Mume Anaithamini Internet Kuliko Mke

 SWALI:

 Assalam  aleykum .kwanza kabisa  ningependa kuwashukuruni. swali  ni kama  lifuatavyo mimi nimeolewa  lakini mume wangu hana  time na  mimi   hata  kwenye tendo la ndoa  tunafika  kukaa    mpaka  miezi  mitatu au zaid bila ya  kuingiliana  na  yeye  anatumia usiku  mwingi kwenye internet   na  mimi nishamwambia sipendo mwendo wake huo  lakini jibu lake ni  kuwa yeye  hawezi kuishi  bila ya internet anaweza kuishi bila ya  mimi  lakini sio  bila  ya internet kwa hiyo mimi  mwenyewe najiona  mimi kwake yeye sina thamani    kuliko ya hiyo internet  je ndoa hii  inakubalika  shekhe? 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani kwa swali lako kuhusu mume kuthamini mtandao (internet) kuliko wewe.

Hakika hili ni tatizo sugu katika jamii yetu na huenda mtu akajiuliza ikiwa mume anathamini kitu kingine chochote kuliko mke ingekuwa bora kwake kutoingia katika ndoa.

Ni vyema ieleweke kuwa ni wajibu juu ya mume kumuingilia mkewe japo kuwa mara moja katika kila miezi minne iwapo atashindwa kiasi cha kumtosha.

Ibn Hazm amesema:

“Ni faradhi kwa mume kumuingilia mkewe kama hana udhuru wowote ule na uchache wake ni kumuingilia japo mara moja katika kila twahara ikiwa ataweza vyenginevyo mume huyo huwa amemuasi Allaah amekwenda kinyume na amri ya Allaah yenye kusema:

“Na wanakuuliza juu ya hedhi. Waambie, huo ni uchafu. Basi jitengeni na wanawake wakati wa hedhi. Wala msiwaingilie mpaka watwaharike. Wakisha twahirika basi waendeeni alivyokuamrisheni Allaah .” Al Baqarah 2: 222.”

Na pia inafaa ieleweka kuwa ni wajibu juu ya mume kumuingilia mkewe katika kila siku nne japo mara moja, na hii ndio uadilifu; kwani mtu ameruhusiwa kuoa wake wanne hivyo inaruhusiwa kumuingilia angalau mara moja katika siku nne au zaidi kulingana na mahitaji ya mke; na hivyo ndivyo ilivyohukumiwa wakati wa ‘Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa: katika kila siku nne usiku mmoja anatakiwa mume amuingilie mkewe kwa kukadiria kuwa ana wake wanne.

Pia ni vyema ieleweke kuwa imethibiti katika Sunnah kuwa tendo la ndoa baina ya mume na mke ni Sadaqah ambayo mtu hupata thawabu na kwa tendo hilo kama vile anapopata dhambi kwa tendo kama hilo ikiwa amelifanya kwa asiyekuwa mkewe.

Asili ya kushauriwa na kupendekezewa mtu kuoa ni kutaka kupatikane kuishibisha nafsi na matamanio ya kijinsia hivyo basi kama mtu hana shauku na wanawake/ mwanamke basi ni vyema asioe na kama atapenda kuoa basi ni vyema amjulishe huyu mwanamke kuwa yeye anapenda kuwa na mke lakini hana uwezo wa kumtimizia tendo la ndoa kwa sababu alizonazo ambazo ni za kishari’ah.

Sasa aliyeamua kuoa aelewe kuwa ni wajibu wake kumtimizia mkewe mahitajio yake na hasa hasa hili hitajio la tendo la ndoa; na kwa mke na mume  ‘kufikia  kukaa    mpaka  miezi  mitatu au zaidi bila ya  kuingiliana’  hili huenda likawa katika yenye kueleweka kama ni kiapo –mume kula yamini kwa Allaah kuwa hatomuingilia mkewe kwa kipindi kinachozidi miezi minne- japo kuwa wakati huo hakuna kiapo hicho lakini kuna chenye kuonyesha na kupelekea kueleweka kuwa kuna hali kama hiyo; hivyo basi hukumu yake ni kama hivyi

“Kwa wanaoapa kuwa watajitenga na wake zao, wangojee miezi minne….” Al-Baqarah2: 226.

