Mume Anachelewa Kurudi Na Ananipiga

SWALI:

Asalamu Alaykum Warakhmatu llah Wabarakatu,

Ningependa kukushukuruni kwa jitihada zenu za kuanzisha website hii ya kiislam yenye manufaa mengi kwa waislamu wote duniani.

1.Swali langu ningependa kuuliza: - Mume wangu ni mtu wa hasira sana na anapenda kunipiga kila siku jee ipo njia gani nifanye ili awache tabia hii mbaya

2. Mume wangu muda mwingi anakuwapo nje na marafiki hana time ya kukaa pamoja na mke wake anapenda sana marafiki, na anapenda sana kuchelewa kurudi nyumbani naomba ufafanuzi zaidi kuhusu njia gani nifanye juu ya swali hili.

Shukran

 

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum)  na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Njia ya kufanya kwanza ni kumlingania kwa kumfahamisha kuwa yeye kama Muislamu na kiongozi wa familia kuwa ni mchunga, na kila mchunga ataulizwa juu ya kile anachokichunga, kama ilivyokuja dalili katika Hadiyth ifuatayo:

((كلكم راع وكلكم مسئول عن رعيته الإمام راع ومسئول عن رعيته والرجل راع في أهله وهو مسئول عن رعيته والمرأة راعية في بيت زوجها ومسئولة عن رعيتها))  

((Kila mmoja kati yenu ni mchungaji, na kila mmoja kati yenu atapaswa kuulizwa ya juu ya kile anachokichunga. Imaam ni mchungaji na ataulizwa kwa anaowachunga. Mume ni mchungaji wa familia yake, naye atapaswa kuulizwa juu ya anaowachunga. Na mke ni mchungaji wa nyumba ya mumewe, naye pia atapaswa kuulizwa juu ya anachokichunga. (Al-Bukhaariy, Muslim)

Kwa maana hiyo anawajibika ajue haki za mke na azitekeleze, na azijue haki zake kama mume kwa mkewe kisha awe na uadilifu kwa pande zote. Na hakutakuwa na mafanikio pasina kutanguliza haki ya msingi ambayo ni haki za Muumba, kwani katika kujua na kuzitekeleza haki za Allaah mkiunganisha na haki za mke na mume kama tulivyoeleza hapo nyuma, hasira zitapungua kama si kwisha kabisa. Kupigana hakutokuwepo wala hakutakuwa na muda wa kupoteza kukaa na marafiki na InshaAllaah atawahi kurudi nyumbani na kujua yanayoisibu familia yake, zaidi ya hayo ni kukithirisha ibada na maombi kwa Allaah Ta’ala Awafanyie wepesi

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share