026 - Ash-Shu'araa

 

الشُّعَرآء

 

026-Ash-Shu’araa 

 

 026-Ash-Shu’araa: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

طسم ﴿١﴾

1. Twaa Siyn Miym.[1]  

 

 

 

تِلْكَ آيَاتُ الْكِتَابِ الْمُبِينِ ﴿٢﴾

2. Hizi ni Aayaat za Kitabu kilicho bayana.

 

 

 

لَعَلَّكَ بَاخِعٌ نَّفْسَكَ أَلَّا يَكُونُوا مُؤْمِنِينَ ﴿٣﴾

3. Huenda utaiangamiza nafsi yako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) (kwa sikitiko) kwamba hawawi wenye kuamini.

 

 

 

إِن نَّشَأْ نُنَزِّلْ عَلَيْهِم مِّنَ السَّمَاءِ آيَةً فَظَلَّتْ أَعْنَاقُهُمْ لَهَا خَاضِعِينَ ﴿٤﴾

4. Tungetaka Tungewateremshia kutoka mbinguni Aayah (Muujiza), kisha zingebakia shingo zao zenye kuunyenyekea.

 

 

 

وَمَا يَأْتِيهِم مِّن ذِكْرٍ مِّنَ الرَّحْمَـٰنِ مُحْدَثٍ إِلَّا كَانُوا عَنْهُ مُعْرِضِينَ ﴿٥﴾

5. Na hauwafikii ukumbusho wowote ule mpya kutoka kwa Ar-Rahmaan isipokuwa walikuwa ni wenye kuupuuza.

 

 

 

فَقَدْ كَذَّبُوا فَسَيَأْتِيهِمْ أَنبَاءُ مَا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ ﴿٦﴾

6. Kwa yakini wamekadhibisha, basi itawafikia khabari ya yale waliyokuwa wakiyafanyia istihzai.

 

 

 

أَوَلَمْ يَرَوْا إِلَى الْأَرْضِ كَمْ أَنبَتْنَا فِيهَا مِن كُلِّ زَوْجٍ كَرِيمٍ ﴿٧﴾

7. Je, hawaioni ardhi? Mimea mingapi Tumeiotesha humo ya kila aina nzuri?

 

 

 

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً ۖ وَمَا كَانَ أَكْثَرُهُم مُّؤْمِنِينَ ﴿٨﴾

8. Hakika katika hayo pana Aayah (Ishara),[2] lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.

 

 

 

وَإِنَّ رَبَّكَ لَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ ﴿٩﴾

9. Na hakika Rabb wako bila shaka Ndiye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Kurehemu.

 

 

 

وَإِذْ نَادَىٰ رَبُّكَ مُوسَىٰ أَنِ ائْتِ الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ ﴿١٠﴾

10. Na Rabb wako Alipomwita Muwsaa kwamba: Nenda kwa watu madhalimu.[3]

 

 

 

قَوْمَ فِرْعَوْنَ ۚ أَلَا يَتَّقُونَ ﴿١١﴾

11. Watu wa Firawni. Je, hawamchi Allaah?

 

 

 

قَالَ رَبِّ إِنِّي أَخَافُ أَن يُكَذِّبُونِ ﴿١٢﴾

12. (Muwsaa) akasema: Rabb wangu! Hakika mimi nakhofu wasije kunikadhibisha.

 

 

 

وَيَضِيقُ صَدْرِي وَلَا يَنطَلِقُ لِسَانِي فَأَرْسِلْ إِلَىٰ هَارُونَ ﴿١٣﴾

13. Na kifua changu kinadhikika, na ulimi wangu haukunjuki vizuri, basi Tuma (Jibriyl na Wahyi) kwa Haaruwn (aje kunisaidia).

 

 

 

وَلَهُمْ عَلَيَّ ذَنبٌ فَأَخَافُ أَن يَقْتُلُونِ ﴿١٤﴾

14. Nao wana shtaka la kosa dhidi yangu, basi nakhofu wasiniue.

 

 

 

قَالَ كَلَّا ۖ فَاذْهَبَا بِآيَاتِنَا ۖ إِنَّا مَعَكُم مُّسْتَمِعُونَ ﴿١٥﴾

15. (Allaah) Akasema: Hapana! Nendeni na Aayaat (Miujiza) Yetu, hakika Sisi Tuko pamoja nanyi Wenye Kusikiliza.

 

 

 

فَأْتِيَا فِرْعَوْنَ فَقُولَا إِنَّا رَسُولُ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٦﴾

16. Basi mfikieni Firawni, na mseme: Hakika sisi ni Rasuli wa Rabb wa walimwengu.

 

 

 

أَنْ أَرْسِلْ مَعَنَا بَنِي إِسْرَائِيلَ ﴿١٧﴾

17.  Ya kwamba waachilie wana wa Israaiyl wende pamoja nasi.

 

 

 

قَالَ أَلَمْ نُرَبِّكَ فِينَا وَلِيدًا وَلَبِثْتَ فِينَا مِنْ عُمُرِكَ سِنِينَ ﴿١٨﴾

18. (Fira’wn) akasema: Je, hatukukulea kwetu ulipokuwa mtoto, na ukaishi kwetu miaka mingi ya umri wako?

 

 

 

 

وَفَعَلْتَ فَعْلَتَكَ الَّتِي فَعَلْتَ وَأَنتَ مِنَ الْكَافِرِينَ ﴿١٩﴾

19. Na ukafanya kitendo chako ambacho ulikifanya nawe ni miongoni mwa wasio na shukurani.

 

 

 

قَالَ فَعَلْتُهَا إِذًا وَأَنَا مِنَ الضَّالِّينَ ﴿٢٠﴾

20. (Muwsaa) akasema: Nilikifanya hapo wakati nilikuwa miongoni mwa waliokosea.

 

 

 

فَفَرَرْتُ مِنكُمْ لَمَّا خِفْتُكُمْ فَوَهَبَ لِي رَبِّي حُكْمًا وَجَعَلَنِي مِنَ الْمُرْسَلِينَ ﴿٢١﴾

21. Nikakukimbieni nilipokukhofuni, na Rabb wangu Akanitunukia hikmah na Akanijaalia miongoni mwa Rusuli.

 

 

 

وَتِلْكَ نِعْمَةٌ تَمُنُّهَا عَلَيَّ أَنْ عَبَّدتَّ بَنِي إِسْرَائِيلَ ﴿٢٢﴾

22. Na hiyo ni neema unayonisimbulia, na wewe umewatia utumwani wana wa Israaiyl.

 

 

 

قَالَ فِرْعَوْنُ وَمَا رَبُّ الْعَالَمِينَ ﴿٢٣﴾

23. Firawni akasema: Na ni nani kwani Rabb wa walimwengu?

 

 

 

قَالَ رَبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا ۖ إِن كُنتُم مُّوقِنِينَ ﴿٢٤﴾

24. (Muwsaa) akasema: Rabb wa mbingu na ardhi na vilivyo baina yake mkiwa ni wenye yakini.

 

 

 

قَالَ لِمَنْ حَوْلَهُ أَلَا تَسْتَمِعُونَ ﴿٢٥﴾

25. (Firawni) akawaambia waliomzunguka: Hivi mnasikia?

 

 

 

قَالَ رَبُّكُمْ وَرَبُّ آبَائِكُمُ الْأَوَّلِينَ ﴿٢٦﴾

26. (Muwsaa) akasema: Rabb wenu na Rabb wa baba zenu wa awali.

 

 

 

قَالَ إِنَّ رَسُولَكُمُ الَّذِي أُرْسِلَ إِلَيْكُمْ لَمَجْنُونٌ ﴿٢٧﴾

27. (Firawni) akasema: Hakika Rasuli wenu ambaye ametumwa kwenu bila shaka ni majnuni.

 

 

 

قَالَ رَبُّ الْمَشْرِقِ وَالْمَغْرِبِ وَمَا بَيْنَهُمَا ۖ إِن كُنتُمْ تَعْقِلُونَ ﴿٢٨﴾

28. (Muwsaa) akasema: Rabb wa Mashariki na Magharibi na vilivyo baina yake, mkiwa nyinyi ni wenye kutia akilini.