Hivyo basi iwe huyo mume hakula kiapo lakini muda ambao hakukutimizia tendo la ndoa ni kama huo uliosema; ‘je ndoa hii inakubalika’ ndugu yetu utahitaji kufikisha madai yako mbele ya Qaadhi, na huyo Qaadhi atatoa hukumu ima amtake arudi akuingilie au akuache bila ya kukuletea madhara na ukaingia katika uchafu:

“ ..Wakirejea basi Allaah hakika ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu….” al-Baqarah 2: 226.

Hivyo basi huyo mumeo kwa kuwa ameacha kukuingilia kipindi cha kiapo bila ya kiapo naye atachukuliwa kama mwenye kuapa, ima akuingilie au akuache endapo utatoa madai yako haya mbele ya Qaadhi.

Katika yenye kusikitisha ni kama haya kuwa, ‘yeye  anatumia usiku  mwingi kwenye internet’   hili lawezekana likawa na sababu au wakati mwengine halina sababu bali huwa ni kama hivi ulivyosema,  ‘yeye  hawezi kuishi  bila ya internet’

Je, ndugu yetu yawezekana kukawa na sababu za upande wako; yawezekana hujitayarishi kwa ajili ya mumeo, yawezekana pia ukawa kila wakati wewe pia uko katika simu na kadhalika, yawezekana pia ukawa hujipambi hata siku moja ili avutike nawe, yawezekana ukawa humfanyii cha kumpelekea kuachana na huyo mke wake wa pili ambaye ni internet ambaye yeye hawezi kumkosa; nini umejaribu katika kuweza kumpelekea kumsahau huyo mkewe wa pili na kukujia wewe kwa mapambo yako na uzuri wako?

Katika yenye kusikitisha ni kuwa wengi katika Waislamu huoa si kwa kuwa ni jambo la ‘Ibaadah bali ni katika mambo ya mila na utamaduni; ndoa wengi hudhania kuwa ni desturi na kawaida za jamii; hivyo huona kuwa baada ya kumaliza nyumba kama anayo na kununua kitanda na viti na jiko na kadhakila kilichobakia katika vifaa vya nyumba ili ionekane kama nyumba za wengine. Kununua huko -mke- hivyo ndio akawa anaona kuwa yeye katimiza vifaa na vyombo vya nyumba na hakuna katika hivyo vifaa vyenye thamani ndio akawa ‘aweza kuishi bila ya wewe – mimi -  lakini sio  bila  ya internet.

Nini anatafuta katika hiyo internet? Jiulize na umuulize? Haelewi kuwa macho hayatakiwi kuangalia ila yaliyo halali kwake? Wewe uliwahi kumueleza hayo?

Umesema, ‘najiona mimi kwake yeye sina thamani kuliko ya hiyo internet’ Ndugu yetu, unayo thamani kwake na kwa wenzake, lakini hujatumia hicho chenye kuthibitisha thamani yako; na je, hali hii au jambo hili limeanza lini? Au ni jambo la karibuni,na kama la karibuni basi yawezekana kuwaka na sababu kama tulivyoeleza kwanza na kama hali ni ya kawaida basi ushauri ndio kama tulivyokueleza.

Tafadhali bonyeza kiungo kifuatacho upate maelezo zaidi:

Mume Anakesha Katika Internet Hampi Mke Haki Yake - Mke Afanyeje?

Twamuomba Allaah Aliyetukuka Akutoe ufumbuzi wa shida hiyo na muweze kuishi na mumeo kwa njia iliyo nzuri.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share