Nasaha Kwa Wakimbizi Wanaoishi Kusema Hawajaoana Ili Wapate Ruzuku Ya Serikali

SWALI:

Assalaam 'Alaykum Warahmatullah,

Jazaka Allaahu Khaira kwa nakala hii ya suala ya ndugu yetu huyu pamoja na majibu yake.  kwa kweli ni tatizo sugu sana kwa wakaazi wa nchi hii Uk waliotokea nyumbani. Nilikuwa nina pendekezo la nyongeza ya suala hili, ili iwe kama ni muongozo kwa wale ambao wapo tayari kujibadilisha haidhuru hata kama watapata consequences.   

1- Jee wafanye nini kwa wanandoa waliodanganya kuwa hawajaoana na kugawana watoto akiwa huyu single mother, na yule single father kwa muda wote waliokaa nchi hii??  Nini ushauri wenu ili wajikwamue na uongo huu?? 

2- Jee kuna wasia gani kwa wale ambao wanaishi kwa kufanya kazi na kujitambulisha wazi kuwa wameoana na kuwa pamoja, ila njia aliokuja nayo katika nchi hii ilikuwa ni ya kutumia uongo (msomali wakati sie) ili apate ukaazi.  Baada ya kupata sheria ndipo alipooa nyumbani na kumleta mkewe kisheria.  Jee kuna jukumu lolote kwa mke huyo juu ya hayo?

Wassalaam Alaykum.

 


JIBU: 

 Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum)  na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Tunashukuru kwa dondoo zilizozalikana na jawabu la kuhusu swali lisemalo “Naiambia Serikali Sina Mume Ili Nipate Msaada Wa Pesa Na Nyumba, Inafaa?”.

Jibu lako la kipengele cha pili, tutaliweka chini kabisa ya maelezo yafuatayo.

Tunatumai kuwa maelezo haya yatakuwa ni ya faida kwa kila mmoja wetu hasa kwa wale wanaoishi katika nchi za Kimagharibi na wenye mpango wa kutaka kwenda kuishi huko kwa njia kama hizo. Kwa hakika suala hili ni zito na linagusa maisha ya ndugu na dada zetu wengi ambao kwa wakati mmoja au mwengine wameongopa ili kupata maslahi madogo ya kidunia. 

Huenda kwa wengine wametekeleza hayo kwa sababu ya ujinga na kutojua, wengine kwa sababu ya kufuata hawaa za nafsi zao, au rafiki aliyemghuri au kwa kujua lakini kutafuta maslahi ya hapa duniani.

Inataka tufahamu umbile la mwanaadamu aliloumbiwa nalo na Allaah Aliyetukuka. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anatueleza umbile hilo pale Aliposema:

“Na mwanaadamu ameumbwa dhaifu” ().

Ni kwa huu udhaifu ndio anasahau, anakosea, anaasi, anadhulumu, anamfuata shetani na mara nyengine hawaa na matamanio ya nafsi yake. Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema kuwa kila mwanaadamu ni mkosa lakini mbora kwa wale wenye kukosea ni wale wenye kutubia.

Ushauri wetu kwa ikhlaasw na nia safi ambao tunaweza kuwapatia ndugu zetu ni kuwa wafanye haraka kurekebisha makosa hayo yaliyofanyika kwa kujirudi kuhusu jambo hilo na kurudi kukaa kisheria pamoja na wake zao. Tukiwa tunanendelea kuishi katika hali hiyo na tunachuma haraam na kuishi kwa haraam, tutakuwa tunazidi kujichumia madhambi kila siku inayohesabiwa. Na inapasa Waislam wawe ni wenye kufanya kazi na kuacha ombaomba na kutegemea ruzuku kwa njia ya uongo na hali wana uwezo wa kufanya kazi na kujikimu kimaisha.

