Muislam Na Mazingira Ya Kazi

 

SWALI:

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakut,

Mimi suala langu ni kuhusiana na mfumo mzima wa maisha ya kazi, Dini inatufundisha nini au katika kufanya haki ndani ya mazingira ya kazi, Kuanzia ngazi za Top Management mpaka mtu wa mwisho kabisa, Haki za Muajiri kwa Muajiriwa, na kinyume chake. (the whole concept of management in working environment)

Shukran na JazaakumuLLaH kheiyr

Ndugu yenu, 

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani kutoka kwetu kwa swali lako hilo. Hili ni swali zuri hasa ukitizama mazingira yetu, hasa vijana wa Kiislamu katika miji yetu ya Afrika Mashariki.

Kazi inamaanisha juhudi, bidii au uajiri uliofanywa kwa ajili ya mtu kupata kipato chake cha halali na kwenye mipaka ya maamrisho ya Allaah na kanuni. Muislamu anapofanya kazi ima ya kuajiriwa au ya kujiajiri mwenyewe huku akiwa na niya nzuri na ikhlasi, huwa anapata thawabu kwani kazi ni Ibaadah.

Katika Uislamu dunia ni shamba la kujitayarisha kwa Akhera, Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema: “Na utafute kwa yale aliyokupa Allaah – makazi mazuri ya Akhera, wala usisahau sehemu yako ya dunia” (28: 77).

Na Anasema tena: “Na Tukaufanya mchana wa kutafuta maisha” (78: 11).

Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) hasa Ameuweka mchana na mwangaza wake ili watu waweze kujishughulisha katika kutafuta riziki kwa kufanya kazi.

Katika kupata fadhila hizo Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Ametufundisha du’aa ambayo pia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiiomba sana. Anasema Aliyetukuka: “Na kuna baadhi ya watu wanaosema: ‘Mola wetu! Tupe katika dunia; nao katika Akhera hawana sehemu yoyote. Na miongoni mwao wapo wasemao: ‘Mola wetu! Tupe mema duniani na mema Akhera, na utulinde na adhabu ya Moto” (2: 200 – 201).

Katika muono wa Kiislam, waumini wa kweli ni wale wenye kutenda amali, ambao sifa yao ya kipekee ni kwamba mambo yao ya kidunia na kazi zao haziwafanyi wao kusahau wajibu wao kwa Muumba wao. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema: “Watu ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi (wala kuwasahaulisha) kumkumbuka Allaah, na kusimamisha Swalah, na kutoa Zakaah; wanaiogopa siku ambayo nyoyo zitadahadari na macho kukodoka” (24: 37).

Muislam mwema na mzuri ni yule ambaye baada Ibaadah kubwa kama Swalah anakwenda kujishughulisha kutafuta fadhila za Allaah kwa kufanya kazi. Anasema Aliyetukuka: “Na itakapokwisha Swalah, tawanyikeni katika ardhi mtafute fadhila za Allaah, na mkumbukeni Allaah kwa wingi, ili mpate kufaulu” (62: 10).

Hakika Uislamu katika eneo letu tunaloishi (Afrika Mashariki) ni sawa na uvivu na Waislamu wanachukuliwa kama watu goigoi wasioweza kufanya kazi yoyote ile. Vijana wenye miili ya afya iliyojenga wanakaa mitaani katika mabaraza wakipiga soga.

Hairuhusiwi kwa Muislamu kutokufanya kazi kwa kisingizio cha kufanya Ibaadah au kumtegemea Allaah. Pia hairuhusiwi kwake yeye kutegemea sadaka tu ikiwa ana uwezo wa kufanya kazi na juhudi katika hilo. Katika hili, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Sadaka si halali kwa tajiri wala aliye na mwili mzuri (uwezo na afya)” (at-Tirmidhiy). Katika riwaya ya Abu Daawuud na an-Nasaa’iy, ‘Ubaydullah bin ‘Adiyy al-Khiyaar (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesimulia: “Watu wawili waliniambia kuwa walikwenda kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati wa Hijjah ya Kuaga alipokuwa anagawa sadaka. Walimuomba usaidizi. Aliwaangalia kuanzia juu (kichwani mpaka chini miguuni) na kuwapata wao wamejengeka na wenye nguvu. Kisha akawaambia: ‘Mukitaka, nitawapatia, lakini hakuna Zakaah kwa aliye tajiri wala yule mwenye nguvu anayeweza kuchuma (kwa kufanya kazi)”.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwakataza Waislamu kuomba bila ya haja wala dharura yoyote kwani kufanya hivyo ni kujivua heshima na hadhi. Hii ilikuwa ni kuwatayarisha na kuwahimiza Waislamu walinde heshima na hadhi, kukuza kujitegemea na kujiondoa katika kuwategemea wengine na kuwa kupe.

Uislamu, njia kamili ya maisha haikuacha jambo lolote isipokuwa limewafundisha wanaadamu wawe ni wenye kushikilia ili wapate kunali saada hapa duniani na kesho Akhera. Miongoni mwayo ni mas-ala ya mazingira ya kazi na haki ya kila mmoja kazini, yaani haki ya muajiri na muajiriwa. Ili kila mmoja acheze dauru yake ni lazima kila mmoja ajifunge kibwebwe ili ajipambe na sifa za mfanyakazi mzuri na muajiri mzuri. Ikiwa jambo hilo halitapatikana basi itakuwa ni kuendeshana mbio tu.