 

 

 

قَالَ لَئِنِ اتَّخَذْتَ إِلَـٰهًا غَيْرِي لَأَجْعَلَنَّكَ مِنَ الْمَسْجُونِينَ ﴿٢٩﴾

29. (Firawni) akasema: Ukichagua mwabudiwa mwengine badala yangu, nitakufanya bila shaka miongoni mwa wafungwao gerezani.

 

 

 

قَالَ أَوَلَوْ جِئْتُكَ بِشَيْءٍ مُّبِينٍ ﴿٣٠﴾

30. (Muwsaa) akasema: Je, hata kama nikikujia na kitu bayana?

 

 

 

قَالَ فَأْتِ بِهِ إِن كُنتَ مِنَ الصَّادِقِينَ ﴿٣١﴾

31. (Firawni) akasema: Kilete ukiwa wewe ni miongoni mwa wakweli.

 

 

 

فَأَلْقَىٰ عَصَاهُ فَإِذَا هِيَ ثُعْبَانٌ مُّبِينٌ ﴿٣٢﴾

32. (Muwsaa) akatupa fimbo yake, tahamaki hiyo ikawa joka kubwa bayana.

 

 

 

وَنَزَعَ يَدَهُ فَإِذَا هِيَ بَيْضَاءُ لِلنَّاظِرِينَ ﴿٣٣﴾

33. Na akavuta mkono wake, tahamaki huo ukawa mweupe kwa watazamao.

 

 

 

قَالَ لِلْمَلَإِ حَوْلَهُ إِنَّ هَـٰذَا لَسَاحِرٌ عَلِيمٌ ﴿٣٤﴾

34. (Firawni) akawaambia wakuu waliomzunguka: Hakika huyu bila shaka ni mchawi mjuzi.[4]

 

 

 

يُرِيدُ أَن يُخْرِجَكُم مِّنْ أَرْضِكُم بِسِحْرِهِ فَمَاذَا تَأْمُرُونَ ﴿٣٥﴾

35. Anataka kukutoeni kutoka ardhi yenu kwa sihiri yake, basi mnashauri nini?

 

 

 

قَالُوا أَرْجِهْ وَأَخَاهُ وَابْعَثْ فِي الْمَدَائِنِ حَاشِرِينَ ﴿٣٦﴾

36. Wakasema: Muakhirishe kidogo na kaka yake, na tuma katika miji wakusanyao wachawi.

 

 

 

يَأْتُوكَ بِكُلِّ سَحَّارٍ عَلِيمٍ ﴿٣٧﴾

37. Watakujia na kila mchawi mjuzi.

 

 

 

فَجُمِعَ السَّحَرَةُ لِمِيقَاتِ يَوْمٍ مَّعْلُومٍ ﴿٣٨﴾

38. Basi wakakusanywa wachawi katika mahali na wakati wa siku maalumu.

 

 

 

وَقِيلَ لِلنَّاسِ هَلْ أَنتُم مُّجْتَمِعُونَ ﴿٣٩﴾

39. Na wakaambiwa watu: Je, mmekwishakusanyika?

 

 

 

لَعَلَّنَا نَتَّبِعُ السَّحَرَةَ إِن كَانُوا هُمُ الْغَالِبِينَ ﴿٤٠﴾

40. Ili tuwafuate wachawi, wakiwa wao ndio watakaoshinda.

 

 

 

فَلَمَّا جَاءَ السَّحَرَةُ قَالُوا لِفِرْعَوْنَ أَئِنَّ لَنَا لَأَجْرًا إِن كُنَّا نَحْنُ الْغَالِبِينَ ﴿٤١﴾

41. Basi walipokuja wachawi walimwambia Firawni: Je, tutapata ujira wowote   ikiwa sisi tutakuwa wenye kushinda?

 

 

 

قَالَ نَعَمْ وَإِنَّكُمْ إِذًا لَّمِنَ الْمُقَرَّبِينَ ﴿٤٢﴾

42. (Firawni) akasema: Naam! Na bila shaka nyinyi hapo mtakuwa miongoni mwa waliokurubishwa (kwangu).

 

 

 

قَالَ لَهُم مُّوسَىٰ أَلْقُوا مَا أَنتُم مُّلْقُونَ ﴿٤٣﴾

43. Muwsaa akawaambia: Tupeni vile mnavyotupa.

 

 

 

فَأَلْقَوْا حِبَالَهُمْ وَعِصِيَّهُمْ وَقَالُوا بِعِزَّةِ فِرْعَوْنَ إِنَّا لَنَحْنُ الْغَالِبُونَ ﴿٤٤﴾

44. Wakatupa kamba zao na fimbo zao, na wakasema: Kwa utukufu wa Firawni! Hakika sisi ni wenye kushinda.

 

 

 

فَأَلْقَىٰ مُوسَىٰ عَصَاهُ فَإِذَا هِيَ تَلْقَفُ مَا يَأْفِكُونَ ﴿٤٥﴾

45. Muwsaa akatupa fimbo yake, tahamaki inameza vyote walivyovizua.

 

 

 

فَأُلْقِيَ السَّحَرَةُ سَاجِدِينَ ﴿٤٦﴾

46. Basi wachawi wakajikuta wameanguka huku wakisujudu.

 

 

 

قَالُوا آمَنَّا بِرَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٤٧﴾

47. Wakasema: Tumemwamini Rabb wa walimwengu.

 

 

 

رَبِّ مُوسَىٰ وَهَارُونَ ﴿٤٨﴾

48. Rabb wa Muwsaa na Haaruwn.

 

 

 

قَالَ آمَنتُمْ لَهُ قَبْلَ أَنْ آذَنَ لَكُمْ ۖ إِنَّهُ لَكَبِيرُكُمُ الَّذِي عَلَّمَكُمُ السِّحْرَ فَلَسَوْفَ تَعْلَمُونَ ۚ لَأُقَطِّعَنَّ أَيْدِيَكُمْ وَأَرْجُلَكُم مِّنْ خِلَافٍ وَلَأُصَلِّبَنَّكُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٤٩﴾

49. (Firawni) akasema: Je, mmemwamini kabla sijakupeni idhini? Hakika bila shaka yeye ndiye mkubwa wenu aliyekufunzeni sihiri. Basi mtakuja kujua. Nitakukatenikateni mikono yenu na miguu yenu kinyume (kulia kwa kushoto), kisha nitakusulubuni nyote.

                             

 

 

قَالُوا لَا ضَيْرَ ۖ إِنَّا إِلَىٰ رَبِّنَا مُنقَلِبُونَ ﴿٥٠﴾

50. Wakasema: Hakuna dhara yoyote! Hakika sisi tunarudi kwa Rabb wetu.

 

 

 

إِنَّا نَطْمَعُ أَن يَغْفِرَ لَنَا رَبُّنَا خَطَايَانَا أَن كُنَّا أَوَّلَ الْمُؤْمِنِينَ ﴿٥١﴾

51. Hakika sisi tunatumai kwamba Rabb wetu Atatughufuria madhambi yetu kwa vile tumekuwa wa kwanza wenye kuamini.

 

 

 

وَأَوْحَيْنَا إِلَىٰ مُوسَىٰ أَنْ أَسْرِ بِعِبَادِي إِنَّكُم مُّتَّبَعُونَ ﴿٥٢﴾

52. Na Tukamfunulia Wahy Muwsaa kwamba: Safiri usiku pamoja na Waja Wangu, hakika nyinyi ni wenye kufuatwa.

 

 

 

فَأَرْسَلَ فِرْعَوْنُ فِي الْمَدَائِنِ حَاشِرِينَ ﴿٥٣﴾

53. Basi Firawni akawatuma wakusanyao wachawi katika miji. 

 

 

 

إِنَّ هَـٰؤُلَاءِ لَشِرْذِمَةٌ قَلِيلُونَ ﴿٥٤﴾

54. (Akisema): Hakika hawa ni kikundi kidhaifu kidogo, wachache.

