Mume Hana Bashasha Hatimizi Wajib Wake

SWALI:

Assalam Allaykum, Nina swali langu moja zito ambalo linanikera sana kwenye moyo wangu... Swala lenyewe ni hivi mimi nina mume na sasa tunaishi kwa miaka 3 na tuna watoto wawili M/Mungu atuwekee Amin. Sasa huyu mwenzangu ni Mtu Anaimani Sana na Roho Nzuri na mtu ambaye anafuata mambo ya dini si mtu wa anasa. Lakini ana tabia moja ambayo mimi inanichukia na nishachoka nayo nikuwa tuko ndani ya nyumba yetu yeye anakuwa simtu wakuzungumza, yeye hasemi kusema yake ni mara moja tu umemuuliza swali basi na jengine ni tukilala mimi na yeye anakuwa hataki hata kuguswa anailekeya huko mpaka asubuhi...  sasa mimi binafsi nilikuwa nataka kusaidiwa kiwamawazo nifanye vipi mpaka ajerekebishe. Wabilahi Tafiq

 

 


 

JIBU

Sifa zote njema Anastahiki Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum)  na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani dada yetu kwa suali lako hilo nyeti sana na tatizo kubwa kwa wanandoa. Lakini hapa nakumbushia tena kuwa tumekuwa tukikariri kila wakati kuwa ni muhimu wenye matatizo ya ndoa watueleze wapo wapi ili tuweze kuwasaidia kwa karibu zaidi. Ni sikitiko kuwa hilo halijatekelezwa mpaka sasa. Hivyo, inakuwa shida kwetu kuweza kumsaidia kiuhakika isipokuwa ni kutoa nasiha za juu juu.

Tatizo la ndoa mara nyingi hupatikana kwa wanandoa wawili lakini kwa mwenye dini haliwi ni lenye kuwa katika kiwango hicho. Mtu mwenye dini hatakuwa ni mwenye kufanya anavyofanya mume wako. Ikiwa labda hakupendi basi anakupatia talaka kwa wema kama mulivyooana kwa wema. Kugeuka upande mwengine katika kitanda hakuruhusiwi isipokuwa unapokuwa na makosa ndio sheria inakubali mume kufanya hivyo alivyofanya.

Suluhisho kwa tatizo hili ni dogo ni wewe kama mke ukakaa na mumeo na kuzungumza naye kinaganaga kuhusu tatizo hilo na kutazama njia ya kutatua. Hayo si maisha ya mume na mke kukaa pamoja. Ni ima mume awe hakutaki au wewe humtaki. Tatizo hili ikiwa halikutatuliwa kwa mazungumzo hayo baina yenu, Qur-aan inatufahamisha kuwa muwaite wazazi wenu au jamaa zenu wasikilize matatizo yenu na wayatafutie suluhisho. Hayo matatizo yazungumzwe na kutafutwe suluhisho la kudumu. Kama njia hiyo imeshindikana basi kutakuwa hakuna jingine la kufanywa isipokuwa kutoka katika ndoa hiyo. Tunakuombea isifike daraja hiyo bali kupatikane suluhisho na mrudi katika bashasha na furaha ya uanandoa. Tunakuombea Du’aa ukanyukwe na matatizo hayo inshaAllaah.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share