102 - At-Takaathur
التَّكَاثُر
102-At-Takaathur
102-At-Takaathur: Utangulizi Wa Suwrah
بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ
أَلْهَاكُمُ التَّكَاثُرُ ﴿١﴾
1. Kumekughafilisheni (na utiifu wa Allaah kwa) kushindana kukithirisha (mali na watoto).
حَتَّىٰ زُرْتُمُ الْمَقَابِرَ ﴿٢﴾
2. Mpaka muingie makaburini.
كَلَّا سَوْفَ تَعْلَمُونَ ﴿٣﴾
3. Laa hasha! Mtakuja kujua.
ثُمَّ كَلَّا سَوْفَ تَعْلَمُونَ ﴿٤﴾
4. Kisha laa hasha! Mtakuja kujua.
كَلَّا لَوْ تَعْلَمُونَ عِلْمَ الْيَقِينِ ﴿٥﴾
5. Laa hasha! Lau mngelijua ujuzi wa yakini.[1]
لَتَرَوُنَّ الْجَحِيمَ ﴿٦﴾
6. Bila shaka mtauona moto uwakao vikali mno.
ثُمَّ لَتَرَوُنَّهَا عَيْنَ الْيَقِينِ ﴿٧﴾
7. Kisha kwa hakika mtauona kwa jicho la yakini.
ثُمَّ لَتُسْأَلُنَّ يَوْمَئِذٍ عَنِ النَّعِيمِ ﴿٨﴾
8. Kisha bila shaka mtaulizwa Siku hiyo kuhusu neema.[2]
[1] Ujuzi Wa Kweli:
Lau mngeyajua yaliyo mbele yenu kwa ujuzi unaofika nyoyoni, msingelighafilika kwa kushughulika na kukithirisha (mali) na mngelikimbilia kutenda mema. [Tafsiyr As-Sa’diy]
Siyo namna hii inatakiwa iwashughulishe kushindana kwa wingi wa mali. Lau mnajua kikweli, basi mngalirudi nyuma na mngelikimbilia haraka kuokoa nafsi zenu kutoka kwenye maangamivu. [Tafsiyr Al-Muyassar]
[2] Kutokushukuru Neema Na Kutokuzitumia Katika Njia Za Kumridhisha Allaah:
Neema mlizotumia katika kustarehe nazo katika dunia hii, je, mlishukuru na mkatimiza haki za Allaah, na wala hamkuzitumia katika maasi ili Akupeni neema kubwa na bora kuliko hizo? Au mlidanganywa nazo na hivyo mkashindwa kushukuru neema hizo, na labda mkazitumia kumuasi Allaah. Atakuadhibuni kwazo kama Anavyosema katika Kauli Yake nyengine:
وَيَوْمَ يُعْرَضُ الَّذِينَ كَفَرُوا عَلَى النَّارِ أَذْهَبْتُمْ طَيِّبَاتِكُمْ فِي حَيَاتِكُمُ الدُّنْيَا وَاسْتَمْتَعْتُم بِهَا فَالْيَوْمَ تُجْزَوْنَ عَذَابَ الْهُونِ بِمَا كُنتُمْ تَسْتَكْبِرُونَ فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَبِمَا كُنتُمْ تَفْسُقُونَ﴿٢٠﴾
Na siku watakaposimamishwa hadharani wale waliokufuru kwenye moto (waambiwe): Je, mshamaliza vizuri vyenu katika uhai wenu wa dunia na mshajistarehesha navyo? Basi leo mtalipwa adhabu ya udhalilifu kwa vile mlivyokuwa mkitakabari katika ardhi bila ya haki, na kwa ufasiki mliokuwa mnaufanya. [Al-Ahqaaf (46:20)]
[Tafsiyr As-Sa’diy]
Rejea Al-Qalam (68:17) kwenye mafunzo yanayotokana na visa viwili vya watu wa shamba walioshukuru neema za Allaah kwa kuzitolea swadaqa, na kinyume chake kuhusu kukufuru neema za Allaah kama kutokuzitolea swadaqa kwa masikini na wahitaji.