 

 

 

وَإِنَّهُمْ لَنَا لَغَائِظُونَ ﴿٥٥﴾

55. Na hakika wao wanatughadhibisha.

 

 

 

وَإِنَّا لَجَمِيعٌ حَاذِرُونَ ﴿٥٦﴾

56. Na hakika sisi, bila shaka ni wengi wenye kuchukua hadhari mno.

 

 

 

فَأَخْرَجْنَاهُم مِّن جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ ﴿٥٧﴾

57. Basi Tukawatoa katika mabustani na chemchemu.

 

 

 

وَكُنُوزٍ وَمَقَامٍ كَرِيمٍ ﴿٥٨﴾

58. Na hazina za aina kwa aina na vyeo vya heshima.

 

 

 

كَذَٰلِكَ وَأَوْرَثْنَاهَا بَنِي إِسْرَائِيلَ ﴿٥٩﴾

59. Hivyo ndivyo (Tulivyofanya), na Tukayarithisha hayo wana wa Israaiyl.

 

 

 

فَأَتْبَعُوهُم مُّشْرِقِينَ ﴿٦٠﴾

60. Basi wakawafuata walipopambazukiwa.

 

 

 

فَلَمَّا تَرَاءَى الْجَمْعَانِ قَالَ أَصْحَابُ مُوسَىٰ إِنَّا لَمُدْرَكُونَ ﴿٦١﴾

61. Yalipoonana makundi mawili, wakasema watu wa Muwsaa: Hakika sisi bila shaka tutadirikiwa kukamatwa.

 

 

 

قَالَ كَلَّا ۖ إِنَّ مَعِيَ رَبِّي سَيَهْدِينِ ﴿٦٢﴾

62. (Muwsaa) akasema: Hapana! Hakika Rabb wangu Yu pamoja nami Ataniongoza.

 

 

فَأَوْحَيْنَا إِلَىٰ مُوسَىٰ أَنِ اضْرِب بِّعَصَاكَ الْبَحْرَ ۖ فَانفَلَقَ فَكَانَ كُلُّ فِرْقٍ كَالطَّوْدِ الْعَظِيمِ ﴿٦٣﴾

63. Tukamfunulia Wahy Muwsaa kwamba: Piga kwa fimbo yako bahari. Basi ikatengana ikawa kila sehemu kama jabali kubwa mno.

 

 

 

وَأَزْلَفْنَا ثَمَّ الْآخَرِينَ ﴿٦٤﴾

64. Na Tukawaleta karibu hapo wengine.

 

 

 

وَأَنجَيْنَا مُوسَىٰ وَمَن مَّعَهُ أَجْمَعِينَ ﴿٦٥﴾

65. Tukamuokoa Muwsaa na walio pamoja naye wote.

 

 

 

ثُمَّ أَغْرَقْنَا الْآخَرِينَ ﴿٦٦﴾

66. Kisha Tukawagharikisha wengine.

 

 

 

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً ۖ وَمَا كَانَ أَكْثَرُهُم مُّؤْمِنِينَ ﴿٦٧﴾

67. Hakika katika hayo pana Aayah (Ishara), lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.

 

 

 

وَإِنَّ رَبَّكَ لَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ ﴿٦٨﴾

 68. Na hakika Rabb wako bila shaka Ndiye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Kurehemu.

 

 

 

وَاتْلُ عَلَيْهِمْ نَبَأَ إِبْرَاهِيمَ ﴿٦٩﴾

69. Na wasomee (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) khabari za Ibraahiym.

 

 

 

إِذْ قَالَ لِأَبِيهِ وَقَوْمِهِ مَا تَعْبُدُونَ ﴿٧٠﴾

70. Alipomwambia baba yake na watu wake: Mnaabudu nini?

 

 

 

قَالُوا نَعْبُدُ أَصْنَامًا فَنَظَلُّ لَهَا عَاكِفِينَ ﴿٧١﴾

71. Wakasema: Tunaabudu masanamu, na tutaendelea kuyakalia kwa kuyaabudu.

 

 

 

قَالَ هَلْ يَسْمَعُونَكُمْ إِذْ تَدْعُونَ ﴿٧٢﴾

72. Akasema: Je, yanakusikieni mnapoyaomba?

 

 

 

أَوْ يَنفَعُونَكُمْ أَوْ يَضُرُّونَ ﴿٧٣﴾

73. Au yanakunufaisheni au yanakudhuruni?

 

 

 

قَالُوا بَلْ وَجَدْنَا آبَاءَنَا كَذَٰلِكَ يَفْعَلُونَ ﴿٧٤﴾

74. Wakasema: Bali tumewakuta baba zetu wakifanya hivyo.

 

 

 

قَالَ أَفَرَأَيْتُم مَّا كُنتُمْ تَعْبُدُونَ ﴿٧٥﴾

75.  Akasema: Je, mnaona hivyo mlivyokuwa mkiviabudu?

 

 

 

أَنتُمْ وَآبَاؤُكُمُ الْأَقْدَمُونَ ﴿٧٦﴾

76. Nyinyi na baba zenu waliotangulia?

 

 

 

فَإِنَّهُمْ عَدُوٌّ لِّي إِلَّا رَبَّ الْعَالَمِينَ ﴿٧٧﴾

77. Basi hakika hao ni adui zangu isipokuwa Rabb wa walimwengu.

 

 

 

الَّذِي خَلَقَنِي فَهُوَ يَهْدِينِ ﴿٧٨﴾

78. Ambaye Ameniumba, Naye Ananiongoza.

 

 

 

وَالَّذِي هُوَ يُطْعِمُنِي وَيَسْقِينِ ﴿٧٩﴾

79. Na Ambaye Ndiye Anayenilisha na Ananinywesha.

 

 

 

وَإِذَا مَرِضْتُ فَهُوَ يَشْفِينِ ﴿٨٠﴾

80. Na ninapokuwa mgonjwa, basi Yeye Ananiponyesha.

 

 

وَالَّذِي يُمِيتُنِي ثُمَّ يُحْيِينِ ﴿٨١﴾

81. Na Ambaye Atanifisha kisha Atanihuisha.

 

 

 

وَالَّذِي أَطْمَعُ أَن يَغْفِرَ لِي خَطِيئَتِي يَوْمَ الدِّينِ ﴿٨٢﴾

82. Na Ambaye natumai Atanighufuria makosa yangu Siku ya Malipo.

 

 

 

رَبِّ هَبْ لِي حُكْمًا وَأَلْحِقْنِي بِالصَّالِحِينَ ﴿٨٣﴾

83. Rabb wangu! Nitunukie hukmah,[5] na Unikutanishe na Swalihina.    

 

 

 

وَاجْعَل لِّي لِسَانَ صِدْقٍ فِي الْآخِرِينَ ﴿٨٤﴾

84. Na Nijaalie kusifika kwa heshima kwa vizazi watakaokuja baadaye.

 

 

 

وَاجْعَلْنِي مِن وَرَثَةِ جَنَّةِ النَّعِيمِ ﴿٨٥﴾

85. Na Nijaalie miongoni mwa warithi wa Jannah ya Neema.

 

 

 

وَاغْفِرْ لِأَبِي إِنَّهُ كَانَ مِنَ الضَّالِّينَ ﴿٨٦﴾

86. Na Mghufurie baba yangu, hakika yeye amekuwa miongoni mwa waliopotea.

 

 

 

وَلَا تُخْزِنِي يَوْمَ يُبْعَثُونَ ﴿٨٧﴾

87. Na wala Usinihizi Siku watakayofufuliwa.

 

 

 

يَوْمَ لَا يَنفَعُ مَالٌ وَلَا بَنُونَ ﴿٨٨﴾

88. Siku hayatofaa mali wala watoto.

 

 

 

إِلَّا مَنْ أَتَى اللَّـهَ بِقَلْبٍ سَلِيمٍ ﴿٨٩﴾

89. Isipokuwa yule atakayemfikia Allaah na moyo uliosalimika.[6]

 

