Mazingatio Na Mafunzo Ya Hajj - Kutoka Kitabu Cha: Alhidaayah Katika Manaasik Za Hajj Na ‘Umrah

Mazingatio Na Mafunzo Ya Hajj 

Kutoka Kitabu Cha: Alhidaayah Katika Manaasik Za Hajj Na ‘Umrah

 

www.alhidaaya.com

 

 

Ukitafakari na kuzingatia yote yanayojiri katika safari ya Hajj, ukalinganisha na mafunzo yaliyomo katika Qur-aan na Sunnah yanayohusiana na Aakhirah, utapata mafunzo mengi. Allaah (سبحانه وتعالى) Ameanza Suwratul-Hajj kwa Aayah tukufu inayogusia hali itakavyokuwa Siku ya Qiyaamah:

 

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمْ ۚ إِنَّ زَلْزَلَةَ السَّاعَةِ شَيْءٌ عَظِيمٌ ﴿١﴾ يَوْمَ تَرَوْنَهَا تَذْهَلُ كُلُّ مُرْضِعَةٍ عَمَّا أَرْضَعَتْ وَتَضَعُ كُلُّ ذَاتِ حَمْلٍ حَمْلَهَا وَتَرَى النَّاسَ سُكَارَىٰ وَمَا هُم بِسُكَارَىٰ وَلَـٰكِنَّ عَذَابَ اللَّـهِ شَدِيدٌ ﴿٢﴾

 ((Enyi watu! Mcheni Rabb wenu. Hakika zilizala la Saa (Qiyaamah) ni jambo adhimu. Siku mtakapoiona (hiyo Saa) kila mnyonyeshaji atamsahau anayemnyonyesha, na kila mwenye mimba ataizaa mimba yake, na utawaona watu (kama) wamelewa, kumbe hawakulewa lakini ni adhabu ya Allaah kali)) [Al-Hajj: 1]

 

Mafunzo mengineyo:

 

1- Inamkumbusha Muislamu kuhusu safari ya Aakhirah na huwa na khofu kwamba, huenda ikawa ni safari yako ya mwisho, kwani utaagana na kufarikiana na ahli zako, jamaa, jirani, marafiki, mali yako na  makazi yako, na safari ya Aakhirah hali kadhalika huwa hivyo.

 

 

 

2-Kama unavyojiandaa safari ya kawaida kuandaa zawadi na vitu na mahitaji ya kukufikisha safarini na hasa safari hii ya Hajj ambayo Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:   

 

وَتَزَوَّدُوا فَإِنَّ خَيْرَ الزَّادِ التَّقْوَىٰ ۚ وَاتَّقُونِ يَا أُولِي الْأَلْبَابِ ﴿١٩٧﴾

 ((Na chukueni masurufu. Na hakika bora ya masurufu ni taqwa. Na nicheni Mimi enyi wenye akili!)) [Al-Baqarah: 197]

 

Hivyo basi, zingatia kwamba safari ya Aakhirah pia inahitaji kujiandaa kwa ‘amali njema ili iwe ni akiba yako ya Aakhirah.

 

 

 

3-Kama utakavyopata tabu katika kusafiri mji kwa mji au nchi kwa nchi, hali kadhalika kumbuka kwamba kuna tabu na mashaka ya safari ya Aakhirah ambayo ni nzito zaidi kwani safari hiyyo inahusiana na Sakaraat Al-Mawt, adhabu za kaburini, kufufuliwa, kuhesabiwa, kupimwa ‘amali katika mizani, kuvuka Asw-Swiraatw, na mtu akiwa ni muovu hatimaye ni adhabu za motoni (Tunajikinga kwa Allaah سبحانه وتعالى).   

 

 

 

4-Unapovaa nguo za Ihraam, kumbuka kafani (sanda) yako kwani hizo ni nguo mbili tu nyeupe zinazokutosheleza kufunikwa mwilini. Pia, kama zilivyokuwa nguo hizo ni nyeupe, unapaswa moyo wako uwe hali hiyo hiyo mweupe bila ya madoa meusi ya madhambi. Pia unapokuwa kwenye Ihraam unazuilika kutenda vitendo fulani usiharibu Ihraam yako, basi na iwe ukumbusho wa kujiepusha na maasi usiharibu Aakhirah yako.

 

 

 

5-Unaposema “Labbayka-Allaahumma Labbayka” unakusudia kumuitikia Rabb wako Mtukufu, hivyo kumbuka kwamba hivyo ndivyo inavyopasa kubakia hali yako daima kuitikia amri zote za Allaah (سبحانه وتعالى) na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم). 

