mifano ya Hadiyth namba (20), (49), (57), (60), (107).

 

 

 

3. Dhihirisho la adabu na khulka ya Swahaba Ibn ‘Umar (رضي الله عنهما) kutokujibu mbele ya hadhara ya mzazi wake na kuwaachia wakubwa wake wajibu. Hii inadhihirisha pia unyenyekevu wake.

 

 

 

4. Elimu ina upeo wake kwa kila mtu, mdogo anaweza kuwa na ujuzi zaidi kuliko mkubwa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَفَوْقَ كُلِّ ذِي عِلْمٍ عَلِيمٌ ﴿٧٦﴾

Na juu ya kila mwenye elimu yuko mwenye elimu zaidi. [Yuwsuf (12: 76)]

 

Na ndio maana hata katika Swalaah, mwenye elimu zaidi ya Qur-aan hata kama ni mdogo anaongoza Swalaah.

 

 

5. Hadiyth nzima imeufananisha mtende na Muumin ambaye sifa zake zote ni nzuri, mwenye khayr na aliyepewa baraka, na mwenye kupendelea usalama na amani kama ifuatavyo:

 

 

1-Mtende:

Umethibiti ardhini kwa mizizi yake

 

Muumini:

Anathibiti iymaan yake daima na huwa na iymaan ya hali ya juu.

 

 

 

2-Mtende:

Tunda lake ni zuri na tamu.

 

Muumini:

Mazungumzo na vitendo vyake ni vizuri na vya kupendeza, na si mwenye maneno maovu yanayoudhi, kudharau, kukashifu, kusengenya, kufitinisha n.k.

 

 

 

 

3-Mtende:

Umepambika vizuri na kufunikika.

 

Muumini:

Mavazi yake ni mazuri ya heshima.

 

 

 

4-Mtende:

Ni wepesi kula tunda lake.

 

Muumini:

Ni wepesi kujadiliana na watu kwa hoja, dalili na kwa busara.

 

 

 

5-Mtende:

Una faida kwa anayekula, kwani matunda yake yana siha mwilini na huwa ni  kinga ya maradhi, uchawi, na kila aina ya maovu kwa kula (aina ya) tende saba  (za aina ya 'ajwah) asubuhi kabla kula chochote.

 

Rejea Hadiyth kuhusu kula tende saba (za aina ya 'ajwah) asubuhi katika Al-Bukhaariy na Muslim.

 

 

Muumini:

EIimu yake anayotoa ina faida kubwa ya kuwaongoza Waislamu na wasio Waislamu kutoka katika upotofu kuingia katika hidaaya na hivyo ni kuutakasa moyo  katika usalama wa shirki na maovu mengineyo, kinyume na moyo wenye maradhi ya shirki, unafiki n.k.

 

 

 

6-Mtende:

Ni mti madhubuti sana wenye kustahmili upepo mkali.

 

Muumini:

Iymaan yake imethibiti vizuri hata anapopata misukosuko na mitihani, huwa na moyo mkubwa wa kustahmili kama ilivyothibiti katika Hadiyth:  

 

((عَجَبًا لإَمْرِ الْمُؤْمِنِ إِنَّ أَمْرَهُ كُلَّهُ خَيْرٌ، وَلَيْسَ ذَاكَ لإَحَدٍ إلاَّ لِلْمُؤْمِنِ. إِنْ أَصَابَتْهُ سَرَّاءُ شَكَرَ فَكَانَ خَيْرًا لَهُ،  وَإِنْ أَصَابَتْهُ ضَرَّاءُ صَبَرَ فَكَانَ خَيْرًا لَهُ)) مسلم

 

((Ajabu ya jambo la Muumin kwamba kila jambo lakeni kheri. Na halipatikani hili isipokuwa kwa Muumin. Anapofikwa na jambo zuri hushukuru nayo ni kheri kwake na anapofikwa na jambo lenye madhara husubiri nayo ni kheri kwake)) [Muslim]

 

 

 

7-Mtende:

Kila unapokuwa mkubwa unazidi kutoa matunda na faida nyinginezo.

 

Muumini:

Kila anapozidi umri huongezeka elimu, busara na huzidi kunufaisha watu kwa khayr zake.

 

 

Na Allaah (سبحانه وتعالى) Anajua zaidi.

 

 

Huo ndio mfano wa mti mzuri unaofanana na Muumini. Na ni sawa Allaah (سبحانه وتعالى) Anavyofananisha neno zuri na mti mzuri katika kauli Yake: 

 

 أَلَمْ تَرَ كَيْفَ ضَرَبَ اللَّـهُ مَثَلًا كَلِمَةً طَيِّبَةً كَشَجَرَةٍ طَيِّبَةٍ أَصْلُهَا ثَابِتٌ وَفَرْعُهَا فِي السَّمَاءِ ﴿٢٤﴾

Je, huoni vipi Allaah Amepiga mfano wa neno zuri kama mti mzuri mizizi yake imethibitika imara na matawi yake yanafika mbinguni? (marefu mno).