 

 

وَأُزْلِفَتِ الْجَنَّةُ لِلْمُتَّقِينَ ﴿٩٠﴾

90. Na itakurubishwa Jannah kwa wenye taqwa.

 

 

 

وَبُرِّزَتِ الْجَحِيمُ لِلْغَاوِينَ ﴿٩١﴾

91. Na utadhihirishwa moto uwakao vikali mno kwa wapotofu.

 

 

 

وَقِيلَ لَهُمْ أَيْنَ مَا كُنتُمْ تَعْبُدُونَ ﴿٩٢﴾

92. Na wataambiwa: Wako wapi wale mliokuwa mkiwaabudu?

 

 

 

مِن دُونِ اللَّـهِ هَلْ يَنصُرُونَكُمْ أَوْ يَنتَصِرُونَ ﴿٩٣﴾

93. Badala ya Allaah. Je, wataweza kukunusuruni au kujinusuru wenyewe?

 

 

 

فَكُبْكِبُوا فِيهَا هُمْ وَالْغَاوُونَ ﴿٩٤﴾

94. Watapinduliwa gubigubi humo wao na wapotofu.

 

 

وَجُنُودُ إِبْلِيسَ أَجْمَعُونَ ﴿٩٥﴾

95. Na majeshi ya Ibliys yote.

 

 

 

قَالُوا وَهُمْ فِيهَا يَخْتَصِمُونَ ﴿٩٦﴾

96. Watasema na huku wao wanagombana humo. 

 

 

 

تَاللَّـهِ إِن كُنَّا لَفِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿٩٧﴾

97. Wa-Allaahi! Hakika tulikuwa bila shaka katika upotofu bayana.

 

 

 

إِذْ نُسَوِّيكُم بِرَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٩٨﴾

98. Tulipokusawazisheni na Rabb wa walimwengu.

 

 

 

وَمَا أَضَلَّنَا إِلَّا الْمُجْرِمُونَ ﴿٩٩﴾

99. Na hakuna aliyetupoteza isipokuwa wahalifu.

 

 

 

فَمَا لَنَا مِن شَافِعِينَ ﴿١٠٠﴾

100. Basi hatuna waombezi wowote.

 

 

 

وَلَا صَدِيقٍ حَمِيمٍ ﴿١٠١﴾

101. Wala rafiki khalisi.

 

 

 

فَلَوْ أَنَّ لَنَا كَرَّةً فَنَكُونَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ ﴿١٠٢﴾

102. Basi lau tungelikuwa tuna fursa ya kurudi (duniani) tungekuwa miongoni mwa Waumini.

 

 

 

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً ۖ وَمَا كَانَ أَكْثَرُهُم مُّؤْمِنِينَ ﴿١٠٣﴾

103. Hakika katika hayo pana Aayah (Ishara), lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.

 

 

 

وَإِنَّ رَبَّكَ لَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ ﴿١٠٤﴾

104. Na hakika Rabb wako bila shaka Ndiye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Kurehemu.

 

 

 

كَذَّبَتْ قَوْمُ نُوحٍ الْمُرْسَلِينَ ﴿١٠٥﴾

105. Watu wa Nuwh waliwakadhibisha Rusuli.

 

 

 

إِذْ قَالَ لَهُمْ أَخُوهُمْ نُوحٌ أَلَا تَتَّقُونَ ﴿١٠٦﴾

106. Alipowaambia ndugu yao Nuwh: Je, hamtokuwa na taqwa?

 

 

 

إِنِّي لَكُمْ رَسُولٌ أَمِينٌ ﴿١٠٧﴾

107. Hakika mimi kwenu ni Rasuli mwaminifu.

 

 

 

فَاتَّقُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُونِ ﴿١٠٨﴾

108. Basi mcheni Allaah na nitiini.

 

 

 

وَمَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ ۖ إِنْ أَجْرِيَ إِلَّا عَلَىٰ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٠٩﴾

109. Na wala sikuombeni ujira wowote juu yake.  Ujira wangu hauko isipokuwa kwa Rabb wa walimwengu.

 

 

 

فَاتَّقُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُونِ ﴿١١٠﴾

110. Basi mcheni Allaah na nitiini.

 

 

 

قَالُوا أَنُؤْمِنُ لَكَ وَاتَّبَعَكَ الْأَرْذَلُونَ ﴿١١١﴾

111. Wakasema: Je, tukuamini na hali kuwa waliokufuata ni watu duni?

 

 

 

قَالَ وَمَا عِلْمِي بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١١٢﴾

112.  Akasema: Na najuaje waliyokuwa wanayatenda?

 

 

 

إِنْ حِسَابُهُمْ إِلَّا عَلَىٰ رَبِّي ۖ لَوْ تَشْعُرُونَ ﴿١١٣﴾

113. Hesabu yao haiko isipokuwa kwa Rabb wangu, lau mngetambua.

 

 

 

وَمَا أَنَا بِطَارِدِ الْمُؤْمِنِينَ ﴿١١٤﴾

114. Nami sitowafukuza walioamini.

 

 

 

إِنْ أَنَا إِلَّا نَذِيرٌ مُّبِينٌ ﴿١١٥﴾

115. Mimi sina kingine zaidi ya kuwa mwonyaji mbainishaji.

 

 

 

قَالُوا لَئِن لَّمْ تَنتَهِ يَا نُوحُ لَتَكُونَنَّ مِنَ الْمَرْجُومِينَ ﴿١١٦﴾

116. Wakasema: Usipoacha ewe Nuwh bila shaka utakuwa miongoni mwa wenye kurajimiwa.

 

 

 

قَالَ رَبِّ إِنَّ قَوْمِي كَذَّبُونِ ﴿١١٧﴾

117. Akasema: Rabb wangu! Hakika watu wangu wamenikadhibisha.

 

 

 

فَافْتَحْ بَيْنِي وَبَيْنَهُمْ فَتْحًا وَنَجِّنِي وَمَن مَّعِيَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ ﴿١١٨﴾

118. Basi Hukumu baina yangu na baina yao (kwa) Hukmu (Yako), na Uniokoe mimi na wale walio pamoja nami miongoni mwa Waumini.

 

 

 

فَأَنجَيْنَاهُ وَمَن مَّعَهُ فِي الْفُلْكِ الْمَشْحُونِ ﴿١١٩﴾

119. Tukamuokoa pamoja na wale waliokuwa naye katika jahazi iliyosheheni.

 

 

 

ثُمَّ أَغْرَقْنَا بَعْدُ الْبَاقِينَ ﴿١٢٠﴾

120. Kisha Tukawagharikisha baada ya hapo waliobakia.

 

 

 

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً ۖ وَمَا كَانَ أَكْثَرُهُم مُّؤْمِنِينَ ﴿١٢١﴾

121.  Hakika katika hayo pana Aayah (Ishara), lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.

 

 

 

وَإِنَّ رَبَّكَ لَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ ﴿١٢٢﴾

122. Na hakika Rabb wako bila shaka Ndiye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Kurehemu.

 

 

 

كَذَّبَتْ عَادٌ الْمُرْسَلِينَ ﴿١٢٣﴾

123. Kina ‘Aad waliwakadhibisha Rusuli.

 

 

 

إِذْ قَالَ لَهُمْ أَخُوهُمْ هُودٌ أَلَا تَتَّقُونَ ﴿١٢٤﴾

124. Alipowaambia ndugu yao Huwd: Je, hamtokuwa na taqwa?

 

 

 

إِنِّي لَكُمْ رَسُولٌ أَمِينٌ ﴿١٢٥﴾

125. Hakika mimi kwenu ni Rasuli mwaminifu.

 

 

 

فَاتَّقُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُونِ ﴿١٢٦﴾

126. Basi mcheni Allaah na nitiini.

 

 

 

وَمَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ ۖ إِنْ أَجْرِيَ إِلَّا عَلَىٰ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٢٧﴾

127. Na wala sikuombeni ujira wowote juu yake.  Ujira wangu hauko isipokuwa kwa Rabb wa walimwengu.

 