 

 

 

6-Kuingia kwako katika Baytul-Haraam Makkah ambayo Allaah (سبحانه وتعالى) Ameijaalia kuwa ni amani kama Anavyosema:

 

 وَإِذْ جَعَلْنَا الْبَيْتَ مَثَابَةً لِّلنَّاسِ وَأَمْنًا

((Na (taja) Tulipoifanya Nyumba kuwa ni mahali pa kurejewa na watu na (pa) amani)) [Al-Baqarah: 125]

 

Ukumbuke umuhimu wa kupata amani Siku ya Qiyaamah, nayo haipatikani ila kwa juhudi zako duniani kufuata maamrisho ya Allaah (سبحانه وتعالى) na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم). Kumbuka ndugu Muislamu kwamba kujiepusha na kumshirikisha Allaah (سبحانه وتعالى) na kubakia katika Tawhiyd ndio jambo kuu litakalokupatia amani Siku hiyo kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

  الَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يَلْبِسُوا إِيمَانَهُم بِظُلْمٍ أُولَـٰئِكَ لَهُمُ الْأَمْنُ وَهُم مُّهْتَدُونَ ﴿٨٢﴾

((Wale ambao wameamini na hawakuchanganya iymaan zao na dhulma (ya kumshirikisha Allaah). Hao ndio watakaopata amani nao ndio walioongoka)) [Al-An’aam: 82]

 

 

 

7-Tafakari kwamba mamilioni ya watu wanajumuika huko, wanaume wakiwa wamevaa aina moja ya nguo, wakimuabudu Mola Mmoja kwa wakati mmoja, wakielekea Qiblah kimoja, hakuna tofauti kati yao; tajiri na masikini, mfalme na mtumwa, mweusi na mweupe. Basi zingatia kwamba huu ni uadilifu wa Allaah (سبحانه وتعالى) wa Dini hii tukufu na kwamba aliye mbora kati yetu ni mwenye taqwa zaidi. Pia zingatia kwamba Siku ya kufufuliwa itakuwa hali ni hiyo hiyo katika Ardhw Al-Mahshar (Ardhi ya kukusanywa viumbe wote Siku ya Qiyaamah)   

 

 

 

8-Al-Ka’bah ni nyumba ya kwanza duniani, Ameijaalia Allaah (سبحانه وتعالى) kuwa ni yenye baraka na Amejaalia kuweko katikati ya dunia nzima ili wana-Aadam wote waelekee huko wanapomuabudu kufuata Dini ya Uislamu ya baba yetu Nabiy Ibraahiym (عليه السلام), kwa hiyo Mitume na watu wote kabla yake walitakiwa waelekee hapo kuitekeleza ‘ibaadah ya Hajj. Basi zingatia kwamba Uislamu ni Dini ya watu wote anayeitaka, na si kwa ummah wa Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) pekee.

 

 

 

9-Tanabahi na kumbuka taadhima ya mwanamke aliyokirimiwa na Allaah (سبحانه وتعالى) kinyume na wanavyodhania makafiri kwamba mwanamke hana hadhi katika Uislamu. ‘Ibaadah ya As-Sa’-y imeanzishwa na Haajar (عليها السلام) mama yake Ismaa’iyl (عليه السلام) na tokea zama hizo mpaka Siku ya Qiyaamah mamilioni ya Waislamu wanaitekeleza ‘ibaadah hii tukufu. Pia, zingatia kwamba huo ulikuwa ni mtihani wa Haajar (عليها السلام) alipoachwa katika bonde lisilokuwa na wakazi wala chochote, lakini alitawakali kwa Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kuwa Ndiye Aliyemuamrisha Nabiy Ibraahiym (عليه السلام) amwache yeye na mwanawe sehemu hiyo peke yao.