Mfanyakazi mzuri Muislamu anafaa awe na sifa zifuatazo:

 

1.     Mwenye ujuzi na elimu ya kazi yake: Nabii Yuusuf (‘Aayhis Salaam) kupewa kazi Misri ilikuwa ni kwa sababu ya uzoefu wake. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema: “Yuusuf akasema: Nifanye mtazamaji wa hazina za nchi; hakika mimi ni mlinzi mzuri na mjuzi hodari” ().

 

2.       Uaminifu na nguvu: Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anatueleza pendekezo lililotolewa na mmoja wa mabinti ya mzee (baba yao) kwa sifa za Nabii Muusa (‘Aayhis Salaam): “Akasema mmoja wa wale wawili: ‘Ewe baba yangu! Mkodi huyu. Bila shaka mbora wa kuajiriwa ni yule mwenye nguvu, mwaminifu” (28: 26).

 

3.     Mwenye kutunza vyema vitu na vifaa vilivyo chini ya uangalizi wake: Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema yafuatayo kuhusu Nabii Yuusuf (‘Aayhis Salaam): “Yuusuf akasema: Nifanye mtazamaji wa hazina za nchi; hakika mimi ni mlinzi mzuri na mjuzi hodari” ().

 

4.     Mwenye bidii: Kipato anachopata mtu kwa kazi ya mkono wake ndio bora kabisa kwa Muislamu. Imesimuliwa na Rafi‘ bin Khadij (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa ni shughuli gani iliyo bora, naye akajibu: “Mtu kufanya kazi na mikono yake na kila biashara iliyoruhusiwa” (Ahmad na at-Tirmidhiy).

 

 

5.       Kufika mapema kazini.

 

6.      Mkweli na uaminifu: Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mfanya biashara muaminifu atakuwa pamoja na Manabii, wakweli na mashahidi” (at-Tirmidhiy na al-Haakim).

Ama sifa ya muajiri mwema ni kama zifuatazo:

Muajiri Muislamu anafaa kuwa ni mwenye kuzingatia hisia za mwenziwe (mwajiriwa), hivyo hafai kumtwika mzigo asiouweza. Tazama jinsi gani mzee mcha Mungu alivyomuambia Nabii Muusa (‘Alayhis Salaam): “Akasema: ‘Mimi nataka nikuoze mmojawapo katika binti zangu hawa wawili kwa kunitumikia miaka minane; na kama ukitimiza kumi ni hiari yako, lakini mimi sitaki kukutaabisha: utanikuta InshaAllaah miongoni mwa watu wema” (28: 27).

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema yafuatayo kuhusu hili kama ilivyonukuliwa na Safwaan kutoka kwa Maswahaba wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka kwa masimulizi ya baba zao ambao walikuwa ni jamaa moja. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Tahadhari, yeyote atakaye mdhulumu majiriwa, au akampunguzia haki zake, au akamlazimisha kufanya kazi asiyoiweza, au akachukua kitu kutoka kwake bila idhini yake, nitamtetea Siku ya Qiyaama” (Abu Daawuud).

Mwajiri hafai kumtwika mzigo asiouweza hata akiwa ni mtumwa kwa kumpatia kazi juu ya uwezo wake, mwajiriwa ni zaidi. Amesimulia Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ni muhimu kumlisha mtumwa, kumvisha sawa sawa na kutomfanyisha kazi juu ya uwezo na nguvu zake” (Muslim).

Riwaya ya Imaam Maalik inasema, Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amehadithia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mtumwa anapatiwa chakula na kivazi kama ada, naye anafaa tu kufanya ile kazi anayoweza”. Maalik amehadithia kuwa ‘Umar bin al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akienda vijijini kila siku ya Jumamosi. Akimkuta mtumwa anafanya kazi asiyoweza alikuwa akimpunguzia.

Mwajiriwa anafaa alipwe mshahara wake pindi anapomaliza kazi au mwisho wa wiki au mwezi. Katika hili Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amehadithia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hapana, mfanyakazi alipwe kikamilifu pale tu atakapomaliza kazi yake” (Ahmad na at-Tirmidhiy).

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anamchukia na Atakuwa dhidi ya mwajiri ambaye halipi ujira au mshahara wa waajiriwa. Amesimulia Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

Allaah Anasema, ‘Nitakuwa dhidi ya watu watatu Siku ya Qiyaama:

-             Yule mwenye kuweka ahadi kwa jina Langu, lakini akafanya hiyana.

-             Mwenye kumuuza mtu huru (kama mtumwa) kisha akala thamani yake.

-             Yule mwenye kumwajiri kibarua ambaye anafanya kazi kwa ukamilifu  wake lakini hamlipi (ujira wake)” (al-Bukhaariy).

 

Hizi ni baadhi ya sifa za mwajiriwa na mwajiri ambazo kwayo unapata haki ya kila mmoja bila kumpunja mwenziwe.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share