02-Madhara Ya Ghiybah: Kutunza Ulimi

Madhara Ya Ghiybah (Kusengenya) na An-Namiymah (Kufitinisha)

 

02- Kutunza Ulimi

 

 

 

Kila binaadamu ana Malaika wawili; mmoja kuliani mwake, na kushotoni mwake. Na kazi zao ni kuandika mema ya mtu na maovu yake; ikiwa ni makubwa au madogo hata kama chembe cha hardali basi huandikwa na Malaika hao, hata kama binaadam atatamka neno liwe dogo mno vipi basi litaandikwa. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ وَنَعْلَمُ مَا تُوَسْوِسُ بِهِ نَفْسُهُ ۖ وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنْ حَبْلِ الْوَرِيدِ﴿١٦﴾

Na kwa yakini Tumemuumba insani na Tunajua yale yanayowaza nafsi yake, na Sisi Tuko karibu naye kuliko mshipa wa koo.

 

إِذْ يَتَلَقَّى الْمُتَلَقِّيَانِ عَنِ الْيَمِينِ وَعَنِ الشِّمَالِ قَعِيدٌ﴿١٧﴾

Pale wanapopokea wapokeaji wawili (Malaika) wanaokaa kuliani na kushotoni. 

 

مَّا يَلْفِظُ مِن قَوْلٍ إِلَّا لَدَيْهِ رَقِيبٌ عَتِيدٌ﴿١٨﴾

Hatamki kauli yeyote isipokuwa anaye mchungaji aliyejitayarisha (kurekodi). [Qaaf: 16-18]

 

  Hakuna kitakachokosekana kuandikwa na Malaika hao, wala binaadamu hawezi kuwakwepa kwani wao wamewekwa kwa ajili hiyo: Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَإِنَّ عَلَيْكُمْ لَحَافِظِينَ ﴿١٠﴾

Na hakika juu yenu bila shaka kuna wenye kuhifadhi (na kuchunga).  

 

 

كِرَامًا كَاتِبِينَ ﴿١١﴾

Watukufu wanaoandika (amali).

 

 

يَعْلَمُونَ مَا تَفْعَلُونَ ﴿١٢﴾

Wanajua yale myafanyayo. [Al-Infitwaar: 10-12]

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ametuumba katika umbo bora kabisa na Amepanga kila kiungo mahali pake panapostahiki. Kwa hikma Yake, Ameviumba viungo viwili muhimu katika mwili wa binaadamu katika sehemu zilizofichika ili vihifadhike visidhihirike nje ya mwili wake. Navyo ni: ulimi na sehemu za siri. Ni viungo ambavyo pindi binaadamu atakapovichunga basi vitampeleka Jannah kama Anavyosema Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

 عَنْ سَهْلِ بْنِ سَعْدٍ رضي الله عنه ، عَنْ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: (( مَنْ يَضْمَنْ لِي مَا بَيْنَ لَحْيَيْهِ وَمَا بَيْنَ رِجْلَيْهِ ، أَضْمَنْ لَهُ الْجَنَّةَ))    متفق عليه

Sahl bin Sa'd (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayenidhaminia kilichomo baina ya taya zake [yaani ulimi] na kilichomo baina ya miguu yake [yaani tupu au sehemu za siri] nami nitamdhamini Jannah)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Katika Hadiyth nyingine:

 

عن عقبة بن عامر رضي الله عنه قال : قلت : يا رسول الله ما النجاة ؟ قال: ((مْسِكْ عَلَيْكَ لِسَانَكَ ، وَلْيَسَعْكَ بَيْتُكَ ، وَابْكِ عَلَى خَطِيئَتِكَ)) رواه الترمذي   صححه الألباني في صحيح الترغيب 3331    

'Uqbah bin 'Aamir (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: "Nilimuuliza Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) "Ee Rasuli wa Allaah, ni kupi kuokoka? Akajibu: ((Uzuie ulimi wako, utosheke na nyumba yako na ulie juu ya dhambi zako)) [At-Tirmidhiy na ameipa daraja ya Swahiyh Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Targhiyb (3331)]

 

 وعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِي اللَّه عَنْه قَالَ : قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ :  (( مَنْ كَانَ يُؤْمِنُ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ، فَلْيَقُلْ خَيْرًا أَوْ لِيَصْمُتْ))    متفق عليه  .

Na kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allahu 'anhu) ambaye amsema: Rasuli wa Allaah  (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mwenye kumuamini Allaah na siku ya Mwisho basi aseme mema au anyamaze)) [Al-Bukhaariy na Muslim]  

 

 

 

 

Share