 

 

أَتَبْنُونَ بِكُلِّ رِيعٍ آيَةً تَعْبَثُونَ ﴿١٢٨﴾

128. Je, mnajenga katika kila sehemu maarufu za mnyanyuko majengo marefurefu kwa ajili ya burudani tu?

 

 

 

وَتَتَّخِذُونَ مَصَانِعَ لَعَلَّكُمْ تَخْلُدُونَ ﴿١٢٩﴾

129. Na mnafanya ngome madhubuti kama kwamba mtaishi milele?

 

 

 

وَإِذَا بَطَشْتُم بَطَشْتُمْ جَبَّارِينَ ﴿١٣٠﴾

130. Na mnapofanya uonevu, mnatumia nguvu kijabari.

 

 

 

فَاتَّقُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُونِ ﴿١٣١﴾

131. Basi mcheni Allaah na nitiini.

 

 

 

وَاتَّقُوا الَّذِي أَمَدَّكُم بِمَا تَعْلَمُونَ ﴿١٣٢﴾

132. Na mcheni Ambaye Amekupeni yale mnayoyajua.

 

 

 

أَمَدَّكُم بِأَنْعَامٍ وَبَنِينَ ﴿١٣٣﴾

133. Amekupeni wanyama wa mifugo na watoto.

 

 

 

وَجَنَّاتٍ وَعُيُونٍ ﴿١٣٤﴾

134.  Na mabustani na chemchemu.

 

 

 

إِنِّي أَخَافُ عَلَيْكُمْ عَذَابَ يَوْمٍ عَظِيمٍ ﴿١٣٥﴾

135. Hakika mimi nakukhofieni adhabu ya Siku iliyo kubwa kabisa.

 

 

 

قَالُوا سَوَاءٌ عَلَيْنَا أَوَعَظْتَ أَمْ لَمْ تَكُن مِّنَ الْوَاعِظِينَ ﴿١٣٦﴾

136. Wakasema: Ni sawa sawa kwetu, ukiwaidhi au usipokuwa miongoni mwa wanaowaidhi.

 

 

 

إِنْ هَـٰذَا إِلَّا خُلُقُ الْأَوَّلِينَ ﴿١٣٧﴾

137. Haya si chochote isipokuwa ni desturi ya watu wa awali.

 

 

 

وَمَا نَحْنُ بِمُعَذَّبِينَ ﴿١٣٨﴾

138. Na sisi hatutoadhibiwa.

 

 

 

فَكَذَّبُوهُ فَأَهْلَكْنَاهُمْ ۗ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً ۖ وَمَا كَانَ أَكْثَرُهُم مُّؤْمِنِينَ ﴿١٣٩﴾

139. Wakamkadhibisha, basi Tuliwaangamiza. Hakika katika hayo pana Aayah (Ishara), lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.

 

 

 

وَإِنَّ رَبَّكَ لَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ ﴿١٤٠﴾

140. Na hakika Rabb wako bila shaka Ndiye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Kurehemu.

 

 

 

كَذَّبَتْ ثَمُودُ الْمُرْسَلِينَ ﴿١٤١﴾

141. Kina Thamuwd waliwakadhibisha Rusuli.

 

 

 

إِذْ قَالَ لَهُمْ أَخُوهُمْ صَالِحٌ أَلَا تَتَّقُونَ ﴿١٤٢﴾

142. Alipowaambia ndugu yao Swaalih: Je, hamtokuwa na taqwa?

 

 

 

إِنِّي لَكُمْ رَسُولٌ أَمِينٌ ﴿١٤٣﴾

143. Hakika mimi kwenu ni Rasuli mwaminifu.

 

 

 

فَاتَّقُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُونِ ﴿١٤٤﴾

144. Basi mcheni Allaah na nitiini.

 

 

 

وَمَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ ۖ إِنْ أَجْرِيَ إِلَّا عَلَىٰ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٤٥﴾

145. Na wala sikuombeni ujira wowote juu yake.  Ujira wangu hauko isipokuwa kwa Rabb wa walimwengu.

 

 

 

أَتُتْرَكُونَ فِي مَا هَاهُنَا آمِنِينَ ﴿١٤٦﴾

146. Je, (mnadhani) mtaachwa mkiwa katika amani kwenye haya hapa mliyonayo? 

 

 

 

فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ ﴿١٤٧﴾

147. Katika mabustani na chemchemu.

 

 

 

وَزُرُوعٍ وَنَخْلٍ طَلْعُهَا هَضِيمٌ ﴿١٤٨﴾

148. Na mimea na mitende makole yake laini, yamewiva.

 

 

 

وَتَنْحِتُونَ مِنَ الْجِبَالِ بُيُوتًا فَارِهِينَ ﴿١٤٩﴾

149. Na mnachonga milimani nyumba kwa uhodari kabisa.

 

 

 

فَاتَّقُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُونِ ﴿١٥٠﴾

150. Basi mcheni Allaah na nitiini.

 

 

 

وَلَا تُطِيعُوا أَمْرَ الْمُسْرِفِينَ ﴿١٥١﴾

151. Na wala msitii amri ya wenye kupindukia mipaka.

 

 

 

الَّذِينَ يُفْسِدُونَ فِي الْأَرْضِ وَلَا يُصْلِحُونَ ﴿١٥٢﴾

152. Ambao wanafanya ufisadi katika ardhi na wala hawatengenezi.

 

 

 

قَالُوا إِنَّمَا أَنتَ مِنَ الْمُسَحَّرِينَ ﴿١٥٣﴾

153. Wakasema: Hakika wewe ni miongoni mwa waliorogwa.

 

 

 

مَا أَنتَ إِلَّا بَشَرٌ مِّثْلُنَا فَأْتِ بِآيَةٍ إِن كُنتَ مِنَ الصَّادِقِينَ ﴿١٥٤﴾

154. Wewe si chochote isipokuwa mtu kama sisi tu, basi lete Aayah (Ishara, Dalili) ukiwa wewe ni miongoni mwa wakweli.

 

 

 

قَالَ هَـٰذِهِ نَاقَةٌ لَّهَا شِرْبٌ وَلَكُمْ شِرْبُ يَوْمٍ مَّعْلُومٍ ﴿١٥٥﴾

155. Akasema: Huyu hapa ngamia jike, ana zamu ya kunywa, nanyi mna zamu ya kunywa siku maalumu.

 

 

 

وَلَا تَمَسُّوهَا بِسُوءٍ فَيَأْخُذَكُمْ عَذَابُ يَوْمٍ عَظِيمٍ ﴿١٥٦﴾

156. Na wala msimguse kwa uovu, ikaja kukuchukueni adhabu ya Siku iliyo kuu kabisa.

 

 

 

فَعَقَرُوهَا فَأَصْبَحُوا نَادِمِينَ ﴿١٥٧﴾

157. Basi wakamuua. Wakapambazukiwa wenye kujuta.

 

 

 

فَأَخَذَهُمُ الْعَذَابُ ۗ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً ۖ وَمَا كَانَ أَكْثَرُهُم مُّؤْمِنِينَ ﴿١٥٨﴾

158. Ikawachukuwa adhabu. Hakika katika hayo pana Aayah (Ishara), lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.

