Ndoa Ya Ahlul-Kitaab Inafungwa Msikitini Au Kanisani?


SWALI:

Asalaam alaykum,

Nimesoma kwenye maswali na nimeona kuwa kuoa mwanamke wa Kitabu ni halali ingawa si halali nzuri, lakini pia ni kuwa mwanamke anayemshirikisha mwenyezi mungu na mabaye atakuwa mlezi wa watoto wako na watajifunza kumshirikisha mwenyezi mungu pia. Swali ni hili je mwanamke huyo unamuoa kwa ndoa ipi? Mnafungaje ndoa hapo, Mnafungia kanisani au msikitini au mnafunga ndoa ya serikali ambayo kila mtu anabaki na dini yake. Je ndoa ya serikali inaswihi, mimi kaka yangu amemuoa mwanamke wa kitabu kwa ndoa ya kiserikali je yuko sahihi? Au anazini tu kuna ndoa hapo?

Wasalaam alaykum

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)  Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allahu 'anhum jamiy'an) na watangu wema mpaka Siku ya Qiyaamah.

 

Shukrani kwa swali lako hilo ambalo limekutia wewe katika wasiwasi na kuwa na dukuduku. Hakika ni kuwa ndoa ya Kiislamu inaweza kufanyika sehemu yoyote ambayo inakubaliwa katika Uislamu na si lazima ifanywe msikitini. Inaweza kufanywa Msikitini, nyumbani, kwenye ukumbi na kadhalika lakini haiwezi kufanyika katika Kanisa, Hekalu au Sinagogi kwa kuwa haijawahi kufanyika hivyo katika historia ya Kiislamu yote. Sehemu ya kufanyia si miongoni mwa masharti ya kukubalika kwa nikaah.

Masharti ya ndoa ya Kiislamu ni kama yafuatayo:

    1.  Kukubali bila ya kutenzwa nguvu kwa mume na mke.

    2. Idhini ya walii k.m. baba, ndugu wa kiume, babu, n.k.

    3. Mashahidi 2 waadilifu.

    4. Mume kutoa mahari kumpatia mkewe.

   5. Sigha (namna, maneno) ya kuozesha ni lazima iwe kwa njia ya kwamba mwenye kuozesha (walii au aliyepewa ruhusa naye kufanya hivyo) awe ni mwenye kusema: Nimekuozesha wewe Fulani binti Fulani kwa mahari yake kadhaa, na mume naye awe ni mwenye kujibu kuwa nimekubali kumuoa …..

 

Ikiwa Nikaah hiyo itafanywa serikalini mara nyingi masharti haya tuliyoyataja huwa hayakamiliki na hasa akiwa mke si Muislamu. Na ikiwa masharti hayatokamilika basi ndoa yenyewe itakuwa haijaswihi. Ikiwa mke mwenye kutaka kuolewa si Muislamu (Ahlul Kitaab), hata hivyo ndoa inafaa ifanywe Msikitini au nyumbani kwani mume ndiye mwenye majukumu na wala sio mke.

Na Allah Anajua zaidi           

 

 

Share