Naruhusiwa Kuchanganya Mafuta Ya Diesel Na Mafuta Taa Ili Kuongeza Mauzo Na Kunyanyua Uchumi Wangu?

 

SWALI:

BISMILLAHI RAHMAAN RAHIIM,

SWALI LANGU NI KWAMBA.MIMI NI MFANYABIASHARA WA MAFUTA YAANI PETROL STATION.NA KATIKA MJI WANGU KUNA WAFANYABIASHARA WENGI WA AINA HII.HIVYO KUNA MVUTANO MKUBWA WA BIASHARA.NA ASILIMIA KUBWA YA WAFANYA BIASHARA HIZI HUZIENDELEZA BIASHARA ZAO KAMA IFUATAVYO:

1. HUNUNUA MAFUTA AINA YA DIESEL KUTOKA DEPOT KISHA KUYACHANGANYA NA MAFUTA YA TAA HIVYO HUPATA FAIDA KUBWA ZAIDI.

2. HUNUNUA MAFUTA KUTOKA KWENYE MAGARI YA MAFUTA YANAYOPAKIA DIESEL YANAYOSAFIRISHA KWENDA NJE YA NCHI (transit goods, HUCHUKUA KWA MADEREVA HAO MATHALANI LITA 2000 ZA DIESEL NA KISHA WAO HUWACHANGANYIA NA MAFUTA YA TAA LITA 2000 ILI KUFIDIA LITA 2000 ZA DIESEL.

NOTE: THAMANI YA DIESEL NI KUBWA ZAIDI KULIKO THAMANI YA MAFUTA YA TAA.

KWA MAANA HIO WAO HUWEZA KUTEREMSHA BEI CHINI ZAIDI NA HIVYO MIMI KUPOROMOKA MAUZO YANGU.

SWALI: JE VIPENGELE HIVYO 2 NI HALALI KUVITUMIA KISHERIA YA DINI NIFANYEJE ILI NIWEZE KUINUKA KIUCHUMI.

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu muuliza swali. Allaah Akuzidishie iymaan yako ya kutaka kujua haki na kujiepusha kufanya dhulma kwa binaadamu wenzako. Hivi ndivyo inavyopasa kwa kila mtu kuwa na tahadhari na ya kuchuma mali ya haraam kwani haitamfaa lolote bali ni kukosa radhi za Mola na malipo mabaya duniani na Akhera

 Hakika ni kuwa Uislamu umeweka nidhamu ya kila kitu ukiwepo muamala wa kibiashara baina ya wanaadamu. Nidhamu ya Kiislamu ya kibiashara ni ya uadilifu kwani haimdhulumu yeyote na dhuluma si katika sifa ya Uislamu wala Muislamu.

Wakati mmoja Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akipita sokoni na akafika kwenye muuzaji nafaka mmoja naye akatia mkono wake kwenye aina moja ya nafaka. Mkono ulipoingia ndani ulipata umajimaji. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuuliza mwenye duka: “Ni nini hii?” Akajibu:

Nilinyeshewa na mvua”. Akamwambia: “Kwa nini usiziweke hizi maji maji juu ili mteja apate kujua hali halisi ya bidhaa zako? Mwenye kutudanganya si katika sisi” (Muslim).

Kisha unamdhulumu mtu ambaye amekuja kununua diesel nawe yako si diesel bali ni mchanganyiko. Pia tufahamu kuwa mafuta ya taa hayakutengenezwa kwa ajili ya kutiwa kwenye gari. Kwa hiyo, kutiwa huko kunaiumiza gari ya mtu mwengine. Suala ni kuwa kama wewe ni mteja ungekubali kuuziwa bidhaa hiyo? Hakika ni kuwa hakuna mwanaadamu atakayekubali hilo. Ikiwa wewe hukubali kwanini unamfanyia mwenzio. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema:

Ole wao hao wapunjao!” (83: 1).

Kwa hiyo, ndugu yetu Uislamu umekukataza kufanya hivyo. Inatakiwa kwako ima uendelee kufanya biashara hiyo ya mafuta bila kughushi, au umwelezee mteja wako kuwa umechanganya diesel na mafuta ya taa au utafute biashara nyingine.

Tunakuombea kila la kheri na fanaka katika shughuli zako.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share