01-Madhara Ya Ghiybah: Maana Ya Ghiybah, Tofauti Baina Ya Ghiybah, Buhtaan Na Ifk

Madhara Ya Ghiybah (Kusengenya) Na An-Namiymah (Kufitinisha)

 

01- Maana Ya Ghiybah, Tofauti Baina Ya Ghiybah, Ifk Na Buhtaan

 

 

Maana ya Ghiybah:

 

Kilugha:  Kila kilichokuwa hakipo mbele yako. Na imeitwa Ghiybah kwa kutokuweko anayetajwa wakati anapotajwa na wengine. 

 

Kishariy’ah: Kumsengenya mtu asiyekuwepo kwa mambo ambayo atachukia kuyasikia. Na maana yake ametujulisha Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipowauliza Maswahaba:

 

 

(( أتدرون ما الغيبة؟))  قالوا: الله ورسوله أعلم؛ قال: (( ذكرك أخاك بما يكره  ...))

((Je mnajua maana ya  Ghiybah?)) Wakasema: Allaah na Rasuli Wake wanajua. Akasema: ((Kumsema ndugu yako anayoyachukia …..))  [Al-Bukhaariy]

 

 

Imaam An-Nawawiy amesema kuhusu Ghiybah: "Kumsema mtu nyuma yake kwa yale anayoyachukia."

 

Akaendelea kusema: "Kumsema mtu kwa anayoyachukia ikiwa yanayohusu mwili wake, au Dini yake, au dunia yake, au nafsi yake, au umbile lake au tabia yake, au mali yake, au wazazi wake, au mtoto wake, au mke wake, au mtumishi wake, au nguo yake, au nyendo (shughuli) zake na mengineyo yote yanayomhusu, ikiwa ni kumsema kwa kauli, au kwa ishara au kukonyeza, hata kama kusema neno la kumkejeli.”

  

Maana nyingine ya Ghiybah ni kama alivyosema Ibn   Taymiyyah (Rahimahu Allaah): "Wengine wanasengenya kwa kauli zao za kustaajabu kama kusema: “Nimeshangazwa na fulani vipi hafanyi kadhaa na kadhaa.” Na wengine wanaosengenya moyoni (kwa niyyah) kwa kunena: “Masikini fulani amenisikitisha anayoyatenda.”

 

Tofauti Baina ya Ghiybah na Buhtaan:

 

Buhtaan ni kumzulia mtu jambo lisilokuwa la kweli. Ametubainishia Rasuli wa Allaah   (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) tofauti baina ya Ghiybah na Buhtaan katika Hadiyth ifuatayo:

 

 

 عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضي الله عنه ، أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَال:   (( أَتَدْرُونَ مَا الْغِيبَةُ ؟ ))  قَالُوا : اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَعْلَمُ ، قَالَ  ((ذِكْرُكَ أَخَاكَ بِمَا يَكْرَهُ )) ، قِيلَ : أَفَرَأَيْتَ إِنْ كَانَ فِي أَخِي مَا أَقُولُ ؟ قَالَ  ((إِنْ كَانَ فِيهِ مَا تَقُولُ فَقَدِ اغْتَبْتَهُ ، وَإِنْ لَمْ يَكُنْ فِيهِ فَقَدْ بَهَتَّهُ))    أخرجه مسلم  

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba aliuuliza Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Je mnajua maana ya  Ghiybah?)) Wakasema: Allaah na Rasuli Wake wanajua. Akasema: ((Ni kumtaja ndugu yako kwa jambo analochukia)). Akaulizwa: Hebu nieleze, iwapo ndugu yangu anayo yale niyasemayo? Akasema: (Ikiwa analo hilo usemalo basi umeshamsengenya, na ikiwa hana hilo usemalo basi umeshamzushia uongo)) [Muslim]

 

Vile vile Hadiyth ifuatayo inaelezea:

 

 

عبد الله بن عمرو أنهم ذكروا عند رسول الله صلى الله عليه وسلم رجلاً فقالوا: لا يأكل حتى يُطعم، ولا يَرحل حتى يُرحل، فقال النبي صلى الله عليه وسلم: ((اغتبتموه)) فقالوا: يا رسول الله: إنما حدثنا بما فيه قال: ((حسبك إذا ذكرت أخاك بما فيه))  المحدثالألباني -  المصدر السلسلة الصحيحة

Kutoka kwa 'Abdullaah bin 'Amru (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba walimtaja mtu mmoja mbele ya Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wakasema: "Hali hadi alishwe, wala haendi hadi apelekwe." Akasema Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ((Mmemsengenya)).  Wakasema: "Ee Rasuli wa Allaah  wa Allaah, tumehadithia ya kweli aliyonayo." Akasema: ((Inakutosheleza kumsema ndugu yako kwa aliyonayo)) [Al-Albaaniy   katika Silsilatus-Swahiyhah]

 

 Na kutoka katika Qur-aan Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

وَالَّذِينَ يُؤْذُونَ الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ بِغَيْرِ مَا اكْتَسَبُوا فَقَدِ احْتَمَلُوا بُهْتَانًا وَإِثْمًا مُّبِينًا ﴿٥٨﴾

Na wale wanaowaudhi Waumini wa kiume na Waumini wa kike bila ya kuwa wamechuma kosa, basi kwa yakini wamejibebea usingiziaji mkuu wa dhulma na dhambi bayana. [Al-Ahzaab: 58]  

 

Vile vile katika kisa cha Ifk (kuzuliwa) Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) Anasema Allaah   (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 وَلَوْلَا إِذْ سَمِعْتُمُوهُ قُلْتُم مَّا يَكُونُ لَنَا أَن نَّتَكَلَّمَ بِهَـٰذَا سُبْحَانَكَ هَـٰذَا بُهْتَانٌ عَظِيمٌ ﴿١٦﴾

Na kwa nini mlipoisikia (kashfa ya kusingiziwa) msiseme: “Haitupasi sisi tuzungumze haya; Subhaanak! (Utakasifu ni Wako) huu ni usingiziaji wa dhulma mkubwa mno!”  [An-Nuwr: 16]    

 

Uzushi unaweza kuwa kwa Ghiybah  (kumsengenya nyuma yake mtu) au mbele yake. 

 

Hasan Al-Baswriy kasema: "Ghiybah ni tatu; zote zimo katika Qur-aan. Ghiybah (kusengenya) ifk (usingiziaji, udaku, umbeya) na buhtaan (kusingizia yasiyo kweli).

 

Ghiybah ni kumsengenya ndugu yako aliyonayo. Ama  Ifk ni kusema unayoyasikia (ya usingiziaji, umbeya) na ama buhtaan ni kusingizia yasiyo kweli."

 

Ghiybah hakika ni hatari mno kwa Muislamu kwani     ghiybah zinamharibia mtu ‘amali zake na hatimaye akute patupu katika miyzaan yake ya ‘amali njema Siku ya Qiyaamah. Hatari hii ni kwa yeyote yule hata kama mtu ni mswalihina au ni mtendaji  wema kwa wingi!    

 

 

 

 

Share