Al-Lajnah Ad-Daaimah: Wanawake Kuvaa Nguo Fupi Mbele Ya Wanawake Wenzao Na Watoto

Wanawake Kuvaa Nguo Fupi Mbele Ya Wanawake Wenzao Na Watoto

 

Al-Lajnah Ad-Daa'imah

 

www.alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

Nini ambacho mwanamke anaruhusiwa kudhihirisha mbele ya wanawake wengine na mahram wake?

Yapi maoni yako kwa wayafanyayo wanawake wengi siku hizi, ambapo wao huvaa nguo fupi sana wakati wako pamoja na wanawake wengine na kunakuwa hakuna wanaume wengine? Baadhi ya nguo hizo huonyesha sehemu kubwa ya nyuma na tumbo, au wanavaa nguo hizo fupi mbele ya watoto wao nyumbani?

 

Jibu:

AlhamduliLlaah,

Kamati ya Kudumu (al-Lajnah al-Daa'imah) ya Utafiti wa Elimu na mas-ala ya Fatwa wana maelezo yafuatayo juu ya suala hili, ambayo inasomeka kama ifuatavyo:

Himdi zinamstahiki Allaah, Rabb wa walimwengu wote, na swalah na salaam ziwe juu ya Nabiy wetu Muhammad, na juu ya familia yake yote na Swahaba zake.

 

Waumini wanawake mwanzo wa Uislamu walikuwa safi sana, wenye hayaa na wenye aibu, jambo ambalo ilikuwa ni baraka ya imani kutoka kwa Allaah na Rasuli Wake, na walikuwa wakifuata Qur-aan na Sunnah. Wanawake katika kipindi hicho walikuwa na ada ya kuvaa nguo za kujisitiri, na haikujulikana kwamba walikuwa wakijifunua wanapokutana na mmoja au wanapokutana na mahram zao. Wanawake wa ummah huu wanatakiwa wafuate tabia hii nzuri - AlhamduliLLaah - kizazi baada ya kizazi mpaka hivi karibuni.

 

 

Lakini wakati uharibifu na fitnah zilipoingia kwa wanawake, njia ya mavazi yao na wanavyojiweka kwa sababu nyingi (inasikitisha sana kabisa), jambo ambalo hatuna nafasi ya kulijadili hapa.

 

Kwa sababu ya idadi kubwa ya maswali ambayo yametumwa kwenye Al-Lajnah Ad-Daaimah kuhusu wanawake kuangalia wanawake wenzao, na nini anachopaswa mwanamke kuvaa, Kamati inawaambia wanawake wote wa Kiislamu kwamba wanawake ni wajibu kwao kuwa na tabia ya kuwa na hayaa, jambo ambalo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alielezea kuwa ni sehemu ya Iymaan na moja ya matawi ya Iymaan.

 

 

Suala la hayaa ambalo ni amri iliyotolewa na Uislamu na kwa desturi ni kuwa wanawake wanapaswa wajisitiri, kuwa na hayaa, tabia na maadili ambayo yatawaweka mbali na kuanguka katika fitnah (majaribio) na hali ya utata.

 

 

Qur-aan inaonyesha wazi kuwa mwanamke hapaswi kuonyesha wanawake wengine chochote zaidi ya wanawake ambao ni Mahram wake, hali ambayo ni ya kawaida yeye kujifunua katika nyumba yake ni wakati wa kufanya kazi za nyumbani, kama jinsi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Anavyosema:

 

  وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا ۖ وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِهِنَّ ۖ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ أَبْنَائِهِنَّ أَوْ أَبْنَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي أَخَوَاتِهِنَّ أَوْ نِسَائِهِنَّ  

Na wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa kwa waume zao, au baba zao, au baba za waume wao, au wana wao wa kiume, au wana wa kiume wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kiume wa kaka zao, au wana wa kiume wa dada zao, au wanawake wao (wa Kiislamu) [An-Nuwr 24:31]

 

Ikiwa haya ndiyo maandiko ya Qur-aan na ndiyo latambulikana katika Sunnah, basi hili ndilo ambalo wake wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  na wanawake katika  Maswahaba  walivyokuwa wakifanya, na wanawake wa Ummah ambao waliwafuata kwa wema mpaka siku ya leo.

 

 

Jambo la kawaida la wanawake kujifunua ni wakati wao wako nyumbani na wakati wanafanya kazi za nyumbani, hali ambayo ni vigumu kujizuia, kama vile kujifunua kichwa, mikono, shingo na miguu.