 

 

 

وَإِنَّ رَبَّكَ لَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ ﴿١٥٩﴾

159. Na hakika Rabb wako bila shaka Ndiye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Kurehemu.

 

 

 

كَذَّبَتْ قَوْمُ لُوطٍ الْمُرْسَلِينَ ﴿١٦٠﴾

160. Watu wa Luutw waliwakadhibisha Rusuli.

 

 

 

إِذْ قَالَ لَهُمْ أَخُوهُمْ لُوطٌ أَلَا تَتَّقُونَ ﴿١٦١﴾

161. Alipowaambia ndugu yao Luutw: Je, hamtokuwa na taqwa?

 

 

 

إِنِّي لَكُمْ رَسُولٌ أَمِينٌ ﴿١٦٢﴾

162. Hakika mimi kwenu ni Rasuli mwaminifu.

 

 

 

فَاتَّقُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُونِ ﴿١٦٣﴾

163. Basi mcheni Allaah na nitiini.

 

 

 

وَمَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ ۖ إِنْ أَجْرِيَ إِلَّا عَلَىٰ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٦٤﴾

164. Na wala sikuombeni ujira wowote juu yake.  Ujira wangu hauko isipokuwa kwa Rabb wa walimwengu.

 

 

 

أَتَأْتُونَ الذُّكْرَانَ مِنَ الْعَالَمِينَ ﴿١٦٥﴾

165. Je, mnawaendea wanaume miongoni mwa walimwengu?

 

 

 

وَتَذَرُونَ مَا خَلَقَ لَكُمْ رَبُّكُم مِّنْ أَزْوَاجِكُم ۚ بَلْ أَنتُمْ قَوْمٌ عَادُونَ ﴿١٦٦﴾

166. Na mnaacha kile Alichokuumbieni Rabb wenu katika wake zenu. Bali nyinyi ni watu mliopindukia mipaka.

 

 

 

قَالُوا لَئِن لَّمْ تَنتَهِ يَا لُوطُ لَتَكُونَنَّ مِنَ الْمُخْرَجِينَ ﴿١٦٧﴾

167. Wakasema: Usipoacha ee Luutw, bila shaka utakuwa miongoni mwa watakaofukuzwa.

 

 

 

قَالَ إِنِّي لِعَمَلِكُم مِّنَ الْقَالِينَ ﴿١٦٨﴾

168. Akasema: Hakika mimi ni katika wanaochukia mno kitendo chenu.

 

 

 

رَبِّ نَجِّنِي وَأَهْلِي مِمَّا يَعْمَلُونَ ﴿١٦٩﴾

169. Rabb wangu! Niokoe na ahli zangu kutokana na yale wanayotenda.

 

 

 

فَنَجَّيْنَاهُ وَأَهْلَهُ أَجْمَعِينَ ﴿١٧٠﴾

170. Basi Tukamuokoa na ahli zake wote.

 

 

 

إِلَّا عَجُوزًا فِي الْغَابِرِينَ ﴿١٧١﴾

171. Isipokuwa kikongwe katika waliobaki nyuma.

 

 

 

ثُمَّ دَمَّرْنَا الْآخَرِينَ ﴿١٧٢﴾

172. Kisha Tukadamiri wengineo.

 

 

 

وَأَمْطَرْنَا عَلَيْهِم مَّطَرًا ۖ فَسَاءَ مَطَرُ الْمُنذَرِينَ ﴿١٧٣﴾

173. Na Tukawanyeshea mvua (ya adhabu). Basi uovu ulioje mvua ya walioonywa!

 

 

 

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً ۖ وَمَا كَانَ أَكْثَرُهُم مُّؤْمِنِينَ ﴿١٧٤﴾

174. Hakika katika hayo pana Aayah (Ishara), lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.

 

 

 

وَإِنَّ رَبَّكَ لَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ ﴿١٧٥﴾

175. Na hakika Rabb wako bila shaka Ndiye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Kurehemu.

 

 

 

كَذَّبَ أَصْحَابُ الْأَيْكَةِ الْمُرْسَلِينَ ﴿١٧٦﴾

176. Watu wa Al-Aykah[7] waliwakadhibisha Rusuli.

 

 

 

إِذْ قَالَ لَهُمْ شُعَيْبٌ أَلَا تَتَّقُونَ ﴿١٧٧﴾

177. Alipowaambia Shu’ayb: Je, hamtokuwa na taqwa?

 

 

 

إِنِّي لَكُمْ رَسُولٌ أَمِينٌ ﴿١٧٨﴾

178. Hakika mimi kwenu ni Rasuli mwaminifu.

 

 

 

فَاتَّقُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُونِ ﴿١٧٩﴾

179. Basi mcheni Allaah na nitiini.

 

 

 

وَمَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ ۖ إِنْ أَجْرِيَ إِلَّا عَلَىٰ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٨٠﴾

180. Na wala sikuombeni ujira wowote juu yake.  Ujira wangu hauko isipokuwa kwa Rabb wa walimwengu.

 

 

 

أَوْفُوا الْكَيْلَ وَلَا تَكُونُوا مِنَ الْمُخْسِرِينَ ﴿١٨١﴾

181. Timizeni kipimo na wala msiwe miongoni mwa wenye kupunja.

 

 

 

وَزِنُوا بِالْقِسْطَاسِ الْمُسْتَقِيمِ ﴿١٨٢﴾

182. Na pimeni kwa mizani iliyosawa.

 

 

 

وَلَا تَبْخَسُوا النَّاسَ أَشْيَاءَهُمْ وَلَا تَعْثَوْا فِي الْأَرْضِ مُفْسِدِينَ ﴿١٨٣﴾

183. Na wala msiwapunje watu vitu vyao, na wala msieneze uovu katika ardhi hali ya kuwa ni wenye kufanya ufisadi.

 

 

 

وَاتَّقُوا الَّذِي خَلَقَكُمْ وَالْجِبِلَّةَ الْأَوَّلِينَ ﴿١٨٤﴾

184. Na mcheni Ambaye Amekuumbeni na viumbe vingi wa awali.

 

 

 

قَالُوا إِنَّمَا أَنتَ مِنَ الْمُسَحَّرِينَ ﴿١٨٥﴾

185. Wakasema: Hakika wewe ni miongoni mwa waliorogwa.

 

 

 

وَمَا أَنتَ إِلَّا بَشَرٌ مِّثْلُنَا وَإِن نَّظُنُّكَ لَمِنَ الْكَاذِبِينَ ﴿١٨٦﴾

186. Nawe si chochote isipokuwa ni mtu tu kama sisi, nasi tuna yakini wewe ni miongoni mwa waongo.

 

 

 

فَأَسْقِطْ عَلَيْنَا كِسَفًا مِّنَ السَّمَاءِ إِن كُنتَ مِنَ الصَّادِقِينَ ﴿١٨٧﴾

187. Basi tuangushie vipande vipande vya mbingu, ukiwa ni miongoni mwa wakweli.

 

 

 

قَالَ رَبِّي أَعْلَمُ بِمَا تَعْمَلُونَ ﴿١٨٨﴾

188. Akasema: Rabb wangu Anajua zaidi yale mnayoyatenda.

 

 

 

فَكَذَّبُوهُ فَأَخَذَهُمْ عَذَابُ يَوْمِ الظُّلَّةِ ۚ إِنَّهُ كَانَ عَذَابَ يَوْمٍ عَظِيمٍ ﴿١٨٩﴾

189. Wakamkadhibisha. Basi adhabu ya siku ya kivuli[8] (cha mawingu) ikawachukua. Hakika hiyo ilikuwa ni adhabu ya Siku kubwa mno.

