02-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Shirki Ni Aina mbili Na Tofauti Zake

 

إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ

Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!

02- Shirki Ni Aina mbili Na Tofauti Zake

Alhidaaya.com

 

 

Shirki ni aina mbili; shirki kubwa na shirki ndogo.

 

1-Shirki Kubwa inamtoa mtu nje ya Uislamu, ‘amali zake zote zinaporomoka, mwenye kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa shirki kubwa huwa ni halali damu yake, na mali yake na ni mwenye kudumu Motoni ikiwa hatotubia kabla ya kufariki kwake. Na dhambi ya shirki kubwa ni dhambi pekee ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Hamsamehi mja atakapokufa bila kutubia. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ 

Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae. [An-Nisaa: 48]

 

Shirki kubwa ni kuelekeza ‘ibaadah na kuomba du’aa kwa asiyekuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Washirikina wao ndio kabisa hawamwabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) japokuwa huenda wengine wanaamini kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ndiye Muumba kama walivyoamini hivyo washirikina wa Makkah. Shirki yao imethibiti katika Uluwhiyyah (‘ibaadah) pale walipoabudu masanamu wakidai kuwa yanawakurubisha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kama ilivyotajwa katika Qur-aan:

 

وَالَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ

na wale waliojichukulia badala Yake walinzi (wakisema): “Hatuwaabudu isipokuwa ili wapate kutukurubisha kwa Allaah tumkaribie”  [Az-Zumar: 3]

 

Wengine ndio wamemshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na viumbe Vyake wakawafanya ni ilaah (waabudiwa) wao. Juu ya hayo, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anamghufuria yeyote yule anayerudi kutubia Kwake baada ya kufuru na shirki kubwa kama hizo.  Dalili ni kauli zifuatazo katika Qur-aan:

 

لَقَدْ كَفَرَ الَّذِينَ قَالُوا إِنَّ اللَّـهَ هُوَ الْمَسِيحُ ابْنُ مَرْيَمَ ۖ وَقَالَ الْمَسِيحُ يَا بَنِي إِسْرَائِيلَ اعْبُدُوا اللَّـهَ رَبِّي وَرَبَّكُمْ ۖ إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ ۖ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ﴿٧٢﴾

Kwa yakini wamekufuru wale waliosema: “Hakika Allaah ni Al-Masiyh mwana wa Maryam.” Na Al-Masiyh alisema: “Enyi wana wa Israaiyl! Mwabuduni Allaah, Rabb wangu na Rabb wenu. Hakika mwenye kumshirikisha Allaah bila shaka Allaah Atamharamishia Jannah, na makazi yake yatakuwa ni motoni. Na madhalimu hawatopata yeyote mwenye kunusuru.”

 

لَّقَدْ كَفَرَ الَّذِينَ قَالُوا إِنَّ اللَّـهَ ثَالِثُ ثَلَاثَةٍ ۘ وَمَا مِنْ إِلَـٰهٍ إِلَّا إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ ۚ وَإِن لَّمْ يَنتَهُوا عَمَّا يَقُولُونَ لَيَمَسَّنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٧٣﴾

Kwa yakini wamekufuru wale waliosema: “Hakika Allaah ni watatu wa utatu.” Na hali hapana Muabudiwa wa haki isipokuwa Ilaah Mmoja Pekee. Na wasipoacha yale wanayoyasema, bila ya shaka itawagusa wale waliokufuru miongoni mwao adhabu iumizayo.

 

أَفَلَا يَتُوبُونَ إِلَى اللَّـهِ وَيَسْتَغْفِرُونَهُ ۚ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٧٤﴾

Je, hawatubii kwa Allaah na wakamwomba maghfirah? Na Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [Al-Maaidah: 72-74]

 

2-Shirki Ndogo: Hii inajulikana kama riyaa, nayo ni kufanya ‘ibaadah au kutenda amali lakini kwa niyyah ya kujionyesh a kwa watu. Shirki hii haimtoi mtu nje ya Uislamu bali ‘amali zake huporomoka na, ni mwenye kuadhibiwa Motoni kwa kadiri ya madhambi yake.

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amewahofia Swahaabah aina hii ya shirki:

 

عن مَحْمُودِ بْنِ لَبِيدٍ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ إنَّ أخوَفَ ما أخافُ عليكم الشِّركُ الأصغرُ، قالوا: وما الشِّركُ الأصغر؟ قال: الرِّياءُ، يقولُ اللهُ عزَّ وجلَّ لأصحابِ ذلك يومَ القيامةِ إذا جازَى النَّاسَ اذهبوا إلى الَّذين كنتم تُرائون في الدُّنيا فانظُروا هل تجِدون عندهم جزاءً؟"  - صححه الألباني في السلسلة الصحيحة(951 )

Imepokelewa kutoka kwa Mahmuwd bin Labiyd ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: Hakika ninachokihofia kwenu zaidi ni shirki ndogo. Wakasema: Ni ipi hiyo shirki ndogo? Akasema: Ar-Riyaa. Allaah ('Azza wa Jalla) Atawaambia watu wa Siku ya Qiyaamah pale watakapolipwa watu jazaa: Nendeni kwa wale mliokuwa mkijionyesha kwa ‘amali zenu duniani kisha tazameni je, mtakuta kwao jazaa? [Ahmad na ameisahihisha Shaykh Al-Albaaniy katika Silsilat Al-Hadiyth Asw-Swahiyhah (951)]

 

 

Share