21-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Kutabiria Ya Ghayb; Kheri, Shari, Nuksi, Unajimu

 

إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم

 

Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!

 

21-Kutabiria Ya Ghayb Ya Khayr Au Shari, Nuksi, Unajimu Na Kutazamia Kwa Mtabiri

Alhidaaya.com

 

 

 

Kubashiria mambo ya ghayb ni katika ujuzi wa ghayb ambayo hakuna mwenye ujuzi nayo isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kama Anavyosema Mwenyewe (‘Azza wa Jalla):

 

 

قُل لَّا يَعْلَمُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ الْغَيْبَ إِلَّا اللَّـهُ ۚ وَمَا يَشْعُرُونَ أَيَّانَ يُبْعَثُونَ ﴿٦٥﴾

Sema: “Hakuna aliyoko katika mbingu na ardhi ajuaye ghayb isipokuwa Allaah. Na wala hawatambui lini watafufuliwa.” [An-Naml: 65]

 

 

Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَعِندَهُ مَفَاتِحُ الْغَيْبِ لَا يَعْلَمُهَا إِلَّا هُوَ

Na Kwake (Allaah) zipo funguo za ghayb; hakuna azijuaye ila Yeye tu [Al-An’aam: 59]

 

Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

إِنَّ اللَّـهَ عِندَهُ عِلْمُ السَّاعَةِ وَيُنَزِّلُ الْغَيْثَ وَيَعْلَمُ مَا فِي الْأَرْحَامِ ۖ وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ مَّاذَا تَكْسِبُ غَدًا ۖ وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ بِأَيِّ أَرْضٍ تَمُوتُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ ﴿٣٤﴾

Hakika Allaah Ana elimu ya Saa (Qiyaamah), na Anateremsha mvua na Anajua yale yaliyomo katika tumbo la uzazi na nafsi yoyote haijui nini itachuma kesho, na nafsi yoyote haijui itafia katika ardhi gani, hakika Allaah ni Mjuzi wa yote, Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika [Luqmaan: 34]

 

 

Na kutabiria au kubashiria ya ghayb ni miongoni mwa shirki kubwa inayomtoa mtu nje ya Uislaam kwa dalili, kauli za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضي الله عنه،  عَنْ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم قَالَ: ((مَنْ أَتَى كَاهِنًا، أَوْ عَرَّافًا، فَصَدَّقَهُ بِمَا يَقُولُ، فَقَدْ كَفَرَ بِمَا أُنْزِلَ عَلَى مُحَمَّدٍ صلى الله عليه وسلم ))

Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Atakayemwendea kahini au mpigaji ramli akamuamini asemayo, basi atakuwa ameshakufuru yale aliyoteremshiwa nayo Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).” [Ahmad, na Aswhaabus-Sunan wanne, na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Targhiyb wat-Tarhiyb (3047)]

 

Na kwa dalili pia kuwa Swalaah hazikubalikiwi siku arubaini!

 

مَنْ أَتَى عَرَّافًا فَسَأَلَهُ عَنْ شَيْءٍ لَمْ تُقْبَلْ لَهُ صَلَاةٌ أَرْبَعِينَ لَيْلَةً

((Atakayekwenda kwa mtabiri akamuuliza kitu haitokubaliwa Swalaah yake siku arubaini)) [Muslim]

 

Basi jiulize ndugu Muislaam unayemshirikisha Allaah! Je, itakuwaje pindi akikufikia Malak-Al-Mawt (Malaika wa kufisha) akakutoa roho yako kipindi hicho wakati uko nje ya Uislaam?

 

Mifano ya njia zinazotabiriwa: 

 

1- Kwenda kwa mtabiri:

 

 

Mtabiri hutazamia kwa mikono na kumbashiria mtu mazuri yatakayomfika siku za mbele au mabaya yatakayomsibu mtu. Hutazamia ima kwa vikombe baada ya huyo mtu anayetazamiwa kunywa chai au kahawa ikabakishwa kidogo, basi huzungushwa kikombe chake cha chai au kahawa kisha hutabiriwa ya khayr au shari kumfikia. Au hutabiri kwa kuandika nambari katika vikaratasi, kwa nyota, au kutazamwa viganja vya mikono n.k.

 

2- Kutazamia kwa unajimu na kutangazwa kwenye magazeti na majarida (horoscope):

 

Pia, kuna wanaotabiri kwa njia ya unajimu (kutazamia nyota) kuhusiana na mwezi aliozaliwa mtu inayojulikana kama 'horoscope'.  Unajimu huu hutiwa magazetini na watu husoma kila mara kutabiri bahati zao au shari zitakazowasibu katika siku fulani. Wanadai kuwa sayari kama gemini, taurus, aries n.k. zinahusiana na mwezi wa mtu aliozaliwa na hivyo basi waliozaliwa katika sayari hizo siku hiyo kwao huwaathiri nafsi zao na kadhaa wa kadhaa.

