Anaporitadi Mwanandoa; Je, Ndoa Itaendelea Au Itavunjika?
Anaporitadi Mwanandoa; Je, Ndoa Itaendelea Au Itavunjika?
SWALI:
Je wanandoa wawili mmoja wao atakaporitadi ndoa itaendelea au itakuwa imevunjika
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Ikiwa mmoja katika wanandoa akaamua kuacha dini kwa sababu zake zozote zile, au akatoka kwenye dini kwa kutamka maneno ya ukafiri au kutukana dini au kumtukuna Allaah au Rasuli Wake, au kufanyia istihzai Aayah za Allaah Ta’aalaa au Sunnah za Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), basi kutoka kwake huko kwenye dini naye yupo kwenye ndoa, ndoa hiyo inavunjika hapo hapo kwa kauli yenye nguvu zaidi.
Ikiwa mume ndiye aliyeritadi, Madh-hab ya Ash-Shaafi’iy na Hanbali wanaona ndoa itavunjika lakini mwanamke atakaa eda na huyo mume na ikiwa mume atarejea kwenye Uislamu wanaona mume anaweza kumrejea mke wake kabla ya eda yake kwisha. Ama eda ikiwa itakwisha kabla hajarudi kwenye Uislamu, basi atafunga ndoa upya.
Lakini upande wa Madh-hab ya Hanafi na Maaliki, wao wanaona ndoa inavunjika hapo hapo anaporitadi.
[Rejea, Al-Mughniy, 7/133; Al-Mawsuw‘ah Al-Fiqhiyyah, 22/198; Al-Inswaaf, 8/216; Kashshaaf Al-Qinaa‘, 5/121; Tuhfat Al-Muhtaaj, 7/328; Al-Fataawa Al-Hindiyyah, 1/339; Haashiyat Al-Dasuwqiy, 2/270.]
Wanachuoni vilevile wanaona kuwa ndoa inayovunjika kwa sababu ya kuritadi, haihesabiki ni talaka.
Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) anaeleza kuhusu yule aliyetoka kwenye Uislamu kwa sababu ya kuacha Swalaah, anaeleza kuwa kuna hali tatu kwa mtu kama huyo:
1. Ikiwa hali hiyo imetokea kabla ya ndoa kufungwa, ndoa hiyo itakuwa haipo tena na huyo mke hatoruhusika kuwa naye huyo aliyeacha kuswali.
2. Ikiwa hali hiyo imetokea baada ya ndoa kufungwa, na kabla hawajaingiliana, jambo ambalo linapelekea eda kuwa ni waajib, basi hapo ndoa itavunjika pindi tu yule mtu anapoacha kuswali.
3. Ikiwa hali hiyo itatokea baada ya ndoa kufungwa au baada ya wanandoa kuingiliana, jambo ambalo linaifanya eda kuwa ni waajib, inategemea kama eda imeisha au bado. Ikiwa alitubia na kuanza kuswali kabla ya eda kwisha, basi mke ataendelea kuwa wake, lakini ikiwa hajatubia kabla ya eda kwisha, basi ndoa itavunjika pale tu wakati alipotoka katika Uislamu – Allaah Aepushe-. Kwa hali hiyo, ikiwa atarejea kwenye Uislamu (kwa mujibu wa baadhi ya Wanachuoni) anaweza kumrejea mke wake akitaka, au (kwa mujibu wa Wanachuoni wengine) hawezi kumrejea. Kuna ikhtilaaf baina ya Wanachuoni katika suala hilo.
[Fataawa Nuwr ‘Alaa Ad-Darb]
Na Allaah Anajua zaidi.