 

تُؤْتِي أُكُلَهَا كُلَّ حِينٍ بِإِذْنِ رَبِّهَا ۗ وَيَضْرِبُ اللَّـهُ الْأَمْثَالَ لِلنَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَتَذَكَّرُونَ ﴿٢٥﴾

Unatoa mazao yake kila wakati kwa idhini ya Rabb wake. Na Allaah Anapiga mifano kwa watu ili wapate kukumbuka. [Ibraahiym (14: 24-25)]

 

 

Ama mfano wa neno ovu na mti muovu Anaendelea Allaah (سبحانه وتعالى) kusema:

 وَمَثَلُ كَلِمَةٍ خَبِيثَةٍ كَشَجَرَةٍ خَبِيثَةٍ اجْتُثَّتْ مِن فَوْقِ الْأَرْضِ مَا لَهَا مِن قَرَارٍ ﴿٢٦﴾

Na mfano wa neno baya ni kama mti mbaya uliong’olewa juu ya ardhi hauna imara. [Ibraahiym (14: 26)]

 

 

Mfano huo wa neno baya ni neno la kufru la kafiri kwa kutokuamini kwake. Amesema Imaam As-Sa’diy (رحمه الله): “Ni mti mbaya kama mti wa “handhwal” na aina yake. Mti huu hauthibitiki wala hautoi matunda mazuri, na hata kama utatoa, basi ni matunda mabaya. Hivyo ndivyo neno la kufru na maasi, halithibitiki kwa manufaa moyoni, wala halitoi ila maneno maovu na vitendo viovu vinavyomdhuru mtu huyo na wala havimnufaishi wala ‘amali zake njema hazipandi kwa Allaah kutakabaliwa, wala ‘amali zake hazimfai nafis yake wala haziwafai wenigneo.”

 

Mti wa handhwal: Ni mti unapatikana jangawani au kichakani, matunda yake yana mibamiba na machungu kama vile mchongoma.

 

 

Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema kuwa Humthibitisha mwenye kuamini katika maisha ya dunia na pia maisha ya Aakhirah kwa neno hilo lililothibiti kama mti, yaani: “Laa ilaaha illa-Allaah.”

 

 

يُثَبِّتُ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ ۖ وَيُضِلُّ اللَّـهُ الظَّالِمِينَ ۚ وَيَفْعَلُ اللَّـهُ مَا يَشَاءُ﴿٢٧﴾

Allaah Huwathibitisha wale walioamini kwa kauli thabiti katika uhai wa dunia na Aakhirah. Na Allaah Huwaacha kupotoka madhalimu. Na Allaah Anafanya Atakavyo. [Ibraahiym (14: 27)]

 

 

Duniani huthibiti kumuamini Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kuendesha maisha yake yote yakiwa katika mipaka ya Rabb wake (عزّ وجلّ) na kutenda mema na kupandishwa ‘amali zake na kutakabaliwa na Allaah (سبحانه وتعالى). Na baada ya kufariki kwake huthibitika kwa kuweza kujibu maswali atakayoulizwa na Malaika wawili kaburini ambao ni Munkar na Nakiyr kama ilivyothibiti katika Hadiyth:

 

 

عَنْ الْبَرَاء بْن عَازِب رَضِيَ اللَّه عَنْهُ أَنَّ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ ((الْمُسْلِم إِذَا سُئِلَ فِي الْقَبْر شَهِدَ أَنْ لاَ إِلَه إِلاَّ اللَّه وَأَنَّ مُحَمَّدًا رَسُول اللَّه فَذَلِكَ قَوْله (يُثَبِّتُ اللَّهُ الَّذِينَ آمَنُوا بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ)) البخاري  وَرَوَاهُ مُسْلِم أَيْضًا وَبَقِيَّة الْجَمَاعَة

Imepokelewa kutoka kwa Al-Baraa bin ‘Aazib (رضي الله عنه)  kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه  وآله وسلم) amesema: ((Muislamu akiulizwa katika kaburi, atashuhudia kwamba: "Laa ilaaha Illa-Allaah wa anna Muhammadar-Rasuwlu-Allaah" (Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na Muhammad ni Rasuli wa Allaah), basi hiyo ndiyo maana ya kauli ya Allaah: ”Allaah Huwatia imara wenye kuamini kwa kauli thabiti katika maisha ya dunia na Aakhirah”)) [Al-Bukhaariy na Muslim na wengineo]

 

 

Hadiyth nyingine imeelezea:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَة قَالَ : قَالَ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((يُثَبِّتُ اللَّهُ الَّذِينَ آمَنُوا بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاة الدُّنْيَا وَفِي الآخِرَة)) قَال: ((ذَلِكَ إِذَا قِيلَ لَهُ فِي الْقَبْر مَنْ رَبّك وَمَا دِينك وَمَنْ نَبِيّك؟ فَيَقُول رَبِّي اللَّه وَدِينِيّ الإسْلاَم, وَنَبِيِّي مُحَمَّد, جَاءَنَا بِالْبَيِّنَاتِ مِنْ عِنْد اللَّه فَآمَنْت بِهِ, وَصَدَّقْت. فَيُقَال لَهُ: صَدَقْت عَلَى هَذَا عِشْت وَعَلَيْهِ مُتّ وَعَلَيْهِ تُبْعَث))  

 

Imekutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه)  kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم ) amesema: ((Allaah Huwatia imara wenye kuamini kwa kauli thabiti katika maisha ya dunia na Aakhirah)). Akasema: ((Hivyo atakapoulizwa kaburini; Nani Rabb wako, nini Dini yako, nani Rasuli wako? Atasema: Rabb wangu ni Allaah, Dini yangu ni Islaam na Rasuli wangu ni Muhammad, ametuletea dalili za wazi kutoka kwa Allaah, nikamuamini na nikamsadikisha. Ataambiwa: Umesema ukweli, umeishi kwa hayo, umefia kwa hayo na utafufuliwa kwa hayo)). [Atw-Twabariy (16: 596)] 

 

 

 

 

 

 

Share