Pia tunawashauri wawe ni wenye kutoa sadaka kwa wingi ili Allaah Awafutie makosa yao. Kwai baada ya toba kwa mabaya yaliyofanyika, kinachofatia ni kutenda mema na mazuri mengi yatakayofuta yale mabaya yaliyotendeka nyuma. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam anasema: “…na ufuatilize jambo zuri kwa lile baya ulilolifanya, litalifuta” [At-Tirmidhiy] 

Kisha kunakuja tatizo la malezi ya watoto ambalo litaleta mushkeli mkubwa zaidi katika jamii ya Kiislamu katika mustakbali wa karibu. Na jukumu la malezi ni la baba na mama na ikiwa hawataweza kutekeleza mas-uliya hayo basi watasualiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala). Mifano mingi tunaiona katika jamii hizo ni kuwa mara kwa mara kwa maslahi hayo yanayopatikana kwa njia hizo za ulaghai, kumesababisha ndoa nyingi kuvunjika kwa sababu ya ugomvi kutokana na matumizi ya vipato hivyo vya uongo! Mwishowe watu wanatengana na baba kukosa watoto wake na huenda malezi yakaangukia kwa mama pekee ukawa mzigo mkubwa kwake na pia kuharibika ukuzwaji wa watoto wale kutokana na misingi isiyo imara. ‘Alaa kulli haal kuna madhara mengi ya kidunia vilevile achilia mbali ya kidini.

Ama kwa yule aliyemuoa mke akidai kuwa yeye ni Msomali au Taifa jengine lolote naye si hivyo, yeye ndiye atakayekuwa na makosa na wala si mkewe. Hivyo, atatakiwa mume huyo atake toba na msamaha kwa Allaah, na Allaah ni Mwingi wa Kusamehe Mwenye kurehemu. Na hapa chini tunatoa dalili ya kukubaliwa kwa toba za mja anaporudi kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa roho na nia safi kama tutakavyobaini. Pia ni jukumu la mke huyo kumshauri na kumkumbusha kila wakati mumewe kuhusu ubaya wa jambo hilo, madhara yake na umuhimu wa kurudi kwa Allaah na kufanya mema. Pia awe anamsisitiza kila wakati mumewe ku

Haya yote yaliyotangulia ni makosa na amali ya madhambi ambayo tayari imepita na ipo katika daftari yetu ya madhambi. Inabidi hivyo tujirudi kwa kutaka na kuomba msamaha kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala). Na katika kuweza kutekeleza hilo tusingoje kesho tuanze leo kwani kesho haina dhamana. Allaah Aliyetukuka Ana sifa ya kusamehe naye ni Mwingi wa kusamehe. Yeye Husamehe madhambi yote na wakati wote kwa yule mwenye kurudi Kwake. Hivyo, tufanye bidii kutaka msamaha kabla hatujachelewa. 

Na anapoomba mtu Tawbah ya kweli bila shaka Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Atamghufuria madhambi yake zote,

“Na hakika Mimi ni Mwingi wa Kusamehe kwa anayetubia, na akaamini, na akatenda mema, tena akaongoka (20: 82)

Wamesema wanavyuoni: “Toba ni wajibu kwa kila dhambi. Ikiwa dhambi aliyofanya mja ni baina mja na Allaah aliyetukuka haiingiliani na haki ya binadamu, itakuwa na sharti tatu: 

Ya kwanza: Kuacha maasiya.

Ya pili: Kujuta kwa kufanya hayo maasiya.

Ya tatu: Kuazimia kutorudia tena kosa lile milele. Likikosekana sharti moja katika hizi tatu basi toba haitosihi”.

Na ikiwa dhambi iliyofanywa ina mafungamano na mwanadamu sharti za kupata toba znakuwa ni nne: “Sharti hizi tatu zilizotajwa hapa juu na ya nne ni kuirudishia haki ya yule mtu, ikiwa ni mali au kitu chengine chochote umrudishie.

Ni wajibu kwa Muislamu kutubu (kuomba msamaha) kwa madhambi yote. Ikiwa atatubia baadhi ya dhambi husihi toba yake kwa dhambi ile na zinabaki zile zilizobakia. Zimedhihiri dalili katika Kitabu na Sunnah na Ijma’a ya Ummah katika uwajibu wa toba.  

Kwa wale ambao wamefanya makosa kwa ujinga na wakafahamu hilo wanatakiwa wafanye haraka kurudi kwa Allaah. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: “Toba inayopokelewa na Allaah ni ya wale wanaofanya uovu kwa ujinga, kisha wakatubia kwa upesi. Hao ndio Allaah huipokea toba yao. Na Allaah ni Mjuzi na Mwenye hikima” ().