 

 

 

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً ۖ وَمَا كَانَ أَكْثَرُهُم مُّؤْمِنِينَ ﴿١٩٠﴾

190. Hakika katika haya pana Aayah (Ishara), lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.

 

 

 

وَإِنَّ رَبَّكَ لَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ ﴿١٩١﴾

191. Na hakika Rabb wako bila shaka Ndiye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Kurehemu.

 

 

 

وَإِنَّهُ لَتَنزِيلُ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٩٢﴾

192. Na hakika hii (Qur-aan) ni Uteremsho wa Rabb wa walimwengu.

 

 

 

نَزَلَ بِهِ الرُّوحُ الْأَمِينُ ﴿١٩٣﴾

193. Ameiteremsha Ar-Ruwh[9] (Jibriyl) mwaminifu.

 

 

 

عَلَىٰ قَلْبِكَ لِتَكُونَ مِنَ الْمُنذِرِينَ ﴿١٩٤﴾

194. Juu ya moyo wako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) ili uwe miongoni mwa waonyaji.

 

 

 

بِلِسَانٍ عَرَبِيٍّ مُّبِينٍ ﴿١٩٥﴾

195. Kwa lugha ya Kiarabu bayana.

 

 

 

وَإِنَّهُ لَفِي زُبُرِ الْأَوَّلِينَ ﴿١٩٦﴾

196. Na hakika hii bila shaka imo katika Vitabu vya hukumu vya awali.

 

 

 

أَوَلَمْ يَكُن لَّهُمْ آيَةً أَن يَعْلَمَهُ عُلَمَاءُ بَنِي إِسْرَائِيلَ ﴿١٩٧﴾

197. Je, haikuwa kwao ni (Aayah (Dalili) kwamba wanavyuoni wa wana wa Israaiyl wanaitambua? 

 

 

 

وَلَوْ نَزَّلْنَاهُ عَلَىٰ بَعْضِ الْأَعْجَمِينَ ﴿١٩٨﴾

198. Na lau Tungeliiteremsha (hii Qur-aan) kwa yeyote miongoni mwa wasio Waarabu.

 

 

 

فَقَرَأَهُ عَلَيْهِم مَّا كَانُوا بِهِ مُؤْمِنِينَ ﴿١٩٩﴾

199. Na akawasomea, wasingelikuwa wenye kuiamini.

 

 

 

كَذَٰلِكَ سَلَكْنَاهُ فِي قُلُوبِ الْمُجْرِمِينَ ﴿٢٠٠﴾

200. Hivyo ndivyo Tumeuingiza (ukanushaji) katika nyoyo za wakhalifu.

 

 

 

لَا يُؤْمِنُونَ بِهِ حَتَّىٰ يَرَوُا الْعَذَابَ الْأَلِيمَ ﴿٢٠١﴾

201. Hawaiamini mpaka waione adhabu iumizayo.

 

 

 

فَيَأْتِيَهُم بَغْتَةً وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ ﴿٢٠٢﴾

202. Iwajie ghafla, nao hawatambui.

 

 

 

فَيَقُولُوا هَلْ نَحْنُ مُنظَرُونَ ﴿٢٠٣﴾

203. Kisha watasema: Je, sisi tutapewa muhula?

 

 

 

أَفَبِعَذَابِنَا يَسْتَعْجِلُونَ ﴿٢٠٤﴾

204. Je, wanahimiza Adhabu Yetu?

 

 

 

أَفَرَأَيْتَ إِن مَّتَّعْنَاهُمْ سِنِينَ ﴿٢٠٥﴾

205. Je, unaonaje kama Tukiwastarehesha miaka.

 

 

 

ثُمَّ جَاءَهُم مَّا كَانُوا يُوعَدُونَ ﴿٢٠٦﴾

206. Kisha yakawajia yale waliyokuwa wanaahidiwa.

 

 

 

مَا أَغْنَىٰ عَنْهُم مَّا كَانُوا يُمَتَّعُونَ ﴿٢٠٧﴾

207. Hayatowafaa yale waliyokuwa wakistareheshewa.

 

 

 

وَمَا أَهْلَكْنَا مِن قَرْيَةٍ إِلَّا لَهَا مُنذِرُونَ ﴿٢٠٨﴾

208. Na Hatukuangamiza mji wowote isipokuwa ulikuwa na waonyaji.

 

 

 

ذِكْرَىٰ وَمَا كُنَّا ظَالِمِينَ ﴿٢٠٩﴾

209.  Ni ukumbusho na Hatukuwa madhalimu.

 

 

 

وَمَا تَنَزَّلَتْ بِهِ الشَّيَاطِينُ ﴿٢١٠﴾

210. Na wala hawakuteremka nayo (hii Qur-aan) mashaytwaan.

 

 

 

وَمَا يَنبَغِي لَهُمْ وَمَا يَسْتَطِيعُونَ ﴿٢١١﴾

211. Na wala haipasi kwao na wala hawawezi.

 

 

 

إِنَّهُمْ عَنِ السَّمْعِ لَمَعْزُولُونَ ﴿٢١٢﴾

212. Hakika wao bila shaka wametengwa mbali kuisikiliza.

 

 

 

فَلَا تَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ فَتَكُونَ مِنَ الْمُعَذَّبِينَ ﴿٢١٣﴾

213. Basi usiombe pamoja na Allaah mwabudiwa mwengine ukaja kuwa miongoni mwa watakaoadhibiwa.

 

 

 

وَأَنذِرْ عَشِيرَتَكَ الْأَقْرَبِينَ ﴿٢١٤﴾

214. Na onya (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) jamaa zako wa karibu.[10]

 

 

 

وَاخْفِضْ جَنَاحَكَ لِمَنِ اتَّبَعَكَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ ﴿٢١٥﴾

215. Na inamisha ubawa wako kwa anayekufuata miongoni mwa Waumini.

 

 

 

فَإِنْ عَصَوْكَ فَقُلْ إِنِّي بَرِيءٌ مِّمَّا تَعْمَلُونَ ﴿٢١٦﴾

216. Wakikuasi, basi sema: Hakika mimi niko mbali na hayo mnayoyatenda.

 

 

 

وَتَوَكَّلْ عَلَى الْعَزِيزِ الرَّحِيمِ ﴿٢١٧﴾

217. Na tawakali kwa Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Kurehemu.

 

 

 

الَّذِي يَرَاكَ حِينَ تَقُومُ ﴿٢١٨﴾

218.  Ambaye Anakuona wakati unaposimama.

 

 

 

وَتَقَلُّبَكَ فِي السَّاجِدِينَ ﴿٢١٩﴾

219. Na mageuko yako katika wenye kusujudu. 

 

 

 

إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ ﴿٢٢٠﴾

220. Hakika Yeye Ndiye Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote.

 

 

 

هَلْ أُنَبِّئُكُمْ عَلَىٰ مَن تَنَزَّلُ الشَّيَاطِينُ ﴿٢٢١﴾

221. Je, nikujulisheni wanaowateremkia mashaytwaan?

 

 

 

تَنَزَّلُ عَلَىٰ كُلِّ أَفَّاكٍ أَثِيمٍ ﴿٢٢٢﴾

222. Wanateremka juu ya kila mzushi mkubwa mwingi wa kutenda dhambi. 

 

 

 

يُلْقُونَ السَّمْعَ وَأَكْثَرُهُمْ كَاذِبُونَ ﴿٢٢٣﴾

223. Wanaotega sikio na wengi wao ni waongo.

 

 

 

وَالشُّعَرَاءُ يَتَّبِعُهُمُ الْغَاوُونَ ﴿٢٢٤﴾

224. Na washairi wanafuatwa na wapotofu.

 

 

 

أَلَمْ تَرَ أَنَّهُمْ فِي كُلِّ وَادٍ يَهِيمُونَ ﴿٢٢٥﴾

225. Je, huoni kwamba wao katika kila bonde wanatangatanga?

 

 

 

وَأَنَّهُمْ يَقُولُونَ مَا لَا يَفْعَلُونَ ﴿٢٢٦﴾

226. Nao wanasema yale wasiyoyafanya.

 

 

 

إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَذَكَرُوا اللَّـهَ كَثِيرًا وَانتَصَرُوا مِن بَعْدِ مَا ظُلِمُوا ۗ وَسَيَعْلَمُ الَّذِينَ ظَلَمُوا أَيَّ مُنقَلَبٍ يَنقَلِبُونَ ﴿٢٢٧﴾

227. Isipokuwa wale walioamini na wakatenda mema, na wakamdhukuru Allaah kwa wingi, na wakapata nusura baada ya kudhulumiwa. Na hivi karibuni watakuja kujua wale waliodhulumu mgeuko gani watakaogeuka.[11]

 

 

 

 

 

[1] الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah):

 

Hizi ni herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Tanbihi ya Al-Baqarah (2:1).

 

[2] Maana Ya "آيَةٌ" :

 

Neno hili limekariri katika Aayah kadhaa kwenye Suwrah hii, na pia limetajwa kwa wingi  katika Suwrah nyenginezo. Na mara limetajwa kwa umoja آيَة (Aayah) na mara kwa wingi  آيات (Aayaat). Rejea kupata mifano katika Suwrah An-Nahl (16:11-13), Ar-Ruwm (30:20-25), Ar-Ra’d (13:3-4), Al-Jaathiyah (45:3-5).

