Kutotimiza Hijaab Mbele Ya Mume Aliyempa Talaka

 

 

SWALI

      Assalam Aleykum Warahmatullahi wabarakatu.

Namshukuru M/Mungu kutujaalia kupata nafasi ya kuuliza maswali kwa lugha yetu na tukapata masheikh wanaoweza kutujibu kwa lugha yetu. Al-Hamdulillah.

Naomba kuuliza swali kuhusu Talaka iliyomfika ndugu yangu wa Kiislam.

Ndugu yangu mmoja wa Kiislam kaachana na mumewe kwa sababu ya matatizo ya familia. Hivi sasa bado yuko kwenye eda, japokua wameachana lakini bado wanapendana, na mwanamme bado anakwenda kwake na anakaa kichwa wazi mbele yake, wanafanya kila kitu kama kukumbatiana lakini sio kitendo chenyewe.
Suala ni kua jee inasihi kuishi hivi kwa sababu bado wapo kwenye eda? Mwenyeenzi Mungu akujazeni kheri kwa jitihada yenu..... Ameen

 


JIBU:

AlhamduliLLaah - Sifa njema zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

Twashukuru kwa swali lako hili kuhusu hayo uliyoyaona. Na tufahamu ya kuwa matatizo hayakosekani katika unyumba na ndio tukahimizwa sana katika Dini yetu kuvumiliana. Hadi ifikie kuwe vigumu sana kukaa pamoja ndio hapo talaka itolewe.

Sheria ya Kiislamu, bado inataka wanandoa hawa warudiane na kuwe na suluhu na hivyo kurudiana na kukaa pamoja. Ikiwa wameachana talaka ya kwanza au ya pili bado wanaweza kurudiana, na ndio sheria ikaweka kuwa lazima mke awe ni mwenye kuishi katika nyumba ya mumewe na hafai yeye kutoka. Anaweza kutolewa tu katika nyumba hiyo ikiwa atakuwa amefanya uchafu (uzinzi) ulio dhahiri kabisa. Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:

 “Msiwatoe katika nyumba zao, wala wasitoke wenyewe, ila wakifanya jambo la uchafu uliowazi. Hiyo ndiyo mipaka ya Allaah, msiikiuke. Na mwenye kuikiuka mipaka ya Allaah, basi amejidhulumu nafsi yake. Hujui; labda Allaah Ataleta jambo jengine baada ya haya (65: 1).

Mume anafaa kumtekelezea mambo yote yake (mkewe) kama chakula, mavazi, matibabu, malazi, na kadhalika. Hivyo, kisheria mke bado ni wa huyo mume mpaka eda imalizike.

Kwa hiyo, hakuna makosa wala ubaya kwa mke kukaa kichwa wazi wala kumkumbatia mumewe. Lakini wakati watafanya mapenzi (jimai) baina yao itakuwa mume tayari amemrudia mkewe. Pia ni vyema kwa familia na marafiki kuingilia kati na kuleta suluhu baina yao ili wanandoa hawa warudiane na waendelee na maisha yao.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share