Mwanangu Kaoa Mbali Lakini Hataki Kwenda Kwa Mkewe

SWALI:

Assalam alaykum ndugu zangu wote wa alhidaaya Swala langu ni: Mimi na mtoto wangu tunaishi Canada Miaka mitatu iliyo pita amekwenda Africa kuowa kwa ridhaa yake na kwa kumpenda Mwanamke mwenyewe, lakin bado hajaingia ndani , tokea mwaka huo alioowa hajenda nyumbani mpaka hivi leo lakini huyo mume anamwangalia mkewe  kiasi kidogo  ,lakin kila nikimwambia aenda kwa mkewe Africa hataki na nikimwambia kwenye nyumba tunagombana... Je shekh naomba msaada wenu munisaidie kuhusu swala hili?

Naomba nijibiwe masaalam

 
JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako hili kuhusu mahusiano ya kijamii. Suala lako limetupatia utata kidogo kwani ibara yako “Miaka mitatu iliyopita amekwenda Afrika kuoa kwa ridhaa yake na kumpenda mwanamke mwenyewe, lakini bado hajaingia ndani”. Hii kauli inamfanya mtu aulize maswali kadhaa. Je, ikiwa alimpenda kwa nini hakuingia ndani? Je, kuna kitu chochote alichokiona au kukijua kuhusu huyo mwanamke alipomuona? Je, walikuwa wanajuana kabla? Je, alishindwa kumuingia kwa kuwa hana uwezo huo? Je, mushawahi kuzungumza ni kwa nini hajaingia ndani? Je, baada ya Nikaah, wanandoa hawa wawili walizungumza na kuafikiana kuwa wasifanye tendo la kimapenzi mpaka baada ya muda fulani?

Haya ni baadhi ya maswali ambayo inafaa kupatiwa majibu kabla ya sisi kuweza kukupatia nasaha muafaka kuhusu tatizo hilo. Huenda kuwa alimuona msichana kwa kutumiwa picha, na pindi alipomuona akaona siye kama yule hivyo mapenzi yake yakafifia na akaona asimuharibie maisha yake kwa kuingia ndani kisha amuache. Ikiwa alishindwa kumuingilia au maume yake hayafanyi kazi hayo ni masuala ya ugonjwa na madaktari wanaweza kumtibu 

Ikiwa anaona huyo mwanamke hamfai, haifai kwa mume kumtesa kwa kumfunga bila kustarehe naye. Huku ni kumdhalilisha na kumdhulumu na yote mawili hayafai kwa Muislamu kumfanyia nduguye Muislamu. Inatakiwa kijana wako afanye uamuzi kwa kumuweka kama mke ima kwa kusafiri kila baada ya muda Afrika au amchukue mkewe Canada. Miaka 3 ni mingi kwa mwanamke aliyeolewa kukaa peke yake bila kuingiliwa. Kwa madhara anayopata msichana ana haki ya kwenda kwa Qaadhi au Shaykh yeyote anayeshughulika na mas-ala ya ndoa amshitakie na kutaka talaka. Kufanya kwake hivyo ni kujikomboa na dhulma pamoja na madhara. Na kwa sababu ya uvumilivu wake kwa muda wote huo Allaah Aliyetukuka Atmpatia badali iliyo nzuri.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share