 

 

 

10-Kuadhimisha Sunnah na kutambua kwamba amri yoyote ya Allaah (سبحانه وتعالى) na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) ina hikmah ndani yake, hata kama hatukutajiwa manufaa yake. Mfano tunapotakiwa kulibusu Al-Hajar Al-As-wad tunafanya hivyo kufuata amri bila ya kuitikadi kwamba jiwe hilo lina manufaa au dhara na ndipo ‘Umar bin Khatwaab(رضي الله عنه)  alisema alipolibusu:

 

إِنِّي  أَعْلَمُ أَنَّكَ حَجَرٌ لَا تَضُرُّ وَلَا تَنْفَعُ وَلَوْلَا أَنِّي رَأَيْتُ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يُقَبِّلُكَ مَا قَبَّلْتُكَ

Hakika mimi najua kwamba wewe ni jiwe hudhuru wala hunufaishi, na lau kama nisingelimuoma Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) anakubusu nisingelikubusu.” [Al-Bukhaariy, Muslim na wengineo]

 

 

 

11-Unapokunywa maji ya Zamzam, kumbuka neema za Allaah (سبحانه وتعالى) kwani hayo ni maji yenye baraka na ni poza ya kila maradhi ukitilia niyyah, na pia sababu ya kutakabaliwa mtu du’aa zake. Zingatia maajabu yake kwamba maji hayo yalitumiwa na watu tokea yalipoanza na watu wanayanywa wala hayamaliziki!   

 

 

 

12-Unaposimama ‘Arafah pamoja na Mahujaji wote siku moja, wakati mmoja, kila mmoja akiwa na hamasa ya kuomba du’aa na kuomba tawbah na maghfirah. Mkusanyiko huo mkubwa mno ni kiasi cha milioni tano na hapo kuna tabu na mashaka, basi zingatia kwamba itakuwaje Siku ya mkusanyo wa kufufuliwa viumbe vyote? Hali yao itakuwa kama alivyosema Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم): 

 

عَنْ عَائِشَةَ قَالَتْ سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ: ((يُحْشَرُ النَّاسُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ حُفَاةً عُرَاةً غُرْلًا)) قُلْتُ:  يَا رَسُولَ اللَّهِ النِّسَاءُ وَالرِّجَالُ جَمِيعًا يَنْظُرُ بَعْضُهُمْ إِلَى بَعْضٍ؟  قَالَ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((يَا عَائِشَةُ الْأَمْرُ أَشَدُّ مِنْ أَنْ يَنْظُرَ بَعْضُهُمْ إِلَى بَعْضٍ))

Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah (رضي الله عنها)  amesema: “Nilimsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: ((Watu watafufuliwa Siku ya Qiyaamah wakiwa hawana viatu, wakiwa uchi, hawakutahiriwa)). Nikasema: Ee Rasuli wa Allaah! Wanawake na wanaume watakuwa pamoja wakitazamana? Akasema (صلى الله عليه وآله وسلم): ((Ee ‘Aaishah! Hali siku hiyo itakuwa ngumu mno hadi kwamba hakuna atakayejali kutazamana!))  [Al-Bukhaariy, Muslim na wengineo]

 

 

13-Katika Jamaraat, kumbuka kwamba unatekeleza amri ya Allaah (سبحانه وتعالى) upate Radhi zake japokuwa huoni faida au hikmah ndani yake.     

 

 

 

14-Unapochinja, kumbuka utiifu wa Nabiy Ibraahiym (عليه السلام) na kutawakali kwake pamoja na mwanawe Ismaa’iyl (عليه السلام) waliposalimu wote kwa Allaah (سبحانه وتعالى) kutekeleza amri ya ndoto.

 

 

 

15-Utakapojivua katika Ihraam baada ya kujizuia makatazo yake, utakuwa umepata faida ya subira yako, na baada ya tabu umefarijika, basi furaha iliyoje kuitekeleza Hajj ipasavyo ukategemea malipo yake ya kufutiwa madhambi yote na kulipwa Jannah! Hali kadhalika utakapovuta subira duniani katika kutii amri za Mola wako, utafaulu Aakhirah.

 

 

 

16-Mwishowe utakaporudi kwa ahili zako, furaha iliyoje kukutana nao, basi kumbuka hapo kwamba kuna furaha kubwa zaidi ya kukutana nao katika Jannah. Na kumbuka kinyume chake kwamba ni khasara kubwa Siku ya Qiyaamah ambayo ni khasara ya nafsi na ahli  kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى): 

 

قُلْ إِنَّ الْخَاسِرِينَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُمْ وَأَهْلِيهِمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ أَلَا ذَٰلِكَ هُوَ الْخُسْرَانُ الْمُبِينُ ﴿١٥﴾

 ((Sema: “Hakika waliokhasirika ni wale waliokhasiri nafsi zao na ahli zao Siku ya Qiyaamah. Tanabahi!  Huko ndiko kukhasirika bayana)) [Az-Zumar: 15]

 

Share