 

Tukienda upande wa kuvuka mipaka katika kujifunua, hakuna dalili katika Qur-aan na Sunnah kwamba inajuzu. Hii pia ni njia inayoongoza kwa mwanamke kumjaribu au kujaribiwa kwa wanawake wengine, ambayo hufanyika kati yao. Pia inakuwa ni mfano mbaya kwa wanawake wengine, kama vile kuwaiga wanawake wa Kikafiri, makahaba na wanawake waovu jinsi wanavyovaa.

Imethibiti kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amesema:

 مَنْ تَشَبَّهَ بِقَوْمٍ فَهُوَ مِنْهُمْ

“Yeyote atakayeiga (jinafananisha) na watu basi atakuwa miongoni mwao.” [Imepokelewa na Imaam Ahmad na Abu Daawuwd. Katika Swahiyh Muslim (2077)]

 

Imesimuliwa kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amr kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alimuona amevaa nguo mbili za hariri, akasema:

 

“Haya ni katika mavazi ya makafiri, usiyavae.”

 

Pia imepokelewa katika Swahiyh Muslim (2128) Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allahu 'anhu): Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

“Aina mbili za watu wa motoni siwaoni; Watu ambao wana fimbo (mijeledi) kama mkia wa ng'ombe dume ambazo wanawapigia watu, na wanawake ambao wamevaa lakini wako uchi, wanawashawishi wanaume wawatongoze, na wanaelekea kwao (kwa kuwa warahisi). Vichwa vyao kama nundu za ngamia zinazoyumba (kwa mtindo wa nywele wanaosuka). Hawataingia Jannah wala hawatasikia harufu yake ingawa harufu yake inaweza kunuswa kutoka masafa kadhaa na kadhaa.”

 

Maana ya kauli hii “wamevaa lakini wako uchi” ni kwamba mwanamke amevaa nguo ambayo haijamsitiri, kwa hiyo amevaa, lakini kwa staili ambayo bado yuko uchi, kama vile wakati anavaa nguo nyembamba ambayo inaonyesha rangi ya ngozi yake, au vazi ambayo inaonyesha hali ya mwili wake, au vazi fupi ambalo haisitiri sehemu za viungo vyake.

 

Kwa hiyo, jambo ambalo wanawake wa Kiislamu wanapaswa kufanya ni kushikamana na uongofu waliokuwa wakifuata Mama wa Waumini (wake wa Nabiy) na wanawake katika Maswahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhunna), na wanawake wa ummah huu ambao wanawafuata hao kwa wema, na wajitahidi kujisitiri na kuwa na hayaa. Hili litawafanya kuwa mbali kuwasababishia fitnah na litawalinda na mambo yanayosababisha uchochezi wa tamaa na kuanguka katika zinaa.

 

Waislamu wanawake wanapaswa kujihadhari kuanguka katika mambo ambayo Allaah na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)   wamekataza, kama kuwaiga wanawake wa kikafiri na makahaba.

 

Wanatakiwa kumtii Allaah na Rasuli Wake, na kwa kutumai kupata malipo kwa Allaah (‘Azza wa Jalla), na kuwa na hofu ya adhabu Yake.

 

Kila Muislamu pia (mwanaume) anapaswa kumuogopa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kuhusiana na wanawake ambao wako chini ya ulinzi wake, na kutowaacha wakavaa mavazi ambayo Allaah na Rasuli Wake wameharamisha, kama vile nguo za kuvutia, au mavazi ambayo ni ya kudhihirisha maumbile na uchi, au yale ya majaribio (fitnah) ya kuwashawishi watu. Anapaswa kukumbuka (mwanaume) kuwa yeye ni mchungaji na ataulizwa kwa alichokichunga siku ya Qiyaamah.

 

Tunaomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Ayaweke mambo ya Waislamu yawe sawa, na Atuongoze sote kwenye njia iliyonyooka, kwa kuwa Yeye ni Mwenye kusikia, Aliye Karibu na Mwenye Kujibu du’aa.

 

Wa Swalla Allaahu ‘alaa Nabiyyinaa Muhammad wa ‘alaa aalihi wa Swahbihi wa sallam.

[Fataawa Al-Lajnah Ad-Daa'imah, (17/290)]

 

Pia imesemwa kwenye Fataawa al-Lajnah Ad-Daa'imah (17/297):

“Kile ambacho mwanamke anaruhusiwa kudhihirisha mbele ya watoto wake ni yale mambo ambayo kidesturi huwa wazi, kama vile uso, mikono, miguu, na kadhalika.”

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share