 

Maana zake ni nyingi kutegemea na muktadha. Nazo ni kama ifuatavyo:

 

(i) Aayah au Aayaat za Qur-aan (ii) Ishara (iii) Dalili (iv) Burhani (dalili za wazi kabisa) (v) Hoja (vi) Muujiza (vii) Mazingatio (viii) Mafunzo. Na maana nyenginezo.

 

[3] Baadhi Ya Visa Vya Rusuli (عليهم السّلام)  Katika Suwrah Hii:  

Suwrah Ash-Shu’araa ni miongoni mwa Suwrah ambazo vimetajwa  visa vya Rusuli kadhaa na kaumu zao. Rusuli hao ni wafuatao: Muwsaa na Haaruwn, Ibraahiym, Nuwh, Huwd, Swaalih, Luutw, Shu’ayb (عليهم السّلام). Na Suwrah nyenginezo ambazo vimetajwa visa vya Rusuli hao na Manabii wengineo ni Suwrah zifuatazo: Al-A’raaf, Yuwnus, Huwd, Al-Anbiyaa, An-Naml, Al’Ankabuwt, Asw-Swaffaat, Swaad, Adh-Dhaariyaat, Al-Qamar.

 

[4] Firawni Kumpachika  Nabiy Muwsaa (عليه السّلام) Sifa Ovu:

 

Kukanusha kwake Firawni Risala ya Allaah, kulimfanya ampachike sifa ovu Nabiy Muwsaa (عليه السّلام). Mara aseme ni mchawi mjuzi, mara majnuni, mara muongo. Rejea Adh-Dhaariyaat (51:52) kwenye maelezo bayana. Na pia rejea Ghaafir (40:24), Al-A’raaf (7:109), Al-Israa (17:101).

 

[5] Hukmah:

 

Kumjua Allaah na Mipaka Yake, ilimu nyingi ya Dini yenye ufaqihi, ufahamu wa kina, busara, na utambuzi wa Sharia (hukumu) ya halali na haramu, na uwezo wa kuhukumu baina ya watu.

 

[6] Moyo Uliosalimika:

 

Aayah namba (88-89) inataja Siku ya Qiyaamah watu watakapofufuliwa kila mtu akiwa pekee. Hayatamfaa mali wala watoto isipokuwa atakayemfikia Allaah na moyo uliosalimika. Na moyo uliosalimika ni ule uliosalimika na shirki, kufru, unafiki, kutilia shaka Dini ya Allaah, kuifanyia istihzai Dini ya Allaah, kila aina ya maasi na madhambi, bid’ah na maovu yote mengineyo.

 

Na moyo uliosalimika ni kama walivyosema ‘Ulamaa na baadhi ya Salaf kuwa, ni moyo wenye ikhlaasw, ilimu, yakini, mapenzi ya Allaah na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa kufuata amri zao na kujiepusha na makatazo yao, na mapenzi ya kupenda khayraat.

Na zifuatazo ni baadhi ya kauli za ‘Ulamaa kuhusiana na moyo huu:

 

(i) Imaam Ibn Kathiyr: Ni moyo uliosalimika na uchafu na ushirikina.

 

(ii) Muhammad bin Siyriyn: Ni moyo unaotambua kuwa Allaah ni Haqq, na kwamba Saa (Qiyaamah) itafika tu hakuna shaka ndani yake, na kwamba Allaah Atafufua walioko makaburini.

 

(iii) Ibn ‘Abbaas: Ni moyo uliojistahi unaoshuhudia Laa ilaaha illa-Allaah.

 

(iv) Sa’iyd Al-Musayyib: Ni moyo wenye uzima, nao ni moyo wa Muumini, kwa sababu moyo wa kafiri na mnafiki una maradhi kama Anavyosema Allaah katika Al-Baqarah (2:10)]

 

(v) Abu ‘Uthmaan An-Niysaabuwriy: Ni moyo usio na chembe ya bid’ah ndani yake, uliotuama kwenye Sunnah.

 

(vi) Mujaahid, Al-Hasan na wengineo: Ni moyo uliosalimika na shirki.

 

Kinyume chake ni moyo uliotajwa katika Qur-aan kuwa una maradhi. Rejea Muhammad (47:20) kwenye maelezo na rejea mbalimbali.

 

Rejea pia Al-Hajj (22:46) ambako kuna maelezo na ufafanuzi wa Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):

فَإِنَّهَا لَا تَعْمَى الْأَبْصَارُ وَلَـٰكِن تَعْمَى الْقُلُوبُ الَّتِي فِي الصُّدُورِ ﴿٤٦﴾

Kwani hakika hayapofuki macho, lakini zinazopofuka ni nyoyo zilizomo vifuani.

 

[7] Watu Wa Al-Aykah:

 

Maana ya Aykah, ni miti mingi iliyosongomana, na kauli iliyo sahihi kabisa ni watu wa Madyan. Na Nabiy Shu’ayb (عليه السّلام)  alikuwa miongoni mwao. Lakini Allaah (سبحانه وتعالى) hapa Hakusema: “Ndugu yao Shu’ayb” kama Alivyotaja hivyo kwa Rusuli wengineo kina Nabiy Nuwh, Huwd, Swaalih na Luutw (عليهم السلام)  katika Aayah zilizotangulia, kwa sababu watu wake Shu’ayb, wamehusishwa na ibaada hiyo ya miti. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

Na Watu wa Al-Aykah wametajwa pia katika Suwrah (Al-Hijr 15:78), (Swaad 38:13), (Qaaf 50:14). Na watu wa Shu’ayb wametajwa pia katika Suwrah (Al-A’raaf 7:85),  (Huwd 11:84), (Al-‘Ankabuwt 29:36). Uasi wao ulikuwa ni: Shirki, dhulma, kughushi katika mizani za kupimia chakula, ufisadi mbalimbali katika nchi, kuvuka mipaka ya kuasi na mengineyo. Waliteketezwa kwa adhabu za tetemeko la ardhi na ukelele angamizi; adhabu ambazo ziliwaangusha kifudifudi majumbani mwao wakafilia mbali.

 

[8] Siku Ya Kivuli:

 

Siku ya kivuli imekusudiwa kama ilivyotajwa katika Tafsiyr ifuatayo: “Wakaendelea kumkanusha (Nabiy wao Shu’ayb), likawapata wao joto kali, wakawa wanatafuta mahali pa hifadhi (pa kivuli) ili wajifinike. Kikawafinika kiwingu (kama kivuli), kikawapatia ubaridi na upepo laini, na walipokusanyika chini yake, moto uliwawakia na ukawachoma, basi hapo yakawa maangamivu yao wote katika siku yenye kitisho kikali.[Tafsiy Al-Muyassar]

 

[9] Maana Za Ruwh Katika Qur-aan:

 

Rejea An-Nahl (16:2).

 

[11] Washairi Waliohidika:

 

Allaah (سبحانه وتعالى)
Amewavua kati ya hao washairi, wale washairi waliohidika kwa kuamini na kufanya matendo mema, na wakamdhukuru Allaah kwa wingi, wakatunga mashairi juu ya kumpwekesha Allaah (
سبحانه وتعالى) na kumsifu na Kumhimidi Yeye, Mwenye   kumtetea Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم), wakasema maneno ya busara yenye mawaidha na adabu nzuri, na wakaunusuru Uislamu, wakawa wanamtukana anayeutukana Uislamu, au anayemtukana Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa kuwaraddi washairi makafiri. Na watajua wale waliozidhulumu nafsi zao kwa ushirikina na matendo ya uasi, wakawadhulumu wasiokuwa wao, kwa kuwanyima haki zao, au kuwafanyia uadui, au tuhuma za urongo, ni marejeo gani ya shari na maangamivu watakayorejea. Kwa kweli, hayo ni mageuko mabaya. [Tafsiyr Al-Muyassar]

 

 

Share