Nataka Kufundisha Bure Kwa Niya Ya Kupata Mchumba, Je, Inafaa?

 

 

 

SWALI:

Mimi ni mvulana wa miaka 24, ninasoma chuo kikuu DSM. Nimekwishafanya juhudi za kutafuta mchumba, nimekosa, na ninapenda bint aliyesoma mpaka walau form six. Sasa nimekusudia tukifunga chuo niende nyumbani kwa ajili ya likizo niwafundishe wanafunzi waislam bure (tution ya bure) nikiwa na malengo mawili: moja ni kusaidia waislam wapate elimu ili uislam uende mbele na nipate thawabu. Mbili ni kutafuta mchumba wa kuoa na si kuzini kutoka katika mabinti watakaokuwemo darasani kwangu. Je kufanya hivi ni uassi yaani dhambi na niache? Je nitapata thawabu kwa ile kufundisha bure kama swadaka ingawa nina malengo mawili? Naomba nijibiwe mapema.


 

JIBU:

Sifa zote njema anastahiki Allah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Salah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'Alayhi Wa Aalihi Wasallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'Anhum)  na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukran kwa swali lako na tunakutakia kila la kheri katika kupata mke ambaye atakuwa ni mwenye Dini na maadili mema pamoja ya kuwa atakuwa mtiifu kwako. Usikate tamaa katika hilo wala usifanye haraka sana kwani ukiwa una haraka utachagua haraka haraka ili mradi umetimiza lile lengo la kupata mke lakini awe si mke kama ulivyotazamia na hivyo kuwa na shida nyingi.

Shughuli hiyo ambayo unataka kuifanya ya kuwasaidia wanafunzi walio katika vidato vya chini ni jambo muhimu. Kwa hakika kufundisha ni amali ambayo inampatia mwenye kuitekeleza thawabu nyingi, kwani Mtume (Swalla Allaahu  'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, “Kutafufuta elimu ni faradhi kwa kila Muislamu” (Ibn Maajah kutoka kwa Anas). Na akasema tena: “Anapofariki mwanadamu amali zake zote hukatika isipokuwa kwa mambo matatu: Sadaka ya kuendelea, elimu yenye manufaa na mtoto mwema mwenye kumuombea dua (mzazi/wazazi anapofariki)” (Muslim kutoka kwa Abu Hurayrah).

Hili jambo la kusaidia wengine peke yake linaonyesha au kutuashiria ya kwamba huu Ummah bado uko hai na utaendelea kuwa hai mpaka Siku ya Kiyama. Hongera ndugu yetu kwa moyo wako huo.

Katika kupata thawabu kwa amali yoyote unayofanya ni lazima kuwe na masharti ambayo umetekeleza, moja wapo ikiwa ni Ikhlaasw, naye kufanya kitendo kwa ajili ya Allah (Subhaanahu wa Ta'ala). Hivyo, lengo kubwa mwanzo la wewe kusaidia katika tuition liwe ni kwa sababu ya Allah (Subhaanahu wa Ta'ala). Ukifanya hivyo utakuwa ni mwenye kuandikiwa thawabu kwa 'amali yako hiyo. Kisha pia jaribu unavyoweza kuweka mazingira ya sehemu ya kufundushia yawe yapo katika misingi na maadili ya Kiislamu. Jaribu hilo mwanzo kwa mfano wako binafsi, uwe wewe mwenyewe ni Muislamu wa kimatendo. Ikiwa sehemu ya tuition ni mchanganyiko basi pia jaribu kuona kuwa wanawake wapo nyuma na wanaume wako mbele na kusiwe na faragha baina yao ili kusitokee mambo ambayo ni mabaya.

 Katika hali hiyo ikiwa utapata msichana ambaye amekuridhisha kwa sura na tabia za nje basi jaribu kuwatumia dada zako au mama, shangazi na jamaa zako wa kike ili kumchunguza kwa wale wanaomjua kwa karibu. Usifanye haraka kwa kuvutiwa na sura peke yake. Ikiwa dini yake na tabia zake baada ya utafiti huo zimekuridhisha wazazi wako wanaweza kukupelekea posa rasmi na kisha kupanga siku ya harusi. Ukitumia njia hiyo hutakuwa na makosa yoyote.

Sijui hapo Chuo upo mda gani kwani kuna jamaa wengi ambao wamepata nusra hapo chuoni. Inaonyesha hujafanya home work vizuri kuhusu mas-ala hayo. Kabla ya kuondoka chuoni kwa ajili ya likizo unaweza kumuona amiri wa MSAUD na huenda wakakusaidia. Na unaporudi nyumbani pia unaweza kuzungumza na wazazi wako nao pia watakusaidia ili kutimiza Sunnah hiyo muhimu.

Kwa hivyo zipo njia nyingi ambazo hujazitumia katika kutafuta mchumba. Tunakuombea mara nyengine tena ili uweze kupata msichana ambaye ameshika Dini barabara.

 

Na Allah Anajua zaidi.

 

Share