03-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Shirki Ndogo - Riyaa (Kujionyesha)

 

إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ

Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!

 

03- Shirki Ndogo : Riyaa (Kujionyesha)

 

www.alhidaaya.com

 

 

‘Amali zote zinahitaji kutangulizwa na niyyah safi. Hadiyth mashuhuri ambayo ‘Ulamaa wamesema kuhusu Hadiyth hii kwamba ni nusu ya ya Dini kama alivyosema Imaam Abu Daawuwd, kwani Dini inakusanya vilivyo dhahiri kama vitendo na visivyo dhahiri kama niyyah. 

 إِنَّما الأَعْمَالُ بالنِّيَّاتِ وإنَّما لكُلِّ امْرِىءٍ ما نَوَى،    

Hakika ‘amali inategemea (malipo) kwa niyyah na kila mtu atapata kwa mujibu wa kila alichotilia niyyah. [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

Imaam Ash-Shaafi’iy naye kasema Hadiyth hii ni nusu ya elimu. Naye Imaam Ahmad na Imaam Ash-Shaafi’iy wamesema Hadiyth hii inakusanya moja ya tatu ya elimu. Imaam Al-Bayhaqiy akafafanua maneno yao hayo kwa kusema, “Hayo ni kwa sababu, mtu huchuma thawabu kwa moyo wake, ulimi na mwili wake. Hivyo, niyyah inahusiana na moja ya viungo hivyo vitatu. [Ibn Hajr, Fat-h Al-Baariy, mj. 1, uk. 11]

 

Na sharti za kupokelewa ‘amali za mja ni ikhlaasw, niyyah safi ya ‘amali kwa kufuata amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kama Anavyoamrisha:

 

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَۚ وَذَٰلِكَ دِينُ الْقَيِّمَةِ ﴿٥﴾

Na hawakuamrishwa isipokuwa wamwabudu Allaah wenye kumtakasia Dini, wenye kujiengua na upotofu kuelemea Dini ya haki na wasimamishe Swalaah na watoe Zakaah; na hiyo ndiyo Dini iliyosimama imara. [Al-Baayyinah: 5]

 

 

Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

فَمَن كَانَ يَرْجُو لِقَاءَ رَبِّهِ فَلْيَعْمَلْ عَمَلًا صَالِحًا وَلَا يُشْرِكْ بِعِبَادَةِ رَبِّهِ أَحَدًا ﴿١١٠﴾

Hivyo anayetaraji kukutana na Rabb wake, basi na atende ‘amali njema na wala asimshirikishe yeyote katika ‘ibaadah za Rabb wake.” [Al-Kahf: 110]

 

Yaani asifanye riyaa (kujionyesha) ‘amali zake kwa watu kama Swalaah, Hajj, Swawm, Zakaah, Swadaqah, kusoma Qur-aan, kufanyia watu wema na ihsaan kwa ajili ya kusifiwa, kujitukuza au kuonekana ni mwema na sifa kama hizo za riyaa.

 

Na Rasuli wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) aliwatahadharisha Swahaabah (Radhwiya Allaahu ‘anhum) kuhusu riyaa. Siku ya Qiyaamah pindi mtu atakapokuja na ‘amali zake itatambulikana kama zilikuwa za ikhlaasw au za riyaa kwani Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema katika Hadiyth:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وآله وسلم): ((إِنَّ اللَّهَ لاَ يَنْظُرُ إِلى أجْسمِكُمْ وَلاَ إِلَى صُوَرِكُمْ وَلَكِنْ يَنْظُرُ إِلَى قُلُوبِكُمْ)) رواه مسلم

Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika Allaah Hatazami viwiliwili vyenu wala sura zenu, lakini Anatazama nyoyo zenu)). [Muslim]

 

Nyoyo ndizo zitakazodhihirisha ikhlaasw ya mtu kwani humo ndipo kunapofichika shirki kama ilivyobainishwa katika Hadiyth ifauatayo:

 

عَنْ أَبِي سَعِيدٍ، قَالَ: خَرَجَ عَلَيْنَا رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ وَنَحْنُ نَتَذَاكَرُ الْمَسِيحَ الدَّجَّالَ، فَقَالَ: ((أَلا أُخْبِرُكُمْ بِمَا هُوَ أَخْوَفُ عَلَيْكُمْ عِنْدِي مِنَ الْمَسِيحِ الدَّجَّالِ؟)) قَالَ: قُلْنَا: بَلَى! فَقَالَ: ((الشِّرْكُ الْخَفِيُّ، أَنْ يَقُومَ الرَّجُلُ يُصَلِّي، فَيُزَيِّنُ صَلاتَهُ، لِمَا يَرَى مِنْ نَظَرِ رَجُلٍ)) سنن ابن ماجه (4204).

Imepokelewa kutoka kwa Abu Sa’iyd (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) alikuja kwetu wakati tulikuwa tukijadiliana kuhusu Dajjaal, akasema: ((Je, niwajulisheni kile nikikhofiacho zaidi kwenu kuliko hata (hatari za) Dajjaal?)) Tukasema: Ndio. Akasema: ((Basi ni shirki iliyojificha. Mtu anasimama kuswali, anaipamba na kuiremba Swalaah yake kwa kujua kuwa kuna watu wanamtazama)) [Sunan Ibn Maajah (4204)]

 

Hiyo ni kama sifa ya wanafiki wanaomhadaa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kama Anavyosema:

 

 إِنَّ الْمُنَافِقِينَ يُخَادِعُونَ اللَّـهَ وَهُوَ خَادِعُهُمْ وَإِذَا قَامُوا إِلَى الصَّلَاةِ قَامُوا كُسَالَىٰ يُرَاءُونَ النَّاسَ وَلَا يَذْكُرُونَ اللَّـهَ إِلَّا قَلِيلًا ﴿١٤٢﴾

Hakika wanafiki (wanadhani) wanamhadaa Allaah, na hali Yeye (Allaah) Ndiye Mwenye kuwahadaa. Na wanaposimama kuswali husimama kwa uvivu, wakijionyesha kwa watu na wala hawamdhukuru Allaah isipokuwa kidogo tu. [An-Nisaa: 142]

 

 

 

Share