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameharamisha unajimu:

 

 عن عبد الله بن عباس (رضي الله عنهما) عن النبي (صلى الله عليه وسلم): ((من اقتبس شعبةً من النجومِ فقد اقتبس شعبةً من السحرِ زاد ما زاد))

Amehadithia ‘Abdullaah bin ‘Abaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Atakayejichumia tawi katika ujuzi wa unajimu, atakuwa amejichumia tawi katika sihri, na itaendelea kuzidi na kuzidi.” [Abuu Daawuwd kwa Isnaad Swahiyh]

 

 

3- Kutabiri khayr au shari au nuksi kutokana na matukio fulani:

 

Ni mambo yanayotabiriwa na watu katika jamii za Kiislamu na kuyaitakidi kwamba ni mambo yatakayomtokea mtu. Mambo hayo huwa ima ya khayr au shari, au nuksi, mkosi, ukorofi n.k. Na hakika itikadi hizi miongoni mwa Waislaam zimekuwa kama ni jambo la kawaida  na ilhali ni jambo la khatari kabisa kwa kuwa ni miongoni mwa shirki kubwa ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Hamghufurii mtu asiporudi kutubia! Yanayotabiriwa yako mengi mno, ila haya yafuatayo ndio ambayo tumejaaliwa kuyajua na kuyanukuu:

 

a) Akitajwa mtu kisha hapo hapo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akajaalia huyo mtu atokee au asikike kwa simu n.k., basi hubashiriwa kuwa atakuwa na umri mrefu!

 

b) Jicho likimcheza mtu upande wa kushoto huamini kuwa itamfika shari na ikiwa upande wa kulia huamini kuwa itamfikia khayr! Na wengine husema: “Sharr ba’iyd na khayr qariyb”(shari iwe mbali na khayr iwe karibu).

 

c) Kusemwa: “Swallu ‘alan-Nabiy!” - inasemwa kwa ajili ya kuondosha jicho baya au husda! Na hutamkwa hivyo katika hali ya kuona jambo zuri, au katika sherehe za harusi kumkinga nayo bi harusi au wenye harusi. Pia kwa ajili ya kunyamazisha mzozano, au anapoona mtu jambo la ajabu n.k. Haya ni mambo ya bid’ah na inaingia katika shirki pia. Vile vile wanawake khaswa kusema kwao katika sherehe: “Aswalaatu was-salaamu ‘alaa habiybinaa Muhammad!” kisha hupigwa vigelegele! Haya pia ni katika bi’dah.

 

d) Pindi mtu akimuona paka mweusi basi inaitakidiwa kuwa siku hiyo itakuwa ni ya mkosi!

 

e) Mkono umkimuwasha mtu basi inabashiriwa kuwa kuna kupata pesa!

 

f) Akifagia mtu usiku basi inatabiriwa kuwa ni kuondosha baraka au kufukuza wageni!

 

g) Akipaliwa mtu hutabiriwa kuwa “anatajwa!”

 

h) Ukikata kucha zote pamoja (ya mikono na miguu) inatabiriwa kuwa shida zikija zitakuja zote pamoja!

 

i) Kushika mbao inaitakidiwa kuwa ni kuepusha hjicho baya na husda! Kwa hiyo unapotaja jambo zuri la kusifia jambo au mtu, itasemwa: “Shika mbao!”

 

j) Mtoto wa kike akivalishwa kofia ya mwanamume ni itikadi kuwa atakosa mahari! 

 

k) Mtu akipatwa na mtihani basi huambiwa akaoge na avue ile nguo kwani ile nguo ina mkosi na ikitokea kuirejea kuvaa ile nguo basi mtu huyo huwa na mashaka kupata tatizo tena. Hali hiyo hupelekea mtu kutoivaa tena ile nguo kwa kuamini akiivaa tu atapata tena mkosi!

 

l) Unapofagia ukapitishia ufagio kama kumsogezea taka binti basi ni itikadi kuwa hatoolewa! 

 

m) Mtoto akichetama na kujichungulia 'awrah (sehemu ya siri) yake, basi watu huamini kuwa mama yake atashika ujauzito!

 

Hizo ni baadhi ya itikadi potofu, za kishirikina na za kijaahiliyyah (zama za ujinga kabla ya Uislaam) kwa sababu washirikina walikuwa wanapotaka kufanya jambo kama vile kusafiri, walikuwa wanatabiria kwa Tatwayyur; (kubashiria mkosi kwa kumrusha ndege). Hurushwa ndege, basi pindi akiruka kuelekea upande wa kulia basi hubashiria kuwa ni khayr na pindi akiruka ndege huyo kuelekea kushoto, basi hubashiria ya shari na hivyo safari huvunjwa!

 

Ukaja Uislaam na kuharamisha shirki hiyo katika Qur-aan na Sunnah. Miongoni mwa Hadiyth za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):  

 

 عن عبد الله بن مسعود قال قال رسول الله صلى الله عليه وسلم : ((الطِّيَرَةُ شِركٌ، الطِّيَرَةُ شِركٌ، الطِّيَرَةُ شِركٌ))

Ibn Mas’uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kwamba: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Atw-Twiyarah (kutabiri nuksi, mikosi n.k) ni shirki, Atw-Twiyarah ni shirki, Atw-Twiyarah ni shirki.” [Swahiyh At-Targhiyb (3098)]

 

Atw-Twiyarah: Maana yake ni kutabiria khayr au kinga ya shari na zaidi inatumika kutabiria nuksi.

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza katika Hadiyth nyengineyo:

 

 

عنْ عُرْوَةَ بْنِ عامِرِ (رضي الله عنه) قال: ذُكِرتِ الطَّيَرَةُ عِنْد رَسُولِ اللَّه صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فقَالَ: ((أحْسَنُهَا الْفَألُ، وَلا تَرُدُّ مُسْلِماً، فَإذا رأى أحَدُكُمْ ما يَكْرَه ، فَلْيقُلْ: اللَّهُمَّ لا يَأتى بالحَسَناتِ إلاَّ أنتَ، وَلا يَدْفَعُ السَّيِّئاتِ إلاَّ أنْتَ، وَلا حوْلَ وَلا قُوَّةَ إلاَّ بك))  

‘Urwah bin ‘Aamir (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kwamba: Ilitajwa habari ya kupiga fali mbaya (mkosi) mbele ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Ilio bora zaidi ni kupiga fali nzuri, wala (kupiga fali mbaya) haimrudishi Muislaam (kutokutenda aliloazimia). Mmoja wenu atakapoona analolichukia, aseme: “Allaahumma laa yaa-tiy bil-hasanaat illa Anta, walaa yadfa’us-sayyiaat illa Anta, walaa hawla walaa quwwata illa Bika“ - Ee Allaah, hakuna anayeweza kuleta mambo mema isipokuwa ni Wewe, wala hakuna anayeweza kukinga mabaya isipokuwa ni Wewe. Hakuna uwezo (wa  kuepuka kutenda mabaya) wala nguvu (ya kutenda mema) isipokuwa ni Kwako.) [Hadiyth Swahiyh ameipokea Abu Daawuwd kwa isnaad Swahiyh]

 

Akasema pia: “Hakuna mkosi, na ni bora tegemea khayr (matumaini mema).” Wakauliza nini matumaini mema (matarajio ya kufanikiwa) Yaa Rasuwla-Allaah? Akasema: “Ni neno jema alisikialo mmoja wenu.” [Al-Bukhaariy]

 

Mas-alah haya ya kubashiria ghayb yanapasa kuzingatiwa kwa kina na kuazimiwa kuwafundisha watu khatari zake, kwa sababu watu wengi hawana ujuzi kuwa ni katika mambo ya kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) wakidhania kuwa ni mambo ya kawaida. Kwa hiyo ni waajib wa kila Muislamu anayesoma makala hizi kufanya juhudi kuwafikisha Waislamu waepukane na shirki hizi.

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amebainisha jinsi mambo kama haya yanavyomwepesisha mtu kuingia katika kufru:

 

عَنْ زَيْدِ بْنِ خَالِدٍ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ) قَالَ: صَلَّى لَنَا رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) صَلاةَ الصُّبْحِ بِالْحُدَيْبِيَةِ عَلَى إِثْرِ سَمَاءٍ كَانَتْ مِنَ اللَّيْلِ، فَلَمَّا انْصَرَفَ أَقَبْلَ عَلَى النَّاسِ، فَقَالَ ((هَلْ تَدْرُونَ مَاذَا قَالَ رَبُّكُمْ؟)) قَالُوا: اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَعْلَمَ. قَالَ: ((قَالَ أَصْبَحَ مِنْ عِبَادِي مُؤْمِنٌ بِي وَكَافِرٌ، فَأَمَّا مَنْ قَالَ مُطِرْنَا بِفَضْلِ اللَّهِ وَرَحْمَتِهِ، فَذَلِكَ مُؤْمِنٌ بِي كَافِرٌ بِالْكَوْكَبِ، وَأَمَّا مَنْ قَالَ مُطِرْنَا بِنَوْءِ كَذَا وَكَذَا، فَذَلِكَ كَافِرٌ بِي مُؤْمِنٌ بِالْكَوْكَبِ))

Zayd bin Khaalid (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kwamba: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alituswalisha Swalaah ya asubuhi Hudaybiyah baada ya usiku wa mvua. Alipomaliza akawakabili watu akasema: “Je, mnajua Rabb wenu Amesema nini?” Wakajibu: Allaah na Rasuli Wake ndio wajuao. Akasema: ‘Allaah Amesema: Baadhi ya waja Wangu wameamka leo wakiwa wenye kuniamini, na wengine wamekufuru. Aliyesema kuwa mvua ni kutokana na fadhila na Rahmah za Allaah, basi huyo ni mwenye kuniamini wala haamini nyota. Ama aliyesema: Tumenyeshewa mvua kutokana na nyota fulani, yeye ni mwenye kunikufuru na mwenye kuamini nyota.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

 

Share