Ujinga wa kitu haudumu hivyo anatambua mtu kuwa yeye alifanya kosa kwa ujinga anafaa arudi haraka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala).

Tufahamu ya kwamba toba haikubaliwi kwa mtu ambaye atangoja mpaka anafika karibu na kukata roho ndio anataka kurudi kwa Allaah. Toba ya mtu huyo haikubaliwi kabisa, kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anaema: “Hawana toba wale ambao hufanya maovu mpaka mauti yamemhudhuria mmoja wao, hapo akasema: “Hakika mimi sasa natubu’... Hao Tumewaandalia adhabu iumizayo” ().

Tusingoje mpaka utakapofika wakati huo. Tufanye hima katika safari ya kurudi kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa haraka iwezekanavyo.

Imepokewa kwa Imaam Ahmad kutoka kwa Abu Dharr (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakika mimi najua mtu wa mwisho ambaye atatolewa Motoni na mtu wa mwisho atakayeingia Peponi. Ataletwa mtu na ataambiwa: ‘Mwondoleeni madhambi yake makubwa na muulizeni kuhusu madhambi yake madogo’. Akasema: Ataambiwa: ‘Ulifanya kadha na kadha siku kadha na kadha, na ulifanya siku kadha, kadhaa na kadhaa’. Atasema: ‘Ndio’. Hataweza kukanusha chochote katika hayo. Ataambiwa: ‘Kwa kila dhambi ulilotenda, utakuwa na thawabu moja sasa’. Atasema: ‘Ewe Mola wangu Mlezi! Nimefanya vitu ambavyo sivioni hapa’. Akasema (Abu Dharr): ‘Hapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akatabasamu mpaka magego yake yakaonekana’ [Ahmad]”. Muslim pia ameipokea Hadiyth hiyo.

 

Amepokea Ibn Abi Haatim kutoka kwa Abu Jaabir kuwa amemsikia Makhuul akiHadiytha, akasema: “Alikuja mzee mkongwe, nyusi zake zikiwa zimeanguka kwenye macho yake, akasema: ‘Ewe Mtume wa Allaah! Mtu amewakhini wenziwe na amefanya uasherati, na hakuna jambo lolote baya isipokuwa amelifanya. Lau madhambi yake yatagawanywa kwa wote wa ardhini, wataangamia. Je, kuna toba yoyote kwake?’ Mtume wa Allaah (Swalla Llaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: ‘Je, umesilimu?’ Akasema: ‘Ama mimi nashuhudia kuwa hapana muabudiwa isipokuwa Allaah peke Yake hana mshirika naye, na kuwa Muhammad ni mja Wake na Mtume Wake’. Akasema Mtume (Swalla Llaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ‘Hakika Allaah Amekusamehe kwa yote uliyofanya mfano wa hayo, na Amekubadilishia maovu yako kuwa mema kwako’. Akasema: ‘Ewe Mtume wa Allaah! Na hata khiyana yangu na uzinzi wangu?’ Akasema: ‘Na khiyana yako na uzinzi wako uliofanya’. Mtu huyo aliondoka huku analeta Tahliyl (Laa ilaha illa Llahu) na Takbiyr (Allaahu Akbar)” [Ahmad].

 

Kisha akasema Aliyetukuka kutupa habari ya ujumla wa rehema Yake kwa waja wake, na kuwa yeyote atakayeleta toba Kwake Atamsamehe kwa dhambi yolote, kubwa au dogo. Akasema Aliyetukuka: “Na aliyetubu na akafanya mema, basi hakika huyo ametubu kweli kweli kwa Allaah”(25: 71).

Hii ina maana kuwa Allaah Aliyetukuka Anakubali toba yake, kama alivyosema Aliyetukuka: “Na anayetenda uovu au akajidhulumu nafsi yake, kisha akaomba maghfira kwa Allaah, atamkuta Allaah ni Mwingi wa maghfira, Mwenye kurehemu” (4: 110).

Na Akasema Aliyetukuka: “Je! Hawajui ya kwamba Allaah Anapokea toba ya waja Wake” (9: 104).

Na amesema Aliyetukuka: “Sema: Enyi waja Wangu mliojidhulumu nafsi zenu! Msikate tamaa na rehema ya Allaah” (39: 53), kwa yule mwenye kurudi na kutubu Kwake. 

Zipo ayah nyengine pamoja na Hadiyth za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambazo zinatufidisha kuwa Allaah ni Mpole, Mkarimu na Mwingi wa kusamehe. Hivyo, sisi hatufai kukata tamaa na rehema ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala). 

Kufaulu kwetu ni kurudi katika twaa ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala), kwani Yeye amesema: “Na tubuni nyote kwa Allaah, enyi Waumini ili mpate kufaulu” (24: 31).

Tufahamu ya kuwa toba inayokubaliwa ni ile ya kweli inayofanywa kwa ikhlasi, kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amesema: “Enyi Mlioamini! Tubuni kwa Allaah toba iliyo ya kweli; huenda Mola wenu Mlezi Akakufutieni maovu yenu na kukuingizeni katika Pepo zipitazo mito mbele yake” (66: 8).

 

Kwa umuhimu huu mkubwa wa kuleta maghfira, tunapata uongofu wa jinsi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyokuwa akifanya. Yeye alikuwa akileta maghfira (kwa kusema Astaghfirullah) kwa siku zaidi mara sabiini (Al-Bukhaariy na at-Tirmidhiy) na katika Hadiyth nyengine mara mia (Muslim na Abu Daawuud).

 

Na imepokewa na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Yeyote atakayetubu kabla ya jua kuchomoza kutoka upande wa magharibi Allaah humsamehe” (Muslim).

 

Na imepokewa Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakika ya Allaah Atiyetukuka hukubali toba ya mja maadamu roho haijafika kooni” (At-Tirmidhy na akasema kuwa hii ni Hadiyth Hasan (Nzuri). Hadiyth hii pia imepokewa na Ahmad, Ibn Maajah, na akaisahihisha Ibn Hibbaan na Al-Haakim. Ipo Hadiyth yenye maana sawa na Hadiyth hii kwa maana ambayo imepokelewa na Ahmad kutoka kwa Abu Dharr (Radhiya Allaahu ‘anhu) na akaisahihisha Ibn Hibbaan na al-Haakim na Hadiyth nyengine iliyopokelewa na Atw-Twabariy kutoka kwa Bashiyr bin Ka‘b (Radhiya Allaahu ‘anhu)).

 

Na katika Hadiyth ya Al-Bukhaariy na Muslim kutoka kwa Abu Sa‘iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaelezea kuhusu mtu aliyeua watu mia moja na aliporudi kutaka msamaha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na akasamehewa dhambi zake na kuingizwa Peponi. Na vile vile kisa cha Ka‘b ibn Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu) na wenzake wawili ambao hawakwenda katika Vita vya Taabuuk na jinsi walivyosamehewa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa kosa hilo pale walipoomba msamaha (Al-Bukhaariy na Muslim).

2- Jee wafanye nini kwa wanandoa waliodanganya kuwa hawajaoana na kugawana watoto akiwa huyu single mother, na yule single father kwa muda wote waliokaa nchi hii??  Nini ushauri wenu ili wajikwamue na uongo huu??

Suala hili linagusa sehemu mbili sehemu ya kwanza ni kudanganya katika mas-ala ya ukaazi ambalo tayari limeshafafanuliwa kwamba kutubu ndiyo suluhisho lake na kukithirisha amali njema.

Sehemu ya pili ya kudanganya kutooana na suluhisho lake ni kutubu na kuzitekeleza shurti zote za toba kwa vitendo – kuacha maasi yenyewe, kujutia kwa kuyatenda na kuazimia kutoyarudia tena.

Kwa sababu kilichowapelekea kuyafanya haya kama ilikuwa ni dharura kwa wakati huo basi dharura hii kwa sasa haipo imekwishaondoka na pia kuendelea kuishi katika mazingira haya kwa ajili tu ya kupata kipato cha haramu  wakati ushafanya haramu  basi unaiongeza haramu juu yake na huku unaendelea kuishi katika haramu na hivyo unachokila ni haramu, unachokivaa ni haramu, unachokitumia ni haramu. Kama Hadiyth ya Mtume ambayo imesimuliwa na Abu Hurayrah kuwa ‘‘Amesema Mtume wa Mwenyeezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) “Hakika Allaah ni Mzuri na hakubali ila vizuri, na kwamba Allaah Amewaamuru Waumini wafanye yale Aliyowaamuru Mitume kufanya, Amesema Allaah Aliyetukuka: {{Enyi Mitume! Kuleni vyilivyo halali na mtende mema}} Na Akasema Aliyetukuka: {{Enyi mlioamini kuleni vya halali Tulivyowaruzuku}} Kisha akataja (kisa cha yule) mtu aliyesafiri safari ndefu, kachafuka na kajaa mavumbi na huku anayanyua mikono yake mbinguni akisema "Ewe Mola! Ewe Mola! Nipe kadhaa, nikinge na kadhaa wakati chakula chake ni cha haramu, na kinywaji chake ni cha haramu, na kivazi chake ni cha haramu, na anashibishwa na haramu, je, vipi atajibiwa (du’aa zake?)’’ [Muslim]

Pia ni kudhulumu kwa kuchukua haki ambayo hustahiki kwa kitendo cha kudanganya. Haki hii itakwenda kuulizwa siku ya siku pia. Si miongoni mwa tabia za Muislam kudhulumu haki ya mtu mwengine hata ikiwa ni Kafiri au ni chombo cha kiserikali. Dini yetu inatufunza kumpa kila anaestahiki haki yake.

Athari zake ni nyingi kama:

1.  Kuwatukanisha wanawake wa Kiislam rasmi (official) kuwa wanazaa bila ya kuwa na waume, kwani kila wakienda DSS (Ustawi wa Jamii) huwa wanasema hawana waume, lakini kila mara huwa wanazaa au hata baada ya miaka miwili au mitatu.Wakati inaeleweka vyema kwamba kuzaa nje ya ndoa Kiislamu ni haramu.

2. Kuwadhalilisha wanawake wa Kiislam mbele ya makafiri kuwa wao ni malaya hata kama wanajidai kuwa hawatendi umalaya. Inayotukanwa hapa ni dini ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala). Na hivyo ni sawa na kuwa tuko tayari kuuza dini yetu kwa maslahi yetu binafsi na madogo ya kidunia.

3. Kubwa kuliko hayo ni kuutukanisha Uislam na kuwa kuzuizi cha wasiokuwa Waislamu kuingia katika Dini ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) kwani wengi hawana nafasi ya kusoma lakini wana nafasi ya kuona, hivyo da’awah ya vitendo hapa ndio inafanya kazi zaidi ya da’awah ya maneno au maandishi kuwa wanawake wa Kiislam huwa wanautukanisha Uislam kivitendo wakati wanapokwenda kuomba msaada wakidai kuwa hawana uwezo!.

Hivyo tunachomshauri  na kumnasihi ndugu yetu huyu kwamba madhara yake ni makubwa mno katika dini na hata dunia yetu kushinda hata “faida” zinazoonekana kupatikana kihali na mali na Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Anatuonya kwa ukali kuchunga nafsi zetu pamoja na familia zetu kama anavyosema katika Suuratu Tahriym, aayah ya 6:

{{Enyi mlioamini! Jilindeni (jiokoeni) nafsi zenu na ahli (familia) zenu na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe. Wanausimamia Malaika wakali, wenye nguvu, hawamuasi Allaah kwa Anayowaamrisha, na wanatenda wanayoamrishwa.}}

Hivyo tunawaasa kwa nia njema kabisa wahusika waliofanya janja hizi kwa kukusudia,au kwa bahati mbaya au kwa kutokuelewa kuamua haraka kubadilika na kwenda kuripoti kunakuhusika na kujitambulisha kwamba wanaishi pamoja na kama ni rizki mtoaji ni Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) ambae anaturuzuku  kwa namna tusiyoitazamia na bila ya kujijua wala kutarajia. Na hili si jambo zito kwa kila amuogopaye Allaah (Subhanahu Wa Ta’ala)

Sema ukweli na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atakutolea njia nyingine za riziki. Kwani Yeye Amesema:

"Na anayemcha Allaah Humtengezea njia ya kutokea. Na Humruzuku kwa njia asiyotazamia. Na anayemtegemea Allaah Yeye Humtosha. Hakika Allaah Anatimiza amri Yake. Allah Kajaalia kila kitu na kipimo chake" (65: 2-3).

Wa Allaahu A’alam

Share