Hukumu Ya Kuuza Ardhi Akijua Kuwa Itatumika Kwa Maasi

 

 

SWALI:

Nini hukmu ya kuuza ardhi ya halali, lakini huku nikijuwa kuwa mnunuzi anataka kujenga hoteli ya kitalii, na hivyo kuuzwa pombe na kulaza wageni
ambao watakuwa hawana mpaka? Tafadhali naomba nisaidiwe hili. Ndugu yen
u  .


 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani sana kwa ndugu yetu kwa swali hili nyeti ambalo limekuwa tatizo kwa jamii zetu zinazoishi katika maeneo ya mwambao wa Afrika Mashariki hasa Kenya na Tanzania. Tufahamu ya kwamba kuna mikakati kabambe ambayo imeandiliwa na wasiokuwa Waislamu katika kubadilisha maeneo hayo ili kuwepo wasiokuwa Waislamu wengi zaidi kuliko Waislamu. Hivyo, watu wa Magharibi na wasiokuwa Waislamu hata wale wanaoishi katika nchi hizo wananunua ardhi kwa fedha nyingi sana ili kufikia malengo yao hayo. Na ni ajabu kwa ule uchumi ulio chini sana katika nchi hizi kupatikana wanati (wananchi) ambao wanatoa bei mara dufu kwa ardhi ndogo sana katika maeneo ya Waislamu.

Mifano katika hili ipo mingi sana hata katika nchi na miji mengine nje ya eneo letu. Hebu hapa tutoe baadhi ya mifano hiyo ambayo baadae inawaletea shida nyingi Waislamu wakazi wa maeneo hayo:

Mji wa Hyderabad ambao upo kusini wa India, ni mji ambao kabla ya India kupata uhuru wake mwaka 1947 kulikuwa na Waislamu walio 90 – 95% lakini kwa sasa wamekuwa chini ya 40%. Serikali ya India ya Kibaniyani (Hindu) ilikuwa na mikakati kabambe hata kuwahamisha wasiokuwa Waislamu na kuwapatia makazi katika sehemu hiyo. Wananchi hao wageni katika eneo hilo walipatiwa usaidizi na serikali hiyo pamoja na kazi mpaka athari nyingi ya Kiislamu zimejaribiwa kubadilishwa.

Tazama Palestina jinsi ilivyochukuliwa kimabavu na Uingereza baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia mwaka 1917 na kisha kutunukiwa Israili kama hadiya kutoka kwa Uingereza. Kuanzia mwaka 1948, Wazeyuni wametumia mbinu zote ili kuhakikisha kuwa Wapalestina wametolewa kimabavu; kwa kuwaua viongozi, kuvunja nyumba za wenyewe, kukata miti ya matunda hasa mizeituni na tini, kuwatoa wenyeji kutoka katika nchi yao na vitimbi vyengine chungu nzima. Wenyeji wenyewe wamebakia kuishi katika mahema na kuzuiliwa haki za msingi. Katika miaka ya karibuni wanafanya vitimbi hata vya kuubomoa Msikiti wa Aqsa pamoja na kuwatoa wanaoishi katika mji wa Al-Quds (yaani Jerusalem) ili wabaki Wazeyuni peke yao.

Mikakati kama hiyo ndiyo inayofanywa katika nchi ya 'Iraaq na Afghanistaan kwa sasa. 

Tuje katika nchi ya Kenya, wakati wa Kenyatta katika mwaka wa 1971, watu kutoka bara walio kabila moja na rais huyo walipatiwa makazi karibu na kisiwa cha Lamu, kwa jina Mpeketoni. Serikali ikawasaidia kwa kuwapatia hifadhi ambayo ilikuwa haipo na shirika la Kikristo kutoka Ujerumani kuwasaidia kwa vifaa vya ukulima na usaidizi mwengine wa kifedha mpaka kwa sasa wamesimama imara kwa miguu miwili lakini bado wanaendelea kusaidiwa. Wazungu kutoka Ulaya walianza kununua ardhi katika kijiji cha Shella katika kisiwa cha Lamu na kwa kuwa walikuwa wakipatiwa fedha nyingi walianza kuuza ardhi mpaka kwa sasa wapo wazungu wengi wenye ardhi kuliko wenyeji waliokuwa 100% Waislamu. Isitoshe Malindi na Lamu zenyewe zimevamiwa na ardhi zao kununuliwa kwa kiasi kikubwa sana na hela wanayotoa hata kwa magofu ya Lamu huweza kununua nyumba kubwa za ghorofa katika mji wa Mombasa. Malindi imekuwa kama Italia na Lamu kuna kila aina ya Wazungu, na huenda baada ya miaka kumi kukawa hakuna Lamu tena. Mombasa pia nayo ina tatizo hilo hilo.

Hebu tutazame Tanzania, ukiangalia mambo yanavyoendelea ni kuwa Wakristo pamoja na mashirika yao wana mikakati kabambe kuhusu kuyabadilisha miji ya Waislamu. Kama Dar es Salaam katika miaka ya 1980 au hata miaka ya 1990 utaona kuwa katika mtaa wa Kariokoo kulikuwa na Waislamu takriban wote lakini sasa yapo maduka chungu nzima ya walokole ambao wanakodisha kwa hela nyingi. Tazama Tanga inakwenda pole pole na hata Zanzibar kumekuwa na mkurupuko wa wageni ambao wanabadili maadili ya Waislamu wa huko kwa kuleta tabia ngeni pamoja na kuchafua mazingira. Makanisa yanaongezeka na hata sasa hivi wananunua mashamba na kufanya miradi yao eti wanawasaidia wenyeji kwa kuwapatia matibabu, elimu na mambo mengineo.

Hivyo, ni muhimu kujua ya kwamba ni lazima tuwe na ghera na Dini yetu pamoja na sehemu zetu tulizozirithi kutoka kwa mababu zetu. Ni afadhali uuze ardhi kwa Muislamu hata kama utapata hela kidogo kuliko kuuza dunia yako kwa Akhera. Haifai kwa Muislamu kumuuzia asiyekuwa Muislamu ardhi eti anataka kujenga hoteli ya kitalii, kwani maasiya na madhambi yoyote yatakayofanyika humo basi nawe muuzaji utakuwa na fungu lako la madhambi. Na ndio Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anatutahadharisha katika Hadiyth iliyopokewa kwa Ibn Mas‘uud (Radhiya Allaahu 'anhu) ya kwamba Mtume (Swall Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakuna nafsi yeyote inayouliwa kwa dhulma isipokuwa yule mwanadamu wa kwanza (yaani Qaabil ambaye alimuua nduguye Haabiil) atapata sehemu yake ya madhambi (ya mauaji) kwani yeye ndiye wa mwanzo kuanzisha mauaji” (Al-Bukhaariy, Muslim na Ahmad).

Hivyo hivyo yule ambaye atauza ardhi yake ili itumike kwa maasiya aina yoyote yale atakuwa ni mwenye kupata madhambi kwa hilo. Ni bora zaidi kutouza kwa watu hao ambao wanataka kuanzisha miradi hiyo. Ikiwa huna budi kufanya hivyo, basi itabidi muandikiane kwa wakili na huyo mnunuzi kuhusu mambo ambayo hutotaka ardhi ile itumike. Na pindi atakapovunja mkataba basi ardhi hiyo itarudi kwako. Lakini hii njia ina vikwazo vingi na hasa kuwa mahakama zetu mara nyingi zinampatia haki mtu mwenye pesa, mwenye kuweza kutoa. Na tatizo jengine ni kuwa unapouza ardhi unanunua kitu chengine, hivyo akivunja mkataba huyo mnunuzi inakuwa shida kuweza kurudisha hela zake.

Nasaha zetu ni kuwa usiuze ardhi yako hiyo kwa mtu mwenye nia kama hiyo uliyosema.

Na Allah Anajua zaidi.

 

Share