07-Swalaah – Kuwajibika Na Fadhila Zake: Adhabu Za Mwenye Kuacha Swalah

Swalaah – Kuwajibika Na Fadhila Zake

 

07-Adhabu Za Mwenye Kuacha Swalaah

 

Alhidaaya.com

 

  

Baadhi ya Waislamu huwa hawatilii mkazo kabisa Swalaah. Kuna wanaozipuuza kwa kutokuziswali kwa wakati wake, na kuna wasioswali kabisa. Na kwa vile Swalaah ni msingi wa Dini, na ni ‘ibaadah tukufu kabisa, basi wanapozidharau na kutokutimiza kuziswali, malipo yake ni mabaya mno ya kuweza kumfikisha mtu motoni. Adhabu kadhaa zimetajwa katika Qur-aan na Sunnah zikiwemo:

 

 

1-Wanaoacha kuswali watakutana na adhabu Motoni: Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) :

 

فَخَلَفَ مِن بَعْدِهِمْ خَلْفٌ أَضَاعُوا الصَّلَاةَ وَاتَّبَعُوا الشَّهَوَاتِ ۖ فَسَوْفَ يَلْقَوْنَ غَيًّا ﴿٥٩﴾

Wakafuata baada yao waovu, walipoteza Swalaah na wakafuata matamanio; basi watakutana na adhabu motoni. [Maryam: 59]

 

 

'Abdullaahi bin Mas'uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema kuhusu “watakutana na adhabu motoni.” ina maana ni "bonde la moto lililokuwa refu lenye chakula kichafu kabisa" [At-Twabariy 18:218]

 

 

 

2-Makazi ya wasioswali yatakuwa ni motoni na watakapoulizwa na wakaazi wa Jannah sababu ya kuwafikisha motoni,  watakiri kuwa sababu mojawapo ni kwa sababu ya kutokuswali. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ رَهِينَةٌ﴿٣٨﴾

Kila nafsi iko katika rehani kwa yale iliyoyachuma.

 

إِلَّا أَصْحَابَ الْيَمِينِ﴿٣٩﴾

Isipokuwa watu wa kuliani.

 

 

فِي جَنَّاتٍ يَتَسَاءَلُونَ﴿٤٠﴾

Katika Jannaat wanaulizana.

 

 

عَنِ الْمُجْرِمِينَ﴿٤١﴾

Kuhusu wahalifu.

 

 

مَا سَلَكَكُمْ فِي سَقَرَ﴿٤٢﴾

 (Watawauliza): “Nini kilichokuingizeni katika motoni?”

 

 

 

قَالُوا لَمْ نَكُ مِنَ الْمُصَلِّينَ﴿٤٣﴾

Watasema: “Hatukuwa miongoni mwa wanaoswali. [Al-Mudath-thir: 38-43]

 

 

 

Hayo yatakuwa ni malipo yao kwa sababu waliridhika na maisha ya dunia na anasa zake hadi wakasahau kama kuna Rabb Aliyewaumba Akawaamrisha wamuabudu.

 

 

 

3-Wanaocha kuswali watapata adhabu ya moto kwa sababu kupuuza Swalaah zao kwa kutokuziswali ipasavyo; ima kwa kuswali na kuacha, au kutokuziswali kwa wakati wake. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

فَوَيْلٌ لِّلْمُصَلِّينَ ﴿٤﴾

Basi Ole kwa wanaoswali ...

 

 

الَّذِينَ هُمْ عَن صَلَاتِهِمْ سَاهُونَ ﴿٥﴾

Ambao wanapuuza Swalaah zao. [Al-Maa'uwn: 4-5]

 

 

 

 

Neno 'wayl'  limetajwa mara kadhaa katika Qur-aan kuwa ni adhabu iwapatayo watu kwa sababu mbalimbali za maasi; mojawapo ikiwa ni kuacha Swalaah. Ni neno la kutisha lenye maana ya kudhalilishwa, kuadhibiwa na kungamizwa.  

 

 

 

4-Adhabu kali pia itawafikia wenye kuacha kuswali ambao hata unapowapa nasaha ya kuwakumbusha umuhimu wa kuswali n.k. hawasikii wala hawaogopi adhabu zake. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَإِذَا قِيلَ لَهُمُ ارْكَعُوا لَا يَرْكَعُونَ﴿٤٨﴾

Na walipokuwa wakiambiwa “Rukuuni (mswali),” hawakuwa wakirukuu.

 

 

وَيْلٌ يَوْمَئِذٍ لِّلْمُكَذِّبِينَ﴿٤٩﴾

Ole Siku hiyo kwa wenye kukadhibisha. [Al-Mursalaat: 48-49]

 

 

 

Ukaidi huo ni hapa duniani, lakini siku ya Qiyaamah watatamani wainamishe vichwa vyao wamsujudie Rabb wao lakini Hayhaata! Hayhaata! (Hayawi! Hayawi!) Hawatoweza Abadan kuinamisha vichwa vyao: Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 

يَوْمَ يُكْشَفُ عَن سَاقٍ وَيُدْعَوْنَ إِلَى السُّجُودِ فَلَا يَسْتَطِيعُونَ﴿٤٢﴾

Siku utakapofunuliwa Muundi na wataitwa kusujudu lakini hawatoweza.

 

 

 

خَاشِعَةً أَبْصَارُهُمْ تَرْهَقُهُمْ ذِلَّةٌ ۖ وَقَدْ كَانُوا يُدْعَوْنَ إِلَى السُّجُودِ وَهُمْ سَالِمُونَ﴿٤٣﴾

Macho yao yatainama chini, udhalilifu utawafunika. Na hali walikuwa wakiitwa wasujudu (kuswali duniani) walipokuwa wazima wa afya. [Al-Qalam: 42-43]

 

 

 

5-Vile vile asiyeswali atafufuliwa na watu waovu kabisa siku ya Qiyaamah kama alivyosema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

 عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عَمْرٍو بن العاص عَنِ النَّبِيِّ صلى الله عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنَّهُ ذَكَرَ الصَّلاةَ يَوْمًا فَقَالَ:  ((مَنْ حَافَظَ عَلَيْهَا كَانَتْ لَهُ نُورًا وَبُرْهَانًا وَنَجَاةً يَوْمَ الْقِيَامَةِ، وَمَنْ لَمْ يُحَافِظْ عَلَيْهَا، لَمْ يَكُنْ لَهُ نُورٌ وَلا بُرْهَانٌ وَلا نَجَاةٌ وَكَانَ يَوْمَ الْقِيَامَةِ مَعَ قَارُونَ وَفِرْعَوْنَ وَهَامَانَ وَأُبَيِّ بْنِ خَلَفٍ)) أخرجه الإمام أحمد في مسنده

 

Kutoka kwa 'Abdullaah bin 'Amru ibn Al-'Aaasw (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba siku moja Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitaja kuhusu Swalaah akasema: ((Atakayeihifadhi atakuwa na nuru na uongofu, na kufuzu siku ya Qiyaamah, na asiyeihifadhi hatokuwa na nuru wala uongofu wala kufuzu, na siku ya Qiyaamah atakuwa pamoja na Qaaruwn, Fir'awn, Haaman na Ubayy bin Khalaf)) [Musnad Ahmad ikiwa na isnaad Swahiyh]

 

 

Katika kuifasiri Hadiyth hii, Ibn Al-Qayyim Al-Jawziy (Rahimahu Allaah) amesema: “Mwenye kuacha Swalaah huwa ameshughulika na mojawapo kati ya yafuatayo: Ima atakuwa imemshughulisha mali yake au ufalme wake au cheo chake au biashara zake. Yule aliyeshughulika na mali yake, atafufuliwa pamoja na Qaaruwn, na aliyeshughulika na ufalme wake, huyo atakuwa pamoja na Fir'awn, na aliyeshughulika na cheo chake atakuwa pamoja na Haaman na yule aliyeshughulika na biashara zake (akaacha kuswali), huyo atakuwa pamoja na Ubayy bin Khalaf.”

 

Ee ndugu Muislamu usiyeswali au kupuuza Swalaah yako, je haujafika wakati wa kukhofu adhabu hizi kali za Rabb wako? Je, utaridhika kufufuliwa na watu waovu kabisa badala ya wapenzi wako kwa sababu tu ya kushughulika na dunia na kuacha ‘Ibaadah ambayo hata dakika kumi haikuchukui kuitimiza?

 

 

 

Share