Makosa Yanayofanywa Baada Ya Hajj: Kutoka Kitabu Cha Alhidaayah Katika Manaasik Za Hajj Na ‘Umrah

Makosa Yanayofanywa Baada Ya Kumaliza Hajj na Kurudi Nyumbani

(Kutoka Kitabu Cha Alhidaayah Katika Manaasik Za Hajj Na ‘Umrah)

www.alhidaaya.com

 

 

Muislamu anapomaliza Hajj anapaswa kuthibitika katika ‘Ibaadah zake. Kubakia katika istiqaamah (kuthibitika) ni dalili ya kutakabaliwa Hajj yako. Aayah na Hadiyth kadhaa zimetaja kuhusu jambo hili; baadhi ni hizi zifuatazo:

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 وَاعْبُدْ رَبَّكَ حَتَّىٰ يَأْتِيَكَ الْيَقِينُ ﴿٩٩﴾

((Na mwabudu Rabb (Mola) wako mpaka ikufikie yakini (mauti))[1]

 

Ndugu Muislamu usije kuwa mfano wa yule mwanamke wa Makkah aliyekuwa akisonga uzi wake tokea asubuhi hadi jioni kisha alikuwa anaufumua wote na kazi yake yote ikawa ni ya bure. Amemtaja Allaah (سبحانه وتعالى) katika kauli Yake:

 وَلَا تَكُونُوا كَالَّتِي نَقَضَتْ غَزْلَهَا مِن بَعْدِ قُوَّةٍ أَنكَاثًا

((Na wala msiwe kama yule mwanamke aliyezongoa uzi wake vipande vipande baada ya (kuusokota na) kuwa mgumu))[2]

Rasuli  (صلى الله عليه وآله وسلم) ametupa nasaha kuhusu kuthibitisha iymaan na ‘amali zetu:

 عَنْ أبي عَمْرَةَ سُفْيَانَ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ (رضي الله عنه)  قَالَ: قُلْتُ يَا رَسُولَ اللَّهِ قُلْ لِي فِي الإسْلاَمِ قَوْلاً لاَ أَسْأَلُ عَنْهُ أَحَدًا غَيْرَكَ)) قَالَ: ((قُلْ آمَنْتُ بِاللَّهِ  ثُمَّ َاسْتَقِمْ)) رواه مسلم

Imepokelewa kutoka kwa Abu ‘Amrah Sufyaan bin ‘Abdillaah (رضي الله عنه) amesema: Nilisema: “Ee Rasuli wa Allaah! Niambie neno katika Uislamu ambalo sitomuuliza yeyote isipokuwa wewe.” Akasema: ((Sema: Nimemwamini Allaah kisha uwe na istiqaamah [msimamo]))[1]

 

Jitahidi kuthibitika katika ‘amali za ‘ibaadah japo kwa kiasi kidogo ambacho cha uwezo wako ili uweze kuendeleza ‘ibaadah zako bila ya kuchoka ubakie katika istiqaamah. Hivyo ndivyo Anavyopenda Allaah (سبحانه وتعالى) kama alivyosema Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم):

(( أَحَبُّ الأعْمَالِ إِلَى اللهِ أَدْوَمُهَا وَإِنْ قَلَّ))  متفق عليه

 ((Vitendo Anavyovipenda Allaah zaidi (kuliko vyote) ni vile vinavyodumishwa japokuwa ni kidogo)[2]

 

Yanayofahamika Sivyo Na Yanayotendeka Kimakosa Baada Ya Kumaliza Hajj Na Kurudi Nyumbani

 

  •  Baadhi ya Mahujaji wanaporudi makwao, hufanyiwa sherehe, mialiko ya watu na karamu kwa ajili ya kupongezwa. Wengine husomewa Mawlid. Hakuna uthibitisho wowote kwamba Mahujaji wafanyiwe jambo lolote lile. Kufanya hivyo ni uzushi katika Dini. Hakuna lolote lipasalo kufanywa ila tu inaruhusiwa jamaa wa karibu na marafiki kumtembelea aliyehiji nyumbani kwake kumpongeza na kumuombea.

 

  • Kuwaita waliohiji ‘Haaj fulani’ au ‘Haajah fulani’. Haipasi kwani hivyo si katika Sunnah na haipasi kujitakasa mtu kwa sifa ya ‘amali aliyoitenda.

 

  • Kudhania kwamba mtu anaporejea Hajj anakuwa na makarama kwa muda wa masiku arubaini, na hivyo watu hukimbilia kumtembelea kupata baraka zake.

 

  •  Kuchinja kwa ajili Mahujaji kabla ya kuingia nyumbani kwake.

 

  • Wengine hurudia katika maasi na hivyo ni kuharibu juhudi zao za Hajj.

 

Subhaanaka-Allaahumma wa bihamdika, nash-hadu an laa ilaaha illa Anta, nastagh-firuka wa natuwbu Ilayka wal-hamduliLlaahi Rabbil-‘aalamiyn, wa-Swalla-Allaahu ‘alaa Nabiyyinaa Muhammad wa ‘alaa aalihi wa swahbihi  wa sallam.

 

 

 

 

 

[1] Muslim.

[2] Al-Bukhaariy